read

Aya 112 – 118: Mlikaa Muda Gani Katika Ardhi

Maana

Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa idadi ya miaka?

Atakayesema ni Mwenyezi Mungu au malaika atakayeamriwa kuuliza kesho, wanaombiwa ni wale waliokana ufufuo na muda wanoulizwa ni ule walioumaliza katika kufuru duniani. Lengo la swali hili ni kuwasuta na kuwatahayariza kutokana na kuipinga kwao siku hiyo na kuwakejeli wale waliokuwa wakiwaonya na vituko vya siku hiyo na adhabu yake.

Watasema: tumekaa siku moja au sehemu ya siku, basi waulize wanaoweka hisabu.

Wapi sisi na swali hili? Tuliyonayo yanatutosha. Ikiwa hakuna budi na kujibu basi tumekaa masaa tu. Wanaojua zaidi ni wale waliokuwa wakiudhibiti umri wetu na matendo yetu ambao hawaachi dogo wala kubwa, lakini sisi hatuna tujualo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:103).

Atasema: Hamkukaa ila kidogo, laiti mngelikuwa mnajua.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawaambia mmekaa miaka, sio siku moja kama mnavyosema, lakini miaka ni michache kwa vile inaisha, na kila chenye kuisha ni kichache hata kama kitakaa muda mrefu. Laiti mngelijua hakika hii mlipokuwa duniani, mkaiamini siku hii na mkajiandaa nayo, basi leo mngelikuwa kwenye amani na salama, lakini mlikufuru, ikawathibitia adhabu.

Je, mnadhani kuwa tuliwaumba bure na kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?

Kwa dhahiri maneno yanaelekezwa kwa wale wanaokana ufufuo, lakini kwa uhalisi yanaelekezwa kwa kila muasi na mfisadi; ni sawa awe amepinga ufufuo tangu mwanzo au aliuamini na asiufanyie kazi.

Bure ni kisicho na faida wala hekima ya kuwako kwake. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameepukana na kufanya mambo bure.

Lau mtu asingefufuliwa baada ya mauti, akajulikana mwema na muovu na kulipwa kila mmoja anavyostahiki, ingelikuwa kuumbwa mtu ni bure tu kusiko na faida yoyote.

Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki.

Mfalme ina maana ya muweza mwenye nguvu. Na haki inaondoa batili na bure. Ikiwa haki ndio iliomuumba mtu, itakuwaje kumbwa kwake kuwe bure? Au vipi imuwache bure bila ya taklifa yoyote na hisabu au bila ya swali na jawabu la wema au uovu alioufanya?

Hapana mungu ila Yeye, Mola wa Arshi tukufu.

Yeye ni mmoja katika ufalme wa ulimwengu bila ya mshirika katika kuumba kwake, kupangilia kwake, elimu yake na hekima yake. Basi kuumbwa mtu na asiyekuwa mtu burebure na ufisadi utatoka wapi?

Na anayemuomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwingine, hana dalili ya hilo.

Ataitoa wapi dalili ya ushirika na kila kitu kinafahamisha kuwa Mungu ni mmoja. Inatosha kuwa ni dalili ya umoja wake nidhamu ya ulimwengu huu ambayo haina kombo wala kuharibika, hakuna anayeweza kupinga hakika hii isipokuwa yule anayepinga misingi ya dhahiri na akakataa dalili zote. Mfano wa mtu huyu ni ni kupuuzwa wala hajadiliwi.

Basi hakika hisabu yake iko kwa Mola wake, naye ndiye atakayemlipa anayostahiki.

Kwa hakika makafiri hawafanikiwi, kwa sababu wameiacha njia.

Kama alivyoifungua Mwenyezi Mungu (s.w.t.) sura hii kwa kusema: "Hakika wamefaulu waumini." basi anaiishilizia hivyo hivyo.

Na sema: Mola wangu! Ghufiria na rehemu nawe ni Mbora wa wanaorehemu.

Yeye peke yake ndiye anayeombwa kutukunjulia kwa rehema zake na maghufira yake, wala asikate matarajio yetu ya kuneemeshwa na neema zake na ukarimu wake, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, rehema za Mwenyezi Mungu zimshukie yeye na kila mwenye kufuata mwenendo wake.