read

Aya 32 – 34: Waozeni Wajane

Maana

Na waozeni wajane miongoni mwenu.

Maneno yanaelekezwa kwa Waislamu wote. Wajane ni wale wasiokuwa na wake au wasiokuwa na waume. Amri hii hapa ni ya Sunna sio ya wajibu. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwaamrisha wanaume na wanawake wahifadhi tupu zao na kujizuia na mambo yaliyo haramu na pia kuwakataza wanawake kujipamba na kudhihirisha kipambo mbele ya watu kando.

Sasa anaamrisha kusaidiana kwa kila anayehitajia ndoa baina ya wanaume na wanawake. Kwa sababu ujane ndio chimbuko la uchafu na uovu; kama zina na ulawiti. Na ndoa ni kinga ya hayo. Ndio maana Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) akasema: "Waovu wenu ni wajane wenu…"

"Ndoa ni katika sunna yangu, atakayejiepusha na sunna yangu basi si katika mimi."

Na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu.

Makusudio ya wema hapa ni waumini. Yaani waozeni watumwa wakiwa ni waumini, maudhui haya hayapo, kwa kutokuwepo utumwa.

Wakiwa mafukara Mwenyezi Mungu atawatajirisha katika fadhila zake

Watu wengi hawaangalii maadili ya mchumba, bali wanaangalia cheo chake au mali yake. Ndipo Mwenyezi Mungu akalaumu fikra hii na akasema kuwa yeye ni muweza wa kila kitu. Kuna Hadith isemayo: "Akiwajia ambaye mnairidhia hulka yake na dini yake, basi muozeni; kama hamtafanya itakuwa fitna katika ardhi na uharibifu mkubwa."

Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.

Anatoa wasaa kwa anaemuomba na asiyemuomba kwa fadhila zake.

Na wajizuilie na machafu wale wasiopata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu awatajirishe.

Unaweza kuuliza: katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu amesema kuwa watu waoe tu, wakiwa mafukara atawatajirisha; kisha hapa anasema, tena moja kwa moja baada ya kauli ya kwanza, kuwa mtu asiyepata mahari wala posho asiingie kwenye uovu na kwamba avumilie mpaka Mwenyezi Mungu ampe wasaa, basi kuna wajihi gani baina ya Aya mbili?

Jibu: Hakuna haja ya kuchanganya Aya mbili hizi, kwa sababu kila moja ina makusudio yake. Ya kwanza inawakusudia mawalii, kwamba akija mchumba msimkatae kwa sababu ya ufukara wake. Aya ya pili inamuhusu fukara mwenyewe, kwamba akinyimwa kuoa kwa sababu ya ufukara wake, basi avumilie na afanye bidii mpaka Mungu atakapompa wasaa wa kuweza kuoa.

Na wale ambao wanataka kuandika katika wale amabao imewamiliki mikono yenu ya kuume, basi waandikieni kama mkiona wema kwao.

Ambaye ana mtumwa wa kike au wa kiume anayeweza kuchuma, anaweza kuandikiana naye mkataba kuwa akitoa kiasi fulani cha pesa mara moja au pole pole, awe huru.

Akitekeleza yote basi anakuwa huru au akitoa baadhi atakuwa ana uhuru wa kiasi kile alichotoa, ikiwa hakuna sharti la kutoa chote; vinginevyo hatakuwa na uhuru wowote.

Imesekana kuwa mtumwa hawezi kugawika; ama awe huru kamili au awe mtumwa kamili. Ni Sunna kwa mwenye mtumwa kumwachia kiasi fulani cha mali waliyoelewana. Hayo ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyowapa.

Mafaqihi wameweka istilahai ya neno mkataba kwa makubaliano haya, kutokana na Mwenyezi Mungu kutumia neno kitab.

Wala msiwalazimishe vijana wenu wa kike kufanya umalaya kwa ajili ya kutafuta pato la maisha, ikiwa wanataka kujichunga.

Makusudio ya vijana wa kike hapa ni wajakazi, ambao hivi sasa hawako. Watu wa wakati wa ujahiliya walikuwa wakiwalazimisha wajakazi wao kufanya zina kwa kutaka mali, ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akalikataza hilo.

Unaweza kuuliza kuwa dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu 'wakitaka kujichunga,' inaonyesha kuwa kama hawataki kujichunga basi wanaweza kulazimishwa kufanya zina, na hali tunajua kuwa zina ni hara- mu kwa nyanja zake zote?

Jibu, maana ya neno 'ikiwa' yanatofautiana kwa kutofautiana makusudio na maneno yalivyo. Inaweza ikawa kwa maana ya sharti hasa, ilivyo. Kwa mfano kumwambia mtu: Ikiwa utafanya hivi na mimi nitafanya kama utakavyofanya. Hapa utakuwa umeweka sharti kwamba hutafanya mpaka afanye yeye.

Mara nyingine inakuwa bila ya kukusudia sharti; kwa mfano kumwambia sahibu yako: "Ikiwa utaruzukiwa mtoto basi usimnunulie baskeli" hapa haina maana kama hataruzukiwa mtoto basi anaweza kumnunulia baskeli; jambo ambalo litakuwa kama kuchanganyikiwa. Isipokuwa unataka kumweleza maoni yako ya kutotaka watoto wapande baskeli.

Maana haya ndiyo yaliyokusudiwa hapa 'ikiwa' limekuja kubainisha hali halisi; kwamba ikiwa wajakazi wanataka kujichunga basi nyinyi itakuwa ni zaidi mjichunge.

Kama tukiliweka neno 'ikiwa' kwa maana ya sharti, itakuwa maana yake ni: walazimisheni wajakazi wenu ikiwa wanataka zina. Na inavyojulikana ni kuwa hakuna kulazimisha ikiwa mtu anataka.

Matamshi Na Uelewa

Kwa maneno mengine ni kuwa neno 'ikiwa' au 'iwapo' au 'kama' na mengineyo mfano wake, huwa linafahamisha vitu viwili kwa wakati mmoja: Maana yake kimatamshi na maana yake kiufahamu na kiuelewa ambayo hayakutamkwa lakini yanafahamika kwa ishara. Kwa istlahi ya watu wa elimu ya usul, wanaita mantuq na mafhum

Mantuq ni kwa mfano kumwambia sahibu yako; ikiwa utanikirimu na mimi nitakukirimu. Kwa hiyo kimatamshi hapa imeeleweka kuwa kumkirimu kwako kutategema yeye ikiwa atakukirimu.

Ama kiufahamu, katika mfano huu ni kuwa, ikiwa hukunikirimu basi nami sikukukirimu. Maana haya hayakutajwa, lakini yamefahamika kutokana na jumla ya kwanza.

Aya tuliyo nayo iko katika aina ya kwanza tu, ya kimatamshi; haiwezi kuingia kwenye aina ya pili.

Yaani kutofaa kutolazimisha zina pamoja na kutaka kujisitiri. Hapo ufahamu hauingii, kwa sababu tukileta ufahamu maana itakuwa ni: kujuzu kulazimisha pamoja na kuitaka hiyo zina. Hapo kutakuwa na mgongano, wa kuwalazimisha na wenyewe wanataka, jambo haliwezekani kwa wakati mmoja. Itakuwaje mtu alazimishwe na wakati huo huo mwenyewe anataka. Pia ni muhali kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kulazimisha uovu kwa namna yoyote ile.

Na atakayewalazimisha basi Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu

Wale waliolazimishwa kufanya zina. Kwa sababu kosa ni la yule aliyelazimisha, sio aliyelazimishwa. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: "Umma wangu umeondolewa yale waliyolazishwa…" Mwenye kumlazimisha mwingine kufanya makosa, Mwenyezi Mungu atamghufiria akitubia na kurejea.

Na hakika tumekuteremshia Aya zinazobainisha na mifano kutokana na waliopita kabla yenu na mawaidha kwa wenye takua.

Makusudio ya Aya ni hukumu za Qur'an na mafundisho yake nazo ziko wazi. Mifano ni habari za waliopita na visa vyao. Mawaidha kwa wenye takua ni uongofu kwa mwenye kutaka kuongoka.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameteremsha Qur'an kubainisha na kuweka wazi hukumu tunazozihitajia, habari za waliopita, uongofu kwa mwenye kuutaka, na nguvu kwa mwenye kumtawalisha Mungu.

اللَّهُ نُورُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ مَثَلُ نُورِهِ كَمِشْكَاةٍ فِيهَا مِصْبَاحٌ ۖ الْمِصْبَاحُ فِي زُجَاجَةٍ ۖ الزُّجَاجَةُ كَأَنَّهَا كَوْكَبٌ دُرِّيٌّ يُوقَدُ مِنْ شَجَرَةٍ مُبَارَكَةٍ زَيْتُونَةٍ لَا شَرْقِيَّةٍ وَلَا غَرْبِيَّةٍ يَكَادُ زَيْتُهَا يُضِيءُ وَلَوْ لَمْ تَمْسَسْهُ نَارٌ ۚ نُورٌ عَلَىٰ نُورٍ ۗ يَهْدِي اللَّهُ لِنُورِهِ مَنْ يَشَاءُ ۚ وَيَضْرِبُ اللَّهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ ۗ وَاللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ {35}

Mwenyezi Mungu ni nuru ya mbingu na ardhi. Mfano wa nuru yake ni kama shubaka ndani yake mna taa. Taa hiyo imo katika tungi. Tungi hilo ni kama nyota inayomeremeta, inayowashwa kwa mafuta yanayotokana na mti uliobarikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakurubia mafuta yake kung'aa ingawa hayajaguswa na moto - Nuru juu ya nuru. Mwenyezi Mungu humuongoza kwenye nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano; na Mwenyezi Mungu ni mwenye kujua kila kitu.

فِي بُيُوتٍ أَذِنَ اللَّهُ أَنْ تُرْفَعَ وَيُذْكَرَ فِيهَا اسْمُهُ يُسَبِّحُ لَهُ فِيهَا بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ {36}

Katika nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameruhusu ziinuliwe na kutajwa humo jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni.

رِجَالٌ لَا تُلْهِيهِمْ تِجَارَةٌ وَلَا بَيْعٌ عَنْ ذِكْرِ اللَّهِ وَإِقَامِ الصَّلَاةِ وَإِيتَاءِ الزَّكَاةِ ۙ يَخَافُونَ يَوْمًا تَتَقَلَّبُ فِيهِ الْقُلُوبُ وَالْأَبْصَارُ {37}

Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kuisimamisha Swala na kutoa Zaka. Wanaihofu siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.

لِيَجْزِيَهُمُ اللَّهُ أَحْسَنَ مَا عَمِلُوا وَيَزِيدَهُمْ مِنْ فَضْلِهِ ۗ وَاللَّهُ يَرْزُقُ مَنْ يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ {38}

Ili Mwenyezi Mungu awalipe mazuri ya yale waliyoyatenda, na awazidishie katika fadhila zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.