read

Aya 1-6: Amemteremshia Furqani Mja Wake

Maana

Amekuwa na baraka yule ambaye ameiteremsha Furqani kwa mtumwa wake, ili awe muonyaji kwa walimwengu wote.

Baraka na neema za Mwenyezi Mungu ni nyingi. Katika zilizojitokeza ni hii Qur'an ambayo ameiteremsha kwa mtumwa wake Muhammad (s.a.w.). Kwani inaongoza kwenye msimamo na inatoa onyo la adhabu chungu.

Neno Furqani lina maana ya kufarikisha baina ya haki na batili. Makusudio yake hapa ni Qur'an. Mwenyezi Mungu amemsifu kwa utumwa uliotegemezwa kwake yeye Mungu, kwa sababu ya kumwadhimisha. Kwani aliye adhimu zaidi katika watu ni yule ambaye hamnyenyekei wala kumdhalilikia isipokuwa yule anayestahiki hivyo.

Na dhalili zaidi na mpuzi kuliko watu wote ni yule anayemdhalilikia au kumtukuza asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (15:1).

Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakufanya mtoto, wala hakuwa na mshirika katika ufalme.

Hii ni kuwarudi warabu wa wakati wa ujahiliya, waliomshirikisha Mwenyezi Mungu na wanaswara waliosema kuwa Masih ni mwana wa Mungu. Njia ya kuwarudi ni kuwa ulimwengu na viliyvomo ndani yake ni miliki ya Mwenyezi Mungu, na anayemilikiwa hawezi kuwa mshirika wa mmliki wala mtoto wake.

Na ameumba kila kitu na akakikadiria kipimo kwa sababu zake, mpangilio wake na nidhamu yake; kwa namna ambayo kitatekeleza wad- hifa wake kwa njia ya ukamilifu. Kimsingi ni kuwa sadfa haina nafasi katika mipangilio, nidhamu na hekima na hawezi kuikimblia isipokuwa mjinga au mwenye inadi.

Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii dhara wala nafuu, wala haimiliki mauti wala uhai wala kufufuka.

Mambo ya dhahiri yanajulikana na mjuzi na asiyekuwa mjuzi. Kwa maumbile yake mtu, anayatambua tu, bila ya kuhitajia dalili; bali hayo yenyewe ni dalili ya mengine. Miongoni mwa mambo yaliyo wazi ni Mungu. Ni laz- ima awe ni muweza wa kuumba, kunufaisha na kudhuru. Vile vile kuleta uhai, kufisha na kufufua baada ya mauti. Masanamu mnayoyaabudu enyi washirikina hayawezi hayo, basi vipi yanaweza kuwa miungu.

Ilivyokuwa hoja hii inawazima washirikina na kutowapa nafasi ya kukana na kuijadili, walikimbilia kwenye uzushi na wamesema wale ambao wamekufuru:

“Haikuwa hii ni chochote ila ni uzushi aliozua, na wamemsaidia haya watu wengine.”

Hii wanakusudia Qur'an na aliouzua wanamkusudia Muhammad (s.a.w.).
Qur'an ilipowabana maadui wa haki, walianza kusema kuwa Qur'an imetengenezwa na Muhammad na mkusanyiko wake wa visa unatokana na watu wa kitabu waliomsaidia Muhammad kisha yeye akaipanga kwa ufasaha na kuinasibisha kwa Mwenyezi Mungu, akiwa na lengo la kupata ukubwa na kuwa juu ya watu wote.

Waliozua uzushi huu ndio hasa wapenda makuu, wanaojiweka juu ya watu wote na kuwakandamiza mafukara na wanyonge. Walizua uzushi huu wakiwa na hakika kuwa Muhammad ni mkweli mwaminifu na kwamba Qur'an haifanani na maneno ya binadamu. Hapo mwanzo alishindana nao na kuwaambia walete angalau Sura moja tu inayofanana na Qur'an, lakini wakashindwa.

Ikiwa Muhammad anasaidiwa na watu wa Kitabu, basi wao si ndio wangesaidiwa kwanza na mayahudi, kwa sababu waliungana nao dhidi ya Muhammad na waislamu.

Kwa vile hawana la kufanya, hawana hoja ya kuikabili hoja, sasa wafanyeje, wasalimu amri na kuingia kwenye Uislamu? Wataingiaje Uislamu nao unawamuweka sawa mwinyi wa kiquraishi na mtumwa wa kihabeshi, wala hakuna ubora wa kiumbe juu ya kiumbe mwenzake isipokuwa kwa takua; na unaharamisha dhulma na unyanyasaji, mambo ambayo ndiyo maisha ya wapinzani hawa?

Kwa hiyo basi hakuna nyenzo ya kulinda maisha yao haya isipokuwa uzushi, kusema Muhammad ni mchawi, ni muongo, ni mwendawazimu na kwamba Qur'an ni ngano za watu wa kale alizozikusanya Muhammad kutoka hapa na pale.

Basi hakika wamekuja na dhulma na uzushi.

Wameleta dhulma kubwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kwa nafsi zao pia. Kwa sababu wameziingiza kwenye maangamizi. Pia wameleta uzushi kuwa Qur'an ni uzushi. Neno dhulma na uzushi linafa- hamisha kwamba wao wamenasibisha uzushi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) wakiwa wanajijua kuwa wao ni waongo.

Kwa hakika wanavyojasiri leo, maadui wa Uislamu, kusema kuwa chimbuko la Qur'an ni Tawrat na Injil, kumetokana na madhalimu na wazushi waliokuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na kwamba msukumo wa dhulma hii na kuvunga huku ni kwa aina moja; ambayo ni kuhofia haki kuwafedhehi hawa na wale na kufichua maovu yao.

Na wakasema: "Hizi ni ngano za wa kale anazoziandikisha anazosomewa asubuhi na jioni."

Wazushi walipigwa na butwaa wasijue la kufanya. Wakafikiriaje, waeneze uvumi kuwa Muhammad amesoma elimu ya Qur'an kwa mwingine? Lakini ni nani atakayewaamini na watu wote wanajua kuwa Muhammad hasomi wala haandiki (ummiy)?

Ndio wakapata njia nyingine - Qur'an si chochote isipokuwa ni visa vya watu wa kale alivyoandikiwa Muhammad na kusomewa mara kwa mara mpaka akavihifadhi, kisha akavileta kwa mfumo mzuri na kuvitangaza kwa watu kuwa vinatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hivi ndivyo wafanyavyo watu wenye malengo mengine kila wakati. Wanaeneza na kuwazulia watu wema wanaotaka kuleta ukombozi; si kwa lolote ila ni kwa kuhofia chumo lao la kidhalimu, lakini watakimbila wapi? Je, mwangaza wajua unaweza kuzimwa na pumzi za mdomo? Je, uongo unaweza kubadilisha uhakika? Muongo analaaniwa na kila ulimi na atafedheka hata kama atasitiriwa na mapazia elfu.

Sema, ameiteremsha ajuae siri za mbinguni na ardhini.

Sema ewe Muhammad: Hapana! Hii si visa na ngano za watu wa kale, wala haikuchukuliwa kwenye Tawrat na Injil. Ni ilimu na nuru, aliyoiteremsha moyoni mwako ili uwaongoze kwayo, vizazi na vizazi, kwenye haki, heri na uadilifu. Inatoka kwa mwenye hekima, mjuzi wa siri za ulimwengu na yaliyo na masilahi na uharibifu kwa viumbe. Na wewe unawafikishia kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale yaliyo na heri yao na shari yao na uokovu wao na maangamizi yao.
Hakika Yeye amekuwa ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.

Anamrehemu aliyeasi kwa kupuuza, pamoja na kumhadharisha na kumuonya. Wala hamfanyii haraka mkosaji; huenda akarudia kwa Mola wake na kutubia dhambi zake.

Akifanya hivyo atamsamehe yaliyopita; vinginevyo atapata malipo yake na adhabu chungu anayostahiki.

وَقَالُوا مَالِ هَٰذَا الرَّسُولِ يَأْكُلُ الطَّعَامَ وَيَمْشِي فِي الْأَسْوَاقِ ۙ لَوْلَا أُنْزِلَ إِلَيْهِ مَلَكٌ فَيَكُونَ مَعَهُ نَذِيرًا {7}

Na wakasema: Ana nini Mtume huyu anakula chakula na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa malaika awe muonyaji pamoja naye?

أَوْ يُلْقَىٰ إِلَيْهِ كَنْزٌ أَوْ تَكُونُ لَهُ جَنَّةٌ يَأْكُلُ مِنْهَا ۚ وَقَالَ الظَّالِمُونَ إِنْ تَتَّبِعُونَ إِلَّا رَجُلًا مَسْحُورًا {8}

Au akaangushiwa hazina, au awe na bustani ale katika hiyo? Na wakasema madhalimu: Hamumfuati ila mtu aliyerogwa.

انْظُرْ كَيْفَ ضَرَبُوا لَكَ الْأَمْثَالَ فَضَلُّوا فَلَا يَسْتَطِيعُونَ سَبِيلًا {9}

Tazama jinsi wanavyokupigia mfano, basi wamepotea, wala hawataiweza njia.

تَبَارَكَ الَّذِي إِنْ شَاءَ جَعَلَ لَكَ خَيْرًا مِنْ ذَٰلِكَ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَيَجْعَلْ لَكَ قُصُورًا {10}

Amekuwa na baraka yule ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo, mabustani yapitayo mito chini yake na akujaalie makasri.

بَلْ كَذَّبُوا بِالسَّاعَةِ ۖ وَأَعْتَدْنَا لِمَنْ كَذَّبَ بِالسَّاعَةِ سَعِيرًا {11}

Bali wameikanusha saa. Na tumemwandalia moto mkali mwenye kuikanusha saa.

إِذَا رَأَتْهُمْ مِنْ مَكَانٍ بَعِيدٍ سَمِعُوا لَهَا تَغَيُّظًا وَزَفِيرًا {12}

Utakapowaona katika mahali pa mbali watasikia hasira yake na mngurumo wake.

وَإِذَا أُلْقُوا مِنْهَا مَكَانًا ضَيِّقًا مُقَرَّنِينَ دَعَوْا هُنَالِكَ ثُبُورًا {13}

Na watakapotupwa humo, mahali palipo finyu hali wamefungwa, ndipo hapo wataomba mauti.

لَا تَدْعُوا الْيَوْمَ ثُبُورًا وَاحِدًا وَادْعُوا ثُبُورًا كَثِيرًا {14}

Msiyaombe mara moja bali ombeni mauti mara nyingi

قُلْ أَذَٰلِكَ خَيْرٌ أَمْ جَنَّةُ الْخُلْدِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ ۚ كَانَتْ لَهُمْ جَزَاءً وَمَصِيرًا {15}

Sema, je, hayo ni bora au Bustani ya milele, ambayo wameahidiwa wenye takua, iwe kwao malipo na marejeo?

لَهُمْ فِيهَا مَا يَشَاءُونَ خَالِدِينَ ۚ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ وَعْدًا مَسْئُولًا {16}

Watapata humo wayatakayo, wakae humo milele. Ni ahadi juu ya Mola wako ya kuombwa.