read

Aya 62 – 64: Hawaondoki Mpaka Wakuombe Ruhusa

Maana

Hakika waumini ni wale tu ambao wamemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakiwa pamoja naye kwa jambo la wote, hawaondoki mpaka wamtake ruhusa.

Wanafiki walikuwa wakitoroka kwa kujificha kila wanapoitwa kwenye jambo muhimu katika kikao pamoja na Mtume. Ndipo ikashuka Aya hii kubainisha wajibu wa kutiiwa Mtume na umma wake, wajibu wa kusaidiana waislamu ili kuuinua Uislamu na kwamba Mwislamu wa kweli ni yule anayeitikia mwito wa Mtume na kusaidiana kwa pamoja, jambo ambalo lina kheri na masilahi, kwa juhudi zake zote. Wala asikimbie wajibu huu kwa kutafuta visababu.

Akiwa ni mkweli katika udhuru basi auleze kwa Mtume (s.a.w.) na amuombe ruhusa. Hali hii ni wajibu kwa kila kiongozi anayetekelea haki za raia kwa ikhlasi.

Hakika wale wanaokuomba ruhusa, wakiwa ni wa kweli katika kauli zao na wana haja ya dharura, hao ndio wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kikwelikweli. Ama wale ambao wanatafuta visababu vya uongo, basi hao ndio wanafiki wanaosema kwa midomo yale ambayo hayako nyoyoni mwao. Muimin ni kama askari, anangojea amri tu ya kiongozi wake wala haiachi ila kama ana udhuru wa kweli, hapo huomba ruhusa.

Na watakapokuomba ruhusa kwa baadhi ya mambo yao, mruhusu umtakaye miongoni mwao na uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufia, Mwenye kurehemu.

Mwenyezi Mungu amemwachia amri Mtume (s.a.w.) akitaka atoe ruhusa au akatae, na akamwamrisha kumuombea Mungu yule mkweli mwenye ikhlasi.

Unaweza kuuliza kuwa Mwenyezi Mungu mahali pengine amesema: "Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini umewapa ruhusa kabla ya kubainika kwako wanaosema kweli na ukawajua waongo?" Juz. 10 (9:43) na kwenye Aya hii amemruhusu kutoa ruhusa, zitaungana vipi Aya hizi?

Jibu: Kule Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake kuthibitisha kuweza kumjua mkweli na muongo. Katika sura hii tuliyo nayo, amem- ruhusu kutoa ruhusa baada ya kujua uhakika wa mwenye kutaka ruhusa, malengo yake na natija ya kutaka idhini awe mumin au mnafiki. Kwa hiyo atatoa ruhusa kwa misingi hii.

Inawezekana ni masilahi kumpa ruhusa mnafiki, ikiwa kubakia kwake kundini kunaleta madhara na pia inawezekana kumnyima ruhusa kukawa na manufaa kwa kuhitajika kwake kundini.

Msifanye kumwita Mtume baina yenu kama mnavyoitana nyinyi kwa nyinyi.

Maneno wanelekezewa wale waliokuwa na Mtume, wakifundishwa adabu wakiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) ambapo waliamrishwa wanapotaka ruhusu wasimwite kwa majina yake au lakabu yake; mfano kusema: ewe Muhammad au Ewe Abul-Qasim; kama wanavyoitana wao kwa wao.

Bali wamwite kwa sifa zake tukufu, za unabii au utume; kwa mfano kusema: Ewe Nabii wa Mungu au Ewe Mtume wa Mungu! Kwani kumheshimu yeye ndio kumheshimu Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amekutanisha twaa yake na ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) katika Aya kadha zikiwemo hizi:

فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنْزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ {157}

"Basi wale waliomuamini na wakamheshimu na wakamsaidia na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye. Hao ndio wenye kufaulu. Juz.9 (7:157).

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ{2}

"Enyi ambao mmeamini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa kelele, kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi." (49:2).

Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wale wanoondoka kwa kujificha.

Yaani kujificha kwa wanafiki wanapotoroka pale wanapoambiwa mambo muhimu, kama jihadi n.k., hakufichiki kwa Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa wanafiki walikuwa wakiondoka kwenye vikao vya Mtume (s.a.w.) kwa kujiziba na wengine.

Basi na watahadhari wale ambao wanahalifu amri yake isije ikawap- ata fitna au ikawapata adhabu chungu.

Amri yake hapa ni amri ya Mungu na makusudio ya fitna hapa ni balaa duniani. Hii ni hadhari na ahadi ya adhabu duniani na akhera kwa mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Ehee! Hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika yeye anajua mliyo nayo. Na siku watakaporudishwa kwake atawaeleza waliyoyafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Mwenyezi Mungu hawahitajii walimwengu. Twaa ya mtiifu haimfai chochote, wala uasi wa muasi haumdhuru chochote.

Yeye ni mjuzi wa yanayokuwa nyoyoni na wa siku ambayo watu watakusanyika ndani yake kwa hisabu. Atawapa habari ya matendo yao na makusudio yao na watapata wanayostahiki wala Mola wako hamdhulumu yoyote.