read

Aya 1 – 5: Hukumu Ya Mzinifu Na Mwenye Kutusi

Maana

Ni Sura tuliyoiteremsha na tukailazimisha na tukateremsha ndani yake Aya zilizo wazi.

Mwenyezi Mungu alimtereshia Mtume wake mtukufu sura hii, ndani yake mkiwa na mafunzo aliyowajibisha kuyatumia kila mukallaf. Kwa sababu yanalenga kujenga jamii ya binadamu kwa ukamilifu kwa manufaa yake na maendeleo yake.

Mafunzo haya yako waziwazi yasiyohitajia ubishi wala mjadala katika malengo yake ya kumlinda mtu na ufisadi na upotevu. Kwa ajili hii au nyingine ndio ikaitwa Sura ya nuru. Na Qur'an yote ni uongofu na nuru.

Ili mkumbuke.

Mwenyezi Mungu ameteremsha Sura hii iliyo wazi wazi ili mjue na muitumie.

Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume mtandikeni kila mmoja wao viboko mia.

Maneno yanaelekezwa kwa yule atakayetekeleza adhabu (hadd), ambaye ni Imam au naibu wake mwenye ujuzi na mwadilifu.

Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa mwenye kuzini atapigwa vibogo awe muhsan au asiyekuwa muhsan. Kwa sababu herufi lam ya jinsiya ikiingia katika nomino pekee, inafahamisha kuenea aina zote.

Muhsan ni yule aliye baleghe na akili timamu akiwa na mke anayemtosheleza wakati wowote akitaka kumjamii. Ikiwa atajamii akiwa ni mtoto au mwenda wazimu, au akiwa ni mseja au ana mke, lakini yuko mbali naye au yuko karibu naye lakini ana maradhi ya kushindwa kumjamii, basi huyo siye muhsan. Vile vile mwanamke.

Imam Abu Jafar Swadiq (a.s.) aliulizwa kuhusu muhsan, akasema: ambaye ana tupu anayoweza kuiendea basi huyo ni muhsan.

Hivi ndivyo ilivyofahamisha dhahiri ya Aya, kwamba mzinifu muhasn na asiyekuwa muhsan watandikwe viboko mia. Lakini imethibiti kwa Hadith mutawatir na kongamano la madhehbu zote za kiislamu kwamba hukumu ya muhsan ni kupigwa mpaka kufa. Kwa hiyo hukumu ya viboko ni ya asiyekuwa muhsan.

Bali imekuja Hadith katika Sahih Bukhari kwamba Umar bin Al-khattwab alisema: "Hakika Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad kwa haki na akamteremshia Kitabu kwa haki, katika aliyoyateremsha ni Aya ya kurujumu (kupiga mawe) tukaisoma na tukaitia akilini na tukaihifadhi."

Rejea Bukhari Juz. 8 Uk. 209 chapa ya kiarabu ya mwaka 1377 A.H. Na Muslim Juz. 2, sehemu ya kwanza Uk. 107 chapa ya kiarabu ya mwaka 1348 A.H. Katika riwaya nyingine ya Bukhari Juz. 9 Uk. 86, Umar alisema: "Lau si kuwa watu watasema Umar amezidisha katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, ningeliiandika kwa mkono wangu Aya ya kurujumu."

Unaweza kuuliza Mwenyezi Mungu mahali pengine anasema: " Juz. 4 (15:4). Katika Aya hii Mwenyezi Mungu amewajibisha mzinifu mwanamke afungiwe nyumbani wala asitoke mpaka afe au Mwenyezi Mungu amjaalie njia nyingine; kisha katika Aya tuliyo nayo Mwenyezi Mungu amewajibisha viboko. Sasa kuna njia gani ya kuchanganya Aya mbili hizi?

Jibu: Kwenye Juz.4 tulisema kwamba makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu au 'awajaalie njia' ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu hakujaalia adhabu ya kufungiwa nyumbani ni ya daima, bali ni kwa muda fulani, kisha alete hukumu ya kudumu. Ndivyo ilivyokuwa, ambapo iliondolewa adhabu ya kufungwa nyumbani na mahali pake pakachukuliwa na adhabu ya viboko au kurujumiwa.

