read

Aya 17 – 20: Siku Atakapowakusanya Na Wanayoyaabudu

Maana

Na siku atakapowakusanya na wale wanaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu na atasema: Je, nyinyi mmewapoteza waja wangu hawa au ni wao wenyewe walipotea njia.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika Aya zilizotangulia, amewataja washirikina na kuli zao kumhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu na yale mambo watakayokumbana nayo kesho, ikiwa ni pamoja na adhabu ya kuunguzwa.

Katika Aya tuliyo nayo, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametaja kwamba Yeye, siku ya Kiyama, atawakusanya washirkina na wale waliowafanya ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliulize lile kundi liloabudiwa mbele ya wale waliowashirikisha. Lengo la swali hili ni kuwanyamazisha washirikina na kusisitiza hoja juu yao iliyowalazimu kupitia kwa Manabii na Mitume.

Watasema: Umetakasika na upungufu! Haikutupasa sisi kuwafanya mawalii badala yako.

Kundi lililoabudiwa litajibu: 'Umetakasika na umetukuka na shirki ewe Mola wetu! Vipi tutake tuabudiwe na hali sisi tunakupwekesha wewe, tunakuabudu na kukufanyia ikhlasi?

Pia tunaogopa adhabu na kutaraji thawabu zako wala hatumtaki msaada asiyekuwa wewe? Kwenye jawabu hili pia kuna kutahayariza, kama ilivyo katika swali.

Lakini uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau ukumbusho na wakawa ni watu walioangamia.

Bado wale walioabudiwa wanaendelea kusema. Maana yake ni kuwa sisi hatukuwapoteza washirikina, lakini hekima yako, ewe Mola wa ulimwengu, imepitisha kuwapa muda wao na baba zao na kuwaneemesha kwa umri mrefu, mali na watoto, ili waweze kutubia na kuomba msamaha, lakini waliuacha, wakaiendea dunia na ladha zake, wakawa ni wenye kuangamia kwa sababu ya uzembe wao na uchaguzi wao mbaya.

Hakika wamewakadhibisha kwa mliyoyasema. Kwa hiyo hamuwezi kujiondolea wala kujisaidia.

Maneno yanatoka kwa Mwenyezi Mungu kuelekea kwa washirikina.

Maana ni kuwa, enyi washirikina! Mlikuwa mkisema kuwa tunawaabudu hