read

Aya 81 – 90: Walisema Kama Walivyosema Wa Mwanzo

Maana

Bali walisema kama walivyosema wa mwanzo.

Waliosema ni washirikina waliokuwa zama za Mtume (s.a.w.). Walikanusha ufufuo, wakatoa sababu mbili: Kwanza ni kustaajabu walikokuleta kwa ibara hii:

Je, tukishakufa tukawa mchanga na mifupa ndio tutafufuliwa?

Pili, kwamba wao hawajamuona aliyekufa kisha akarudi kuwa hai. Maana haya yamekusudiwa katika kauli yao:

Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni vigano vya wa kale.

Yaani tumeyasikia kabla yako ewe Muhammad, pia tuliyasikia kwa wazee wetu, lakini hakujatokea athari yoyote. Ni nani aliyekufa kisha akarudi kutoa habari?

Lau wangelitaamali uumbaji wa kwanza wasingelipinga uumbaji wa pili. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:5) na Juz. 15 (17:49).

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewajadili wapinzani hawa, kwa mfumo wa kielimu wenye hekima, katika Aya tatu zifuatazo:-

1. Sema, ni ya nani ardhi na vilivyomo ndani yake, kama nyinyi mnajua?
Alimwamrisha Mtume wake kuwakabili na swali hili. Kwa sababu wao wanakiri na kukubali kwamba Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa ulimwengu, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Watasema, ni vya Mwenyezi Mungu.

Yaani ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi Mungu; wala hakuna maana ya kuwa ni vyake ila ni kwakuwa ameviumba na kuvianzisha. Ikiwa Mwenyezi Mungu ni muweza wa kuumba ardhi basi vilevile Yeye anaweza kufufua wafu.

Basi je, hamkumbuki na kufikiria hakika hii ambayo ni aliyeweza kuanzisha mara ya kwanza pia anaweza kurudisha mara ya pili? Kila anayeweza kitu, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, anashindwa na vingine, anajua vichache na hajui vingi. Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ni Muweza na Mjuzi wa kila kitu.

2. Sema, ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa arshi tukufu? Watasema, ni vya Mwenyezi Mungu.

Arshi ni kinaya cha ufalme wake Mwenyezi Mungu Mtukufu na utawala wake. Ambaye mbingu na ardhi ni yake basi ni wepesi kwake kumrudisha aliyekufa humo.

Sema, basi je, hamuogopi ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake?

Tumezungumzia kuhusu mbingu saba katika Aya 17 ya sura hii

3. Sema, ni nani mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu?

Makusudio ya ufalme wa kila kitu ni kuwa kila kitu kinamnyenyekea na kumhitajia Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba hahitajii chochote.

Na yeye ni mlinzi wala hapalindwi kwake, kama mnajua.

Yeye ni rehema kwa mwenye kutaka rehema na ni uokovu kwa anayetaka kuokoka; wala hapana mwenye kuweza kumrehemu au kumuokoa yule ambaye anastahiki ghadhabu na adhabu yake.

Watasema, ni wa Mwenyezi Mungu.

Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake.

Sema, basi vipi mnadanganyika?

Maadamu mnakubali hayo, basi vipi mnaukana ufufuo na kuhadika na haki?

Bali tumewaletea haki.

Hapana! Hawakudanganyika na haki wala hawakutatizika na batili, baada ya kuwasimamia hoja na dalili zilizo wazi. Na kwa hakika wao ni waongo. Hawakuhadaika isipokuwa wamejitia kuhadaika na kudhihirisha uongo na uzushi. Wao hawakutosheka na ufufuo kwa hoja kwamba dalili zake zimejificha.

Unaweza kuuliza: Imejulikana vipi kwamba wao walikana ufufuo wakiwa na imani nao, na kuna Aya nyingi zimeonyesha mshangao wao na kutojua kwao kukisia uumbaji wa kwanza na ufufuo?

Jibu: Ndio ni kweli, lakini kila ambaye amepatiwa hoja za kutosha zilizo wazi na akaendelea kukataa, ni sawa na yule anayekataa makusudi.

مَا اتَّخَذَ اللَّهُ مِنْ وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَٰهٍ ۚ إِذًا لَذَهَبَ كُلُّ إِلَٰهٍ بِمَا خَلَقَ وَلَعَلَا بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ سُبْحَانَ اللَّهِ عَمَّا يَصِفُونَ {91}

Mwenyezi Mungu hakujifanyia mwana, wala hanaye mungu mwingine. Ingelikuwa hivyo basi kila Mungu angelichukua alivyoviumba. Na baadhi yao wangeliwashinda wengine. Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu.

عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ {92}

Mjuzi wa ghaibu na dhahiri. Ametukuka juu ya hayo wanayomshirikisha nayo.

قُلْ رَبِّ إِمَّا تُرِيَنِّي مَا يُوعَدُونَ {93}

Sema, Mola wangu! Ukinionyesha waliyoahidiwa.

رَبِّ فَلَا تَجْعَلْنِي فِي الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ {94}

Mola wangu usinijaalie katika watu madhalimu.

وَإِنَّا عَلَىٰ أَنْ نُرِيَكَ مَا نَعِدُهُمْ لَقَادِرُونَ {95}

Na hakika sisi ni wenye kuweza kukuonyesha tuliyowaahidi

ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ السَّيِّئَةَ ۚ نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَصِفُونَ {96}

Kinga maovu kwa yaliyo mema zaidi. Sisi tunayajua wanayoyasifia.

وَقُلْ رَبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ {97}

Na sema, Mola wangu! Najikinga kwako na wasiwasi wa shetani.

وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَنْ يَحْضُرُونِ {98}

Na ninajilinda kwako wasinikaribie.

حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ {99}

Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu nirudishe.

لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ ۚ كَلَّا ۚ إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا ۖ وَمِنْ وَرَائِهِمْ بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ {100}

Ili nitende mema badala ya yale niliyoyaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kuna kizuizi mpaka siku watakapofufuliwa.