Baadhi ya ulama wanasema kuwa hatuwezi kukimbilia kufutwa hukumu mpaka kupatikane nukuu ya kufuta hukumu hiyo au iwe haiwezekani kutumia nukuu mbili. Inavyochukuliwa ni kuwa sharia haikuleta nukuu ya kufuta hukumu hiyo na kwamba kuzichanganya nukuu mbili ni jambo lisilo na uzito, basi inafaa kuzitumia Aya zote mbili, kwamba mzinifu apigwe viboko na pia afungiwe nyumbani vile vile.

Sisi tunaweza kukubaliana na anayesema hivi ikiwa atatukinaisha kuwa makusudio ya 'njia' ni kitu kingine kisichokuwa hukumu ya kudumu ambayo ndiyo inayofahamika mwanzo. Ama kufasiri njia kwa maana ya ndoa, kama alivyosema mwenye fikra hii, hiyo iko mbali na ufahamu.

Wala isiwashike huruma kwa ajili yao katika dini ya Mwenyezi Mungu.

Msicheleweshe hukumu ya mzinifu mwanamume na mzinifu mwanamke, bali mutekeleze wala isiwazuie huruma. Kwa sababu hakuna kuhurumiana katika dini ya Mwenyezi Mungu. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: "Lau Fatima ataiba nitamkata mkono wake." Katika Nahjul-bal- agha, imeelezwa: "Mwenyezi Mungu amefaradhisha kisasi kuhifadhi damu na ameweka adhabu kuheshimu miko."

Ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Huu ni msisitizo na himizo la kutekeleza adhabu na kwamba kuipuuza ni kudharau dini.

Na lishuhudie adhabu yao kundi la waumini.

Lengo la hilo ni kuenea tukio la adhabu kwa watu ili wapate kuonyeka na wakome. Imesemekana kuwa uchache wa kuitwa kundi ni watu watatu, wengine wakasema hata mmoja pia, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na ikiwa makundi mawili katika waumini.." (49:9).

Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu maelezo ya zina, masharti yake, mafungu yake, njia za kuithibitisha, adhabu na utekelezaji wake, toba yamzinifu na mengineyo waliyoyaeleza mafaqihi, katika kitabu Fiqhul-Imam Ja'farus swadiq (a.s) Juz. 6.

Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mwanamume mshirikina.

Imesemkana kuwa Aya hii ni miongoni mwa zenye kutatiza. Kwa sababu dhahiri yake inaonyesha kuwa mwanamume mzinifu haoi ila mzinifu au mshirikina. Vile vile mwanamke; pamoja na kwamba mzinifu huwa anamuoa mwanamke msafi aliye mtukufu.

Vile vile mwanamke mzinifu huwa anaolewa na mwanamume msafi aliye mtukufu. Sasa imekuwaje dhahiri ya Aya ikawa kinyume na hali halisi ya mambo?

Tuonavyo sisi Aya hii iko wazi kabisa. Kwa sababu yenyewe sio kuwa inaleta habari ya hali halisi ya mambo ilivyo, wala sio hukumu ya sharia ya kumlazimisha mzinifu aoe mzinifu mwenzake au mshirikina; kama walivyodai wafasiri wengi. Hapana sivyo kabisa! Kwa sababu Mwislamu haruhusiwi kumuoa mshirikina hata kama imethibiti zina juu yake. Vile vile mwanamke Mwislamu haruhusiwi kuolewa na mshirikina hata kama amezini.

Kwa hiyo hayo siyo makusudio yake; isipokuwa maana yake - bila ya kuangalia sababu iliyoshukia - ni kuwa zina ni jambo ovu na la fedheha kabisa, haifanyi ila malaya muovu.
Akitaka kuzini mtu basi atapata aliye mfano wake katika uovu. Malaya ni wa malaya. Kwa ufupi ni kuwa maana ya Aya yanafanana na kusema: Hakuna anayekubaliana na kosa lako ila mkosa kama wewe ambaye hana dini wala dhamiri. Sasa ni wapi na wapi haya na kuleta hukumu ya sharia?

Kauli yake Mwenyezi Mungu 'Au mshirkina' ni kuashiria kwamba zina iko kwenye daraja ya ushirikina. Mwenyezi Mugu amelinganisha sawa hukumu ya shirk, kuua na kuzini, pale aliposema: "Na wale wasiomwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu ila kwa haki, wala hawazini na mwenye kufanya hivyo atapata madhambi' (25:68). Mtume (s.a.w) aliulizwa kuhusu madhambi makubwa, akataja haya matatu.

Na hayo yameharamishwa kwa waumini. Hayo ni hayo ya Kuzini.

Na wale ambao wanawasingizia wanawake wanaoheshimika, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni viboko thamanini.

Makusudio ya kusingizia hapa ni kusingizia zina. Neno la kiarabu, lililofasiriwa 'ambao,' lina dhamiri ya wanaume, lakini wanakusudiwa wote. Makusudio ya wanaoheshimika hapa ni wale wanawake wasafi wanaojichunga na zina; ni sawa wawe wameolewa au la. Ulama wamelinganisha hukumu ya mwanamume sawa na mwanamke. Kwa maneno mengine ni kuwa hukumu ya kutandika viboko inamuhusu mwanamume na mwanamke.

Msingiziaji mwanamume au mwanamke atatandikwa ikiwa hakuleta mashahidi wane walioshuhudia uingiaji wa tupu na utokaji wake, kama kinavyoingia kijiti cha wanja kwenye kichupa chake. Lengo la mkazo huu na mashahidi wengi ni kulinda familia zisitawanyike kwa kusingiziana.

Na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio mafasiki. Isipokuwa wale waliotubia baada ya hayo na wakatengenea; kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria, Mwenye kurehemu.

Wanaelzewa wale wenye kuisingizia. Maana ni kuwa mwenye kumsingizia mwenye kujichunga na asithibishe kwa ushahidi, basi huyo ni fasiki, ushahidi wake haukubaliwi kabisa kwenye jambo lolote, ila baada ya kutubia na kufanya mambo mema. Akishatubia na akawa na sera nzuri, basi ushahidi wake utakubaliwa; ni sawa awe ametubia baada ya adhabu au kabla.

Abu Hanifa anasema: "Ushahidi wake haukubaliki kabisa hata akitubia, kwa sababu kukataliwa kwake ni miongoni mwa adhabu na kutiwa adabu..." Lakini huku ni kutatizika.

Kwa sababu kauli yake Mwnyezi Mungu, 'Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kughufiria Mwenye kurehemu,' iliyokuja moja kwa moja inaashiria kukubaliwa kwake hata kama ametubia baada ya adhabu. Inayofafanua zaidi Aya hii ni kauli ya Mtume (s.a.w.): "Mwenye kutubia dhambi ni kama asiye na dhambi."

وَالَّذِينَ يَرْمُونَ أَزْوَاجَهُمْ وَلَمْ يَكُنْ لَهُمْ شُهَدَاءُ إِلَّا أَنْفُسُهُمْ فَشَهَادَةُ أَحَدِهِمْ أَرْبَعُ شَهَادَاتٍ بِاللَّهِ ۙ إِنَّهُ لَمِنَ الصَّادِقِينَ {6}

Na wale wanaowasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli.

وَالْخَامِسَةُ أَنَّ لَعْنَتَ اللَّهِ عَلَيْهِ إِنْ كَانَ مِنَ الْكَاذِبِينَ {7}

Na mara ya tano kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.

وَيَدْرَأُ عَنْهَا الْعَذَابَ أَنْ تَشْهَدَ أَرْبَعَ شَهَادَاتٍ بِاللَّهِ ۙ إِنَّهُ لَمِنَ الْكَاذِبِينَ {8}

Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu, kwamba huyo mume ni miongoni mwa waongo.

وَالْخَامِسَةَ أَنَّ غَضَبَ اللَّهِ عَلَيْهَا إِنْ كَانَ مِنَ الصَّادِقِينَ {9}

Na mara ya tano kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, kama mume ni miongoni mwa wasemao kweli.

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّهَ تَوَّابٌ حَكِيمٌ {10}

Na lau kuwa si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kutakabali toba, Mwenye hekima.