read

Aya 39 – 42: Vitendo Vyao Ni Kama Sarabi (Mangati)

Maana

Na wale ambao wamekufuru vitendo vyao ni kama sarabi jangwani, mwenye kiu huyadhania ni maji, hata akiyaendea hapati chochote.

Makusudio ya makafiri hapa ni wale wanaokana utume wa Muhammad, kwa sababu ya inadi, ubaguzi, kupuuza au uzembe; yaani hakuutafuta uhakika akiwa ana uwezo wa kufanya utafiti na kuchunguza.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwataja wale ambao mambo ya dunia hayawafanyi wakaacha akhera na kwamba yeye atawalipa kwa yale mema waliyoyafanya, sasa anawataja hawa wapinzani wakanushaji, kwamba wao wametegemea batili na wakaitakidi kuwa ni haki itakayowafaa mbele ya Mwenyezi Mungu; sawa na mwenye kiu anavyotegemea mazigazi. Akitaka kuyafikia basi anakuta ni jua kali linalomzidishia kiu.

Wala hakuhusika na wasifa huu yule anayemkufuru Mwenyezi Mungu au utume wa Muhammad (s.a.w.) tu. Isipokuwa wanahusika wengi katika umma wa Muhammad (s.a.w.) ambao wanajidhania kuwa ni watu wa heri na takua, huku wakiwafanyia chuki na hasadi waja wa Mwenyezi Mungu na wakiipupia dunia na majanga yake.

Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa-sawa. Na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.

Kumkuta Mwenyezi Mungu ni kukuta hisabu yake na malipo yake. Maana ni kuwa kafiri anaitakidi akiwa duniani kwamba yeye ataokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu kutokana na amali njema aliyoifanya, lakini atakaposimama mbele ya Mwenyezi Mungu ili aangalie hisabu, hatapata kitu katika vile alivyoviwazia; bali atakuta dhambi, hisabu na adhabu. Matumaini yote yatayeyuka, kama yalivyoyeyuka ya yule aliyetegemea mangati.

Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyofunikwa na mawimbi juu ya mawimbi na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mkono wake anakurubia asiuone.

Bahari kuu ni bahari yenye maji mengi, mawimbi yamepandana na juu yake kuna mawingu mazito. Huu ni mfano fasaha zaidi wa watu wenye matamanio ambao wamezama katika bahari ya maovu na machafu: uongo, riya, mifundo, majisifu, kiburi, tamaa, pupa na mengineyo yasiyokuwa na kikomo. Mwenye kuishi katika giza hili ambalo haoni kitu, ataona vipi hakika na kuielewa.
Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru, basi huyo hana nuru.

Tabrasi amesema: "Makusudio ni ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia wokovu katika akhera, basi hana uokovu." Tuonavyo sisi ni kuwa wale ambao hawaongoki kwenye njia ya haki aliyowapa muongozo Mwenyezi Mungu, basi wao wataishi katika kuzubaa, ujinga na upotevu.

Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtaksa vilivyomo mbinguni na ardhini na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwishajua Swala yake na tasbihi yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wayatendayo.

UmepitamfanowakekatikaJuz.15(17:44).

Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, kwa sababu ndiye aliyeziumba na muumba ni mfalme wa kweli.

Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya hisabu na malipo.

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يُزْجِي سَحَابًا ثُمَّ يُؤَلِّفُ بَيْنَهُ ثُمَّ يَجْعَلُهُ رُكَامًا فَتَرَى الْوَدْقَ يَخْرُجُ مِنْ خِلَالِهِ وَيُنَزِّلُ مِنَ السَّمَاءِ مِنْ جِبَالٍ فِيهَا مِنْ بَرَدٍ فَيُصِيبُ بِهِ مَنْ يَشَاءُ وَيَصْرِفُهُ عَنْ مَنْ يَشَاءُ ۖ يَكَادُ سَنَا بَرْقِهِ يَذْهَبُ بِالْأَبْصَارِ {43}

Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatanisha pamoja, kisha huyafanya mrundo? Basi utaona mvua ikitokea kati yake. Na huteremsha kutoka mbinguni, kwenye milima ya mawingu, mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmemetuko wa umeme wake kupofua macho.

يُقَلِّبُ اللَّهُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِأُولِي الْأَبْصَارِ {44}

Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hilo kuna mazingatio kwa wenye busara.

وَاللَّهُ خَلَقَ كُلَّ دَابَّةٍ مِنْ مَاءٍ ۖ فَمِنْهُمْ مَنْ يَمْشِي عَلَىٰ بَطْنِهِ وَمِنْهُمْ مَنْ يَمْشِي عَلَىٰ رِجْلَيْنِ وَمِنْهُمْ مَنْ يَمْشِي عَلَىٰ أَرْبَعٍ ۚ يَخْلُقُ اللَّهُ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {45}

Na Mwenyezi Mungu amemuumba kila mnyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo, na wengine huenda kwa miguu miwili na wengine huenda kwa minne. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

لَقَدْ أَنْزَلْنَا آيَاتٍ مُبَيِّنَاتٍ ۚ وَاللَّهُ يَهْدِي مَنْ يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ {46}

Hakika tumeteremsha Ishara zinazobainisha. Na Mwenyezi Mungu humuongoza atakaye kwenye njia iliyonyooka.