read

Aya 43 – 46: Maji

Maana

Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatanisha pamoja, kisha huyafanya mrundo. Basi utaona mvua ikitokea kati yake. Na huteremsha kutoka mbinguni, kwenye milima ya mawingu, mvua ya mawe.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hupeleka upepo unoasukuma mawingu kutoka mji mmoja hadi mwingine, kisha huyakusanya pamoja yakiwa mrundo kwa umbo la mlima. Kwenye mawingu haya kunakuwa na maji yanayomiminika na yanayoganda katika vipande vya theluji ambavyo ndivo vinavyoitwa mvua ya mawe.

Akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye.

Mwenyezi Mungu kutumia mvua ya mawe kwa mujibu wa hekima. Ikiwa hekima imepitisha kuangamia mimea au kitu chochote, basi huipelekea mvua; vinginevyo huiepusha.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13: 12 -13). Huko na sehemu nyingine zinazonasibiana nazo tumeeleza kuwa dhahiri ya ulimwengu inategemea sababu zake za kimaumbile moja kwa moja na zinakomea kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuwa ndiye muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.

Hukurubia mmemetuko wa umeme wake kupofua macho.

Umeme wake ni wa hayo mawingu. Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema: "Unakurubia umeme kunyakua macho yao." Juz. 1 (2:20).

Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana, kwa urefu na ufupi.

Hakika katika hilo la kubadilisha kuna mazingatio kwa wenye busara, ambao hawagandi tu kwenye sababu za maumbile, bali wanamtafuta aliyezifanya na kuzitengeneza na kumtambua.

Na Mwenyezi Mungu amemuumba kila mnyama kutokana na maji. Wengine katika wo huenda kwa matumbo, na wengine huenda kwa miguu miwili na wengine huenda kwa minne.

Hakika uweza wa Mwenyezi Mungu na umoja una ushahidi mwingi usiokuwa na idadi. Miongoni mwao ni ule unajitokeza katika kuumba vitu vilivyoganda, tunayoyashuhudia katika uumbaji mimea, wanyama na wanaotembea ardhini.

Hayo ndiyo yaliyoashiriwa katika Aya hii. Tukiangalia mfungamano wa maji katika kutengenezwa mnyama ni kuwa hakika ya maji ni moja, lakini wanyama walioumbwa kutokana na maji hayo wanatofautiana, wengine wanatembea kwa tumbo, kama wale wanaotambaa, wengine wanatembea kwa miguu miwili, kama binadamu na wengine kwa miguu mine, kama ngamia nyumbu wanyama mwitu na wengineo ambao Mwenyezi Mungu amewaashiria kwa kauli yake:

Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

Wanyama wote, kuanzia aina ndogo hadi kubwa, wako kwenye nidhamu kamili, ambapo kila mmoja anafanya kuliangana na inavyoafikiana na maslahi yake. Hii ni dalili mkataa kwamba nyuma ya yote hayo kuna mpangaji aliye hodari na mwenye hekima.

Hakika tumeteremsha Ishara zinazobainisha.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameleta dalili za kuweko kwake, ukuu wake na umoja wake; kama hizi za kuumba aina mbalimbali za wanyama. Hakuacha udhuru wowote kwa mwenye kutafuta sababu. Imam Ali (a.s.) anasema: "Amewabunia umbile la ajabu katika vyenye uhai na visivyokuwa na uhai na vilivyotulia na vyenye harakati, akaweka ushahidi na ubainifu katika utovu wa utengenezaji wake na ukuu wa cheo chake, kiasi cha akili kuweza kumfuata na kumkubali na kusalimu amri kwake."

Na Mwenyezi Mungu humuongoza atakaye kwenye njia iliyonyooka.

Hakuna shaka kwamba mwenye kufuata njia iliyonyooka ambayo Mwenyezi Mungu ameiamrisha basi huyo ameongoka mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kuasi amri yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, huyo amepotea kwa Mungu na kwa watu wote, hilo halina shaka.

وَيَقُولُونَ آمَنَّا بِاللَّهِ وَبِالرَّسُولِ وَأَطَعْنَا ثُمَّ يَتَوَلَّىٰ فَرِيقٌ مِنْهُمْ مِنْ بَعْدِ ذَٰلِكَ ۚ وَمَا أُولَٰئِكَ بِالْمُؤْمِنِينَ {47}

Na wanasema tumeamini Mwenyezi Mungu na Mtume na tumetii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala wao si wenye kuamini.

وَإِذَا دُعُوا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِنْهُمْ مُعْرِضُونَ {48}

Na wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili awahukumu baina yao, ndipo kikundi kimoja kinakataa.

وَإِنْ يَكُنْ لَهُمُ الْحَقُّ يَأْتُوا إِلَيْهِ مُذْعِنِينَ {49}

Na ikiwa haki ni yao wanamjia kwa kutii.

أَفِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ أَمِ ارْتَابُوا أَمْ يَخَافُونَ أَنْ يَحِيفَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ وَرَسُولُهُ ۚ بَلْ أُولَٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ {50}

Je, wana maradhi katika nyoyo zao au wanaona shaka au wanahofia kuwa atawadhulumu Mwenyezi Mungu na Mtume wake? Bali wao ndio madhalimu.

إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَنْ يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۚ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ {51}

Haiwi kauli ya waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ila ni kusema: Tumesikia na tumetii. Na hao ndio wenye kufaulu.

وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَيَخْشَ اللَّهَ وَيَتَّقْهِ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ {52}

Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu.

وَأَقْسَمُوا بِاللَّهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَئِنْ أَمَرْتَهُمْ لَيَخْرُجُنَّ ۖ قُلْ لَا تُقْسِمُوا ۖ طَاعَةٌ مَعْرُوفَةٌ ۚ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ {53}

Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao ya kwamba ukiwaamrisha, hakika watatoka. Sema: msiape! Utiifu unajulikana. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.

قُلْ أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِنْ تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُمْ مَا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِنْ تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ {54}

Sema: mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kama mkikengeuka basi yaliyo juu yake ni aliyobebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyobebeshwa. Na mkimtii yeye mtaongoka na hapana juu ya mtume ila kufikisha (ujumbe) wazi wazi