Aya 30 – 31: Hijabu Na Kuinamisha Macho
Maana
Aya mbili hizi ni miongoni mwa Aya za hukmu, na zimeeleza wajibu wa kuinamisha jicho kwa wanawake na wanaume, kuhifadhi tupu na zina na hijabu. Ufafanuzi ni huu ufuatao:
1. Na waambie waumini wanaume wainamishe katika macho yao.
Mwenyezi Mungu amewaamrisha wanaume wazuie macho yao, lakini hakubainisha wayazuie macho yao kwenye nini. Ameyanyamazia hayo kwa kutaka yafahamike kutokana na mfumo wa maneno. Kwani lilio dhahiri ni kuharamishwa kuwaangalia watu kando.
Wameafikiana mafaqihi wengi kwamba haijuzu kwa mwanamume kuangalia kitu katika mwili wa mtu kando mwanamke, isipokuwa uso wake na viganja kwa sharti ya kuangalia bila ya kujiburudisha na kutohofia kuingia katika haramu. Hii ni kwa mwanamke Mwislamu ambaye dini yake inamkataza kujiweka wazi. Ama yule ambaye dini yake haimkatazi kujiweka wazi, wametofautiana mafaqihi katika kujuzu kuwangalia bila ya kujiburudisha. Wengine wakasema inajuzu kuangalia nywele za wanawake waislamu mabedui wasiokatazika.
2. Na wazilinde tupu zao na zina.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameingiza neno 'katika' kwenye macho, lakini hakuingiza kwenye tupu. Kwa sabu ni wajibu kusitiri tupu wakati wote isipokuwa katika faragha ya mume na mke, lakini kuangalia si haramu katika hali zote isipokuwa katika baadhi ya hali.
Hilo ni usafi zaidi kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za wanayoyafanya.
Hilo ni hilo la kuinamisha macho na walio haramu kuwaangalia, jambo ambalo ni twahara zaidi kwa nafsi na karibu zaidi kwa takua na linaweka mbali dhambi.
3. Na waambie waumini wanawake wainamishe katika macho yao na wazilinde tupu zao.
Mafaqihi wa kishia wamesema kuwa ni haramu kwa mwanamke kumtazama mwanamume aliye mtu kando, vile ilivyo haramu kwa mwanamume juu ya mwanamke. Kwa hiyo haijuzu kwa mwanamke kuangalia nywele za mwanamume n.k. Lakini wengine wamesema kuwa inajuzu kwa mwanamke kumwangalia mwanamume sehemu zote isipokuwa sehemu iliyo baina ya kitovu na magoti. Ufafanuzi uko kwenye kitabu chetu cha Fiqh ala madhahibul-khamsa (Fiqh katika madhebu tano) sehemu ya yaliyo wajibu kuangalia na yaliyo haramu.
4. Wala wasionyeshe uzuri wao, isipokuwa unaodhihirika.
Makusudio ya uzuri hapa ni sehemu zao. Kwa sababu si haramu kuangalia uzuri. Makusudio ya unaodhihirika ni sehemu za uso na viganja viwili tu. Mafaqihi wametoa dalili kwa Aya hii, juu ya wajibu wa hijabu na kwamba mwili wote wa mwanamke ni uchi isipokuwa uso na viganja viwili vya mikono.
Imam Ja'far Swadiq (a.s.). Aliulizwa kuhusu mikono miwilli kuwa je, ni katika uzuri aliouzungumzia Mwenyezi Mungu? Akasema ndio na sehemu yoyote isiyokuwa uso na viganja viwili ni katika uzuri ulioharamishwa. Katika kitabu Ahkamul-Ayat cha Aljasas, mmoja wa maimamu wa kihanfi anasema: "Makusudio ya unaodhihiri ni uso na viganja viwili. Katika Tafsir ya Razi ambaye ni wa madhehebu ya Shafi anasema: "Wameafikiana kuwa uso na viganja viwili si sehemu ya tupu."
Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao.
Neno vifua, limefasiriwa kutokana na neno juyub lenye maana ya uwazi wa magauni. Yaani ni wajibu kwa wanawake kuangusha mitandio yao kwa mbele ili isitiri, shingo na vifua.
Wanawake wa wakati wa jahilia, walikuwa wakifunika vichwa vyao kisha wanangusha shungi zao kwa nyuma, shingo zao na vifua vyao vinakuwa wazi. Wakaendela kuwa hivyo hata wakati wa Uislamu, mpaka iliposhuka Aya hii wakawa wanaangusha kwa mbele na kusitiri shingo na vifua.
Kujiweka Wazi Au Kujiuza?
Uislamu umeruhusu mwanamke afunue uso wake na viganja vyake, kwa sababu kuna dharura ya kimaisha. Sehemu nyinginezo zisizokuwa hizo, zimezingatiwa kuwa ni uchi, kwa sababu ni hatari. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: "Mwenye kuchunga kondoo wake kandokando ya ugo nafsi yake inamvuta kuchunga ndani yake."
Hivi ndivyo ilivyo hasa. Popote uendapo utajionea maajabu. Mwanamke alianza kufunua kichwa chake baada ya kwenda saloni, akendela kufunua kifua na mabega hadi kufikia minisketi na mavazi mengine ya maajabu yanaonyesha umbile zima la mwanamke; huku akijitembeza barabarani kama kwamba ni nyama inayouzwa sokoni. Siri ya hilo ni kwamba wanawake wengi hawaendi mbali zaidi ya kujionyesha na kuonyesha urembo wao tu.
Maajabu zaidi niliyoyasoma kuhusu mambo haya ni kwamba huko mjini Humburg, Ujerumani ya magharibi, kuna barabara ya kutisha ambayo pambizoni mwake mna sehemu zilizo na wanawake wakiwa uchi, katika hali isiyokuwa ya kawaida ambayo haingiliki akilini. Kila ambalo unaliona kuwa haliwezi kufanyika basi hapo linafanyika kiuhakika. Huu ndio upeo wa uhuru.
Nimesoma makala hii nikiwa natetema, na kufikiria kwamba barabara hii iliyo uchi, kama sio hivi karibuni basi baadae itafika kwenye miji yetu; sawa na ilivyofika minisketi na mengineyo; maadamu tunaigiza magharibi. Mungu apishe mbali na yatakayokuja kesho.
Kwa mnasaba huu tunadokeza kwamba, ikiwa mwanamke anapenda sana kuonyesha urembo wake na uzuri wake na kutengeneza shepu yake kwa kila njia, basi kuna wanaume wengi wanaopenda kuonyesha umashuhuri wao, hata kama ni kwa njia ya uongo na kudanganya. Ikiwa mwanamke anamfanyia chuki anayeshindana naye kwa uzuri na urembo, basi wanaume wanaopenda kujionyesha wana hasadi zaidi hasa kwa yule ambaye jina lake linatajwa.
Mnamo mwaka 1957, mwandishi mmoja wa Kimisri, alitoa makala ambayo ndani yake aliibeza fat-wa ya masheikh wa Al-azhar kuharamisha mwanamke kuvaa nguo ya kuogelea. Miongoni mwa aliyoyasema ni: Uislamu uko mbali na fatwa hii.
Mimi nilitoa makala kupinga maelezo yake haya, na nikathibitisha kuwa masheikh wa Al-Azhar wametamka neno la Uislamu na Qur'an, na nikatoa ushahidi wa Aya: 'Wala wasidhihirishe uzuri wao.'
Baada ya kupita siku, ikasadifu mimi na mwenzangu mmoja kumtembelea sheikh mmoja. Tulipotulia yule sheikh akanikabili na kusema: "Vipi wewe unahalalisha kuvaa nguo ya kuogelea na kuwarudi masheikh wa Al-azhar ambao wametoa fatwa ya kuharamisha?
Nikamwambia: Hapana ni kinyume na hivyo. Mimi nimewaunga mkono masheikh na nikaiponda rai ya mwenye kuwarudi.
Akasema: "Hapana! Mimi ninalo gazeti lilo na makala hiyo, ngoja nikuonyeshe."
Nikamwambia ailete.
Basi akaenda haraka na akaja na gazeti mkononi mwake, akaanza kulisoma kwa hamasa kubwa.
Nikamwambia: Je, umeona nini?
Akapigwa na butwaa, gazeti likamponyoka mikononi. Alhamdulillah, hapo pia alikuwako rafiki wa sheikh na sheikh mmoja miongoni mwa jamaa zake. Hao wawili bado wako hai hivi sasa tukiwa katika wakati wa kusi mwaka 1969.
Siwezi kupata tafsiri ya sheikh huyu ambaye alijiumbua mwenyewe isipokuwa Mungu amsamehe. Yeye alitaka anitie aibu na kuniumbua, akawa anatafuta taa na utambi, kama wasemavyo watu wa Amol, ili aanze kueneza na kutangaza.
Na pale aliposoma jina langu kwenye gazeti chuki yake iliyojificha ililipuka na kupenda kwake umashuhuri kukampofusha, weupe akauona ni weusi na haki kuwa ni batili. Sio siri kwamba chuki ni sawa na mapenzi, inapofusha na kufanya uziwi. "Wana nyonyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi. Hao ndio walioghafilika." Juz. 9 (7:179).
Sikutaja kisa hiki kwa kulalamika au kushtakia, hapana! Uzoefu umenifundisha kutowajali waongo, lakini kalamu yangu imenizidia na haikunipa hiyari. Hivi ndivyo nilivyo mimi na kalamu yangu.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwakataza wanawake Waislamu kutofunua sehemu zao isipokuwa uso na viganja, sasa anabainisha wale ambao inafaa kuwadhihirishia ambao ni aina kumi na mbili:
1. Wala wasidhihirishe uzuri wao ila kwa waume zao. Kila mmoja kati ya mume na mke anaweza kumwangalia mwenzake popote atakapo.
2. Au baba zao. Hapa wanaingia mababu wa upande wa baba na mama.
3. Au baba wa waume zao. Wanaingia mababa wa waume na mababu zao wa upande wa baba na mama
4. Au watoto wao. Mtoto wa mtoto, mwanamume au mwanamke, pia ni mtoto.
5. Au watoto wa waume zao na kuendelea chini.
6. Au ndugu zao wa baba mmoja tu au mama mmoja tu au wote.
7. Au watoto wa kaka zao na kuendelea chini.
8. Au watoto wa dada zao vilevile kuendelea chini.
9. Au wanawake wao. Ieleweke kuwa ni haramu kuwa uchi kabisa mwanamke mbele ya mwanamke mwenzake hata kama ni mama yake au binti yake, kama ambavyo ni haramu kwake yeye pia kuwaangalia uchi. Ni halali kuangaliana sehemu zisizokuwa hizo, ikiwa ni Mwislamu. Ama mwanamke asiyekuwa Mwislamu haifai kuwa wazi mbele yake. Hivi ndivyo ilivyofahamisha Aya. Linalokhalifu hilo liachwe. Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa wanawake wasiokuwa waislamu wakijifunua mbele ya wanawake wasiokuwa waislamu wanaenda kuwasifia waume zao.
10. Au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, katika wajakazi tu. Ama mtumwa wa kiume haijuzu kumwangalia isipokuwa uso na viganja viwili; hata kama ni hasi. Kauli na riwaya zinazokhalifu hayo basi zinaachwa. Kwa vyovyote, ni kuwa maudhui haya hayapo siku hizi, ambapo hakuna utumwa.
11. Au wafuasi wanaume wasio na matamanio. Hao ni wale wanaochanganyika na familia na kuwa nao mara nyingi, waki- wa hawana matamanio ya wanawake, kwa sababu za kimwili; kama uzee na uhanithi au za kuathirika kisaikolojia.
12. Au watoto wadogo ambao hawajajua uchi wa wanawake. Yaani watoto wadogo ambao hawawezi kupambanua baina ya uchi na kiungo kingine.
Wala wasipige miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha.
Wanawake walikuwa wakivaa vikuku miguuni, mpaka sasa desturi hii inaendelea katika miji mingi ya waarabu. Baadhi walikuwa wakipiga miguu yao chini ili vigongane vikuku vyao kuwavutia wanaume au wajue kuwa wamevaaa vikuku. Ndipo Mwenyezi Mungu akawakataza hilo. Hapo inaashiria kwamba haifai kwa mwanamke kufanya jambo lolote litakalomvutia mwanamume.
Na tubieni kwa Mwenyezi Mungu nyote enyi waumini, ili mpate kufanikiwa.
Acheni yale aliyowakataza Mwenyezi Mungu, na ambaye atateleza kufanya makosa basi afanye haraka kutubia.
وَأَنْكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنْكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ ۚ إِنْ يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ ۗ وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ {32}
وَلْيَسْتَعْفِفِ الَّذِينَ لَا يَجِدُونَ نِكَاحًا حَتَّىٰ يُغْنِيَهُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ ۗ وَالَّذِينَ يَبْتَغُونَ الْكِتَابَ مِمَّا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ فَكَاتِبُوهُمْ إِنْ عَلِمْتُمْ فِيهِمْ خَيْرًا ۖ وَآتُوهُمْ مِنْ مَالِ اللَّهِ الَّذِي آتَاكُمْ ۚ وَلَا تُكْرِهُوا فَتَيَاتِكُمْ عَلَى الْبِغَاءِ إِنْ أَرَدْنَ تَحَصُّنًا لِتَبْتَغُوا عَرَضَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۚ وَمَنْ يُكْرِهْهُنَّ فَإِنَّ اللَّهَ مِنْ بَعْدِ إِكْرَاهِهِنَّ غَفُورٌ رَحِيمٌ {33}
وَلَقَدْ أَنْزَلْنَا إِلَيْكُمْ آيَاتٍ مُبَيِّنَاتٍ وَمَثَلًا مِنَ الَّذِينَ خَلَوْا مِنْ قَبْلِكُمْ وَمَوْعِظَةً لِلْمُتَّقِينَ {34}