read

Aya 57 – 62: Tena Sifa Za Waumini

Maana

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja wale wanaoishi kwenye mghafala wa upotevu, huku wenyewe wakiona kuwa wanaharakishiwa kheri, sasa anawataja waumini, kwamba ni wale wanaosifika na mambo yafuatayo:

1. Hakika wale ambao humwogopa Mola wao wanamnyenyekea.

Unaweza kuuliza kuwa kunyenyenyekea pia ni kuogopa, sasa itakuwaje wao wawe 'wanaogopa kuogopa'?

Jibu: Makusudio ya kunyenyekea hapa ni kupupia kumtii Mwenyezi Mungu. Makadirio ya maneno ni, wao wanapupia kumtii Mwenyezi Mungu kwa kuhofia adhabu yake.

2. Na wale ambao wanaamini ishara za Mola wao.

Yaani wanaamini dalili za kuweko Mungu na ukuu wake, utume wa Mitume yake na ukweli wa vitabu vyake.

3. Na wale ambao hawamshirikishi Mola wao.

Unaweza kuuliza: Wale ambao wanaziamini ishara zake bila shaka hawawezi kumshirikisha, sasa kuna haja gani ya kurudia maneno? Razi amejibu kuwa makusudio ya shirki hapa ni ile shirki iliyojificha; kama vile ria na kukosa ikhlasi katika matendo. Makusudio ya imani katika Aya iliyotangulia ni kule kuamini tu.

4. Na wale ambao wanatoa walichopewa na hali nyoyo zao zinaogopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao.

Wanatoa katika vile alivyowapa Mwenyezi Mungu na kutekeleza haki yake na haki za watu kwa ukamilifu, lakini pamoja na hayo wanahofia kuwa Mwenyezi Mungu hatawatakabalia.

Hao ndio wanaokimbilia kwenye kheri na ndio watakaotangulia kuzifikia.

Yaani wale ambao wametimiza masharti haya yaliyotajwa ndio wanaoharakia twaa ya Mwenyezi Mungu na wala hawangojingoji. Kwa ajili hiyo basi wao watawatangulia watu kuingia peponi kesho.

Na hatuikalifishi nafsi ila kwa uwezo wake.

Kwa sababu kukalifisha lisilowezekana ni dhulma, na Mwenyezi Mungu ambaye ameikataza dhulma hawezi kuifanya.

Na tuna kitabu kisemacho kweli.

Kinasajili dogo na kubwa na Mwenyezi Mungu atalipa kwacho; ikiwa ni kheri basi ni kheri na ikiwa ni shari basi ni shari.

Nao hawatadhulumiwa kwa kupunguziwa thawabu mwenye kufanya wema wala kuzidishiwa adhabu mwenye kufanya uovu.

بَلْ قُلُوبُهُمْ فِي غَمْرَةٍ مِنْ هَٰذَا وَلَهُمْ أَعْمَالٌ مِنْ دُونِ ذَٰلِكَ هُمْ لَهَا عَامِلُونَ {63}

Bali nyoyo zao zimo ujingani na haya na wana vitendo vingine wanavyovitenda.

حَتَّىٰ إِذَا أَخَذْنَا مُتْرَفِيهِمْ بِالْعَذَابِ إِذَا هُمْ يَجْأَرُونَ {64}

Mpaka tutakapowatia katika adhabu wale waliodekezwa na starehe kati yao, hapo ndipo watakapoyayatika.

لَا تَجْأَرُوا الْيَوْمَ ۖ إِنَّكُمْ مِنَّا لَا تُنْصَرُونَ {65}

Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi.

قَدْ كَانَتْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَكُنْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ تَنْكِصُونَ {66}

Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa nanyi mkirudi nyuma juu ya visigino vyenu.

مُسْتَكْبِرِينَ بِهِ سَامِرًا تَهْجُرُونَ {67}

Na huku mkiifanyia kiburi na mkiizungumza usiku kwa dharau.

أَفَلَمْ يَدَّبَّرُوا الْقَوْلَ أَمْ جَاءَهُمْ مَا لَمْ يَأْتِ آبَاءَهُمُ الْأَوَّلِينَ {68}

Je, hawakuifikiri kauli au yamewafikia yasiyowafikia baba zao wa zamani?

أَمْ لَمْ يَعْرِفُوا رَسُولَهُمْ فَهُمْ لَهُ مُنْكِرُونَ {69}

Au hawakumjua Mtume wao ndio maana wanamkataa?

أَمْ يَقُولُونَ بِهِ جِنَّةٌ ۚ بَلْ جَاءَهُمْ بِالْحَقِّ وَأَكْثَرُهُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ {70}

Au wanasema ana wazimu? Bali amewajia na haki na wengi wao wanaichukia haki.

وَلَوِ اتَّبَعَ الْحَقُّ أَهْوَاءَهُمْ لَفَسَدَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ وَمَنْ فِيهِنَّ ۚ بَلْ أَتَيْنَاهُمْ بِذِكْرِهِمْ فَهُمْ عَنْ ذِكْرِهِمْ مُعْرِضُونَ {71}

Na lau haki ingelifuata matamanio yao basi zingeliharibika mbingu na ardhi na waliomo ndani yake. Bali tumewaletea utajo wao na wanajitenga mbali na utajo wao.

أَمْ تَسْأَلُهُمْ خَرْجًا فَخَرَاجُ رَبِّكَ خَيْرٌ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ {72}

Au unawaomba ujira? Lakini ujira wa Mola wako ni bora na Yeye ndio mbora wa wanaoruzuku.