Aya 7 – 16: Anakula Chakula Na Kutembea Masokoni
Maana
Hekima ya Mwenyezi Mungu kupeleka mitume kwa watu ni kuwabainishia yale yaliyo na maslahi kwao na yaliyo na uharibifu, ili waweze kujua mambo yao vizuri na iwe ni hoja ya Mwenyezi Mungu kwao Siku ya Malipo na Hisabu. Hekima hii haiwezi kuhakikika ila akiwa huyo mtume ni wa aina moja na watu katika maisha yake, maumbile yake na hisia zake.
Lau angelikuwa wa jinsi nyingine, basi wangelimkimbia wala wasingelimtegemea; isipokuwa yule anayefanana na wao; akizungumza wanayozungumza wao, akifanya wanayofanya wao na akiathirika kama wanavyoathirika wao.
Hata hivyo, ni lazima Mtume awe na ukamilifu wa juu anaoweza kuufikia binadamu, katika mipaka ya ubinadamu kwa sifa zake na uwezo wake. Kwa sababu ukamilifu ndio nguvu tekelezi ya ujumbe wake na mafunzo yake. Tazama Juz. 16 (20:17 - 35).
Baada ya utangulizi huu, tuangalie kauli za washirikina na kupinga kwao utume wa Muhammad (s.a.w.) ambazo ni :
1. Na wamesema: Ana nini Mtume huyu anakula chakula na anatembea masokoni.
Wanataka aishi kwenye nyumba ya kifahari na azungukwe na walinzi; kama wafanyavyo watawala. Hawajui au wanajitia kutojua kuwa mtekelezaji wa risala yoyote, awe Mtume au mwengineo, haiwezekani kutekeleza risala yake ila akiwa pamoja na watu, katika tajruba zao na kazi zao. Vipi watamwitikia ikiwa atawawekea kizuizi au kuwa kwenye ulimwengu mwingine.
2. Mbona hakuteremshiwa malaika awe muonyaji pamoja naye?
Maoni ya washirikina ni kuwa Muhammad (s.a.w.) awe pamoja na malaika. Si ajabu hilo kwa wale ambao wanamfanyia Mwenyezi Mungu washirika, sembuse Muhammad, watampinga tu akiwa hana mshirika kati- ka kutekeleza risala yake. Kabla yao Firauni alimsema Musa (a.s.):
فَلَوْلَا أُلْقِيَ عَلَيْهِ أَسْوِرَةٌ مِنْ ذَهَبٍ أَوْ جَاءَ مَعَهُ الْمَلَائِكَةُ مُقْتَرِنِينَ {53}
"Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu au kuja malaika pamoja naye wakimwandama? (43:53).
Mantiki Ya Watu Wa Pesa Ni Benki Na Ardhi
3. Au akaangushiwa hazina au awe na bustani ale katika hiyo.
Haya ndiyo mantiki ya watu wa pesa: Benki na ardhi. Vipi wataweza kumwamini anayesema kuwa hakuna ubora baina ya mwarabu na asiyekuwa mwarabu isipokuwa kwa takua, na wanasema kuwa ubora kwao ni mali, bila ya kutoka jasho? Yule anayetoka jasho kwao ni mtumwa, anatakikana asikilize na kutii amri. Vipi Mwenyezi Mungu amchague Muhammad na kumfadhilisha kuliko watu wengine naye ni fukara? Lau angelikuwa amechaguliwa, kama anavyodai, basi angeliteremshiwa hazina ya pesa au akawa na bustani ambayo hakuitolea jasho.
Hali hii bado inaendelea hadi leo. Serikali katika nchi nyingi ni za wenye mashirika na viwanda au zinasimamiwa na wale waliowachagua kulinda maslahi yao. Tazama Juz. 15 (17: 90 - 96), kifungu cha 'Kufikiria mali.'
4. Na walisema madhalimu -kuwambia waumin- hamumfuati ila mtu aliyerogwa.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17: 101).
Tazama jinsi wanavyokupigia mfano kwamba wewe ni fukara na umerogwa. Basi wamepotea, wala hawataiweza njia ya kubatilisha utume wako na kukurudi kwa hoja na dalili.
Alivyo Mjinga Aliyehadaika
Walikadhibisha risala ya Muhammad (s.a.w.) wakampa sifa za uzushi, wakawa wao ndio wazushi. Kwa sababu mwenye kumwambia mjuzi kuwa ni mjinga, na mwenye ikhlasi kuwa ni mhaini, basi amejisema yeye mwenyewe kuwa ni mjinga na ni mhaini.
Kwa hiyo basi mifano waliyompigia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) ni ushahidi na mfano wa ujinga wao, uzushi wao na inadi yao, lakini wao hawatambui; sawa na anayejiangalia kwenye kioo akaona ubaya akafikiria ubaya uko ndani ya kioo, sio katika sura yake.
Amekuwa na baraka yule ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo, mabustani yapitayo mito chini yake na akujaalie makasri.
Ambaye ameumba ulimwengu pamoja na ardhi yake na mbingu yake, hawezi kushindwa kumpa Mtume wake mtukufu mali nyingi, lakini utukufu mbele ya Mwenyezi Mungu haupimwi kwa mali; isipokuwa unapimwa kwa takua na amali njema na malipo ya wenye takua na wema ni neema na raha ya daima. Maisha ya duniani, si kitu cha maana kwa Mwenyezi Mungu kuwapa mawalii wake.
Kuna Hadith isemayo: "Lau dunia ingelikuwa inapimwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ubawa wa mbu, basi asingelikunywa kafiri hata tama moja la maji."
Bali wameikanusha saa.
Saa ni saa ya Kiyama. Walikanusha utume wa Muhammad (s.a.w.) wakaleta sababu kuwa yeye ni fukara na amerogwa, wakiwa wanajidanganya.
Lengo lao kuu ni kuhofia masilahi na manufaa yao na wakasema hakuna ufufuo, ili wasiaambiwe kuwa wameathirika na yanayokwisha wakaacha yanayobakia.
Kila mwenye kupima ubora kwa mali na akaathirika nayo kuliko radhi ya Mwenyezi Mungu, basi atakuwa katika hukumu ya mwenye kukanusha kukutana na Mwenyezi Mungu hata kama atakuwa anamwamini kinadharia.
Na tumemwandalia moto mkali mwenye kuikanusha saa. Utakapowaona katika mahali pa mbali watasikia hasira yake na mngurumo wake.
Imesekana kuwa utakaoona, kuwa na hasira na kuunguruma ni moto. Wengine wakasema ni watunzaji wa moto. Pia ikasemekana kuwa Mwenyezi Mungu kesho ataufanya moto uwe na uhai na akili. Tuonavyo sisi ni kuwa hicho ni kinaya cha adhabu kali na vituko vikubwa.
Na watakapotupwa humo, mahali palipo finyu hali wamefungwa, ndipo hapo wataomba mauti. Msiyaombe mara moja bali ombeni mauti mara nyingi.
Moto wa Mwenyezi Mungu hauwi finyu; kama ilivyoweka wazi hilo kauli yake Mwenyezi Mungu:
يَوْمَ نَقُولُ لِجَهَنَّمَ هَلِ امْتَلَأْتِ وَتَقُولُ هَلْ مِنْ مَزِيدٍ {30}
Kwa hiyo makusudio ya ufinyu wa moto ni ufinyu wa watu wa motoni watakaona dhiki na kuchukia kuingia humo. Aliulizwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kuhusu Aya hii, akasema:
"Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake! Hakika wao watachukia kama inavyochukia nguzo kwenye ukuta" yaani wataingia kwa kulazimishwa. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 13 (14: 46 -52) kifungu cha 'Jahnnam na silaha za maangamizi.'
Sema, je, hayo ni bora au Bustani ya milele, ambayo wameahidiwa wenye takua, iwe kwao malipo na marejeo? Watapata humo wayatakayo, wakae humo milele. Ni ahadi juu ya Mola wako ya kuombwa.
Neno 'juu ya' linafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amejilazimishia kutekeleza ahadi yake. Katika Tafsir Ar-Razi kuna melezo haya: "Ikisemwa kuwa adhabu ni bora au Pepo ni kama kumwambia mwenye akili kuwa sukari ni tamu au shubiri (subili)? Tutajibu: Hii inafaa katika hali ya kukaripia; kama vile mtu akimpa mtumwa wake mali kisha akawa na kiburi akampiga pigo la kuumiza huku akimwambia, hii ni tamu au ile."
وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ وَمَا يَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ فَيَقُولُ أَأَنْتُمْ أَضْلَلْتُمْ عِبَادِي هَٰؤُلَاءِ أَمْ هُمْ ضَلُّوا السَّبِيلَ {17}
قَالُوا سُبْحَانَكَ مَا كَانَ يَنْبَغِي لَنَا أَنْ نَتَّخِذَ مِنْ دُونِكَ مِنْ أَوْلِيَاءَ وَلَٰكِنْ مَتَّعْتَهُمْ وَآبَاءَهُمْ حَتَّىٰ نَسُوا الذِّكْرَ وَكَانُوا قَوْمًا بُورًا {18}
فَقَدْ كَذَّبُوكُمْ بِمَا تَقُولُونَ فَمَا تَسْتَطِيعُونَ صَرْفًا وَلَا نَصْرًا ۚ وَمَنْ يَظْلِمْ مِنْكُمْ نُذِقْهُ عَذَابًا كَبِيرًا {19}
وَمَا أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ إِلَّا إِنَّهُمْ لَيَأْكُلُونَ الطَّعَامَ وَيَمْشُونَ فِي الْأَسْوَاقِ ۗ وَجَعَلْنَا بَعْضَكُمْ لِبَعْضٍ فِتْنَةً أَتَصْبِرُونَ ۗ وَكَانَ رَبُّكَ بَصِيرًا {20}