read

Aya 21 -25: Msifuate Nyayo Za Shetani

Maana

Enyi amabo mmeamini! Msifuate nyao za shetani kwa kutangaza uovu kwa wale ambao wameamini, wala kwa jambo linalotia wasiwasi na kuwavutia kwake.

Na atakayefuata nyayo za shetani, basi yeye huamrisha machafu na maovu.

Anayewezwa na shetani nafsini mwake, humuongoza kwenye mabaya na machafu.

Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, asingelitakasika miongoni mwenu yoyote kabisa.

Mwenyezi Mungu ametufahamisha njia ya kheri na njia ya shari, akatukataza hili na akatuamrisha lile, akatupa uwezo wa kutenda na kuacha na akaufungua mlango wa toba kwa mwenye kuasi. Hii ndiyo fadhila yake. Ama utakaso wake huwa hampi isipokuwa mwenye kusikia na akatii.

Lakini humtakasa amtakaye na Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi na mwenye hekima pia. Hawatakasi isipokuwa wenye amali na nyoyo safi.

Na wale katika nyinyi wenye wasaa wasiape kutowapa walio jamaa na maskini na waliohama katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Imepokewa kuwa Aya hii ilishuka kwa ajili ya Abu Bakri alipoapa kutomsaidia Mistah Bin Athatha baada ya kushiriki pamoja na aliyeshiriki kueneza uvumi wa uovu kumhusu Ummul-mu'min (Mama wa waumin). Sifa hizi tatu zote anazo Mistah: Ni mtoto wa mama mdogo wa Abu bakr, ni maskini asiyekuwa na mali naye ni katika wahajiri na waliopigana Badri.

Na wasamehe na waachilie mbali. Je, nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu awasamehe? Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu.

Hii ni ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kumsamehe na kumre- hemu atakayemsamehe aliyemfanyia ubaya. Imam Zaynul'abidin (a.s.) alikuwa akimsamehe anayemfanyia ubaya, kisha anamwambia Mwenyezi Mungu: Ewe Mola wetu! Hakika wewe umeamrisha tumsamehe atakayetudhulumu, nasi tumesamehe, kama ulivyoamrisha, basi tusamehe; kwani hakika wewe ndiwe mbora zaidi wa hilo kuliko sisi.

Hakika wanaowasingizia wanawake wanaoheshimika, walioghafilika walio waumini, wamelaaniwa duniani na akhera na watapata adhabu kubwa.

Katika Aya ya 4 ya Sura hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alibainisha kwamba mwenye kumtuhumu mwanamke kwa zina na asilete mashahidi wane basi adhabu yake duniani ni kuchapwa viboko thamanini vyovyote vile atakavyokuwa na hakutaja adhabu yake akhera.

Katika Aya hii tuliyo nayo, anabainisha malipo yake huko akhera, ambayo ni adhabu kubwa, ikiwa aliyetuhumiwa ni ni msafi mwenye kujiheshimu na hayo aliyotuhumiwa. Ndio makusudio ya wenye kughafilika; yaani wenye kughafilika na zina, hawaifanyi wala hawaifikirii.

Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyokuwa wakiyatenda.
Duniani inahitajika ushahidi ikiwa mwanamke anadai kuwa ametuhumiwa na mdaiwa akikataa. Akishindwa kuthibitisha basi madai yake yatakataliwa. Lakini huko akhera hakuhitajiki ushahidi, kwa sababu mtendaji hana njia ya kukana. Lau tukikadiria kuwa atakana au kujaribu kukana, basi viungo vyake vitamshuhudia. Kila kiungo kitashuhudia kile kilichofanya. Ulimi wake utashuhudia ulichozungumza, mkono na ulichokishika na mguu na ulichokiendea n.k.

Siku hiyo atawatekelezea sawa malipo yao ya haki na watajua kwam- ba hakika Mwenyezi Mungu ndiye haki iliyo wazi.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawahisabu kesho na kuwalipa malipo ya haki na ya uadilifu. Hapo ndio watajua kwamba ufufo, hisabu na malipo walioahidiwa ni kweli, hakuna kuyakimbia.

الْخَبِيثَاتُ لِلْخَبِيثِينَ وَالْخَبِيثُونَ لِلْخَبِيثَاتِ ۖ وَالطَّيِّبَاتُ لِلطَّيِّبِينَ وَالطَّيِّبُونَ لِلطَّيِّبَاتِ ۚ أُولَٰئِكَ مُبَرَّءُونَ مِمَّا يَقُولُونَ ۖ لَهُمْ مَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ {26}

Mambo ya uhabithi ni ya mahabithi na mahabithi ni wa mambo ya uhabithi. Na mema ni ya walio wema na walio wema ni wa mema. Hao wameepushwa na wanayoyasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّىٰ تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَىٰ أَهْلِهَا ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ {27}

Enyi ambao mmeamini! Msiingie nyumba zisizo nyumba zenu mpaka muombe ruhusa na muwatolee salaam wenyewe. Hayo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka.

فَإِنْ لَمْ تَجِدُوا فِيهَا أَحَدًا فَلَا تَدْخُلُوهَا حَتَّىٰ يُؤْذَنَ لَكُمْ ۖ وَإِنْ قِيلَ لَكُمُ ارْجِعُوا فَارْجِعُوا ۖ هُوَ أَزْكَىٰ لَكُمْ ۚ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ {28}

Na msipomkuta yoyote humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa rudini, basi rudini. Hivyo ni usafi zaidi kwenu na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda.

لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَنْ تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ مَسْكُونَةٍ فِيهَا مَتَاعٌ لَكُمْ ۚ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مَا تُبْدُونَ وَمَا تَكْتُمُونَ {29}

Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisizokaliwa amabazo ndani yake mna bidhaa zenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyadhirisha na mnayoyaficha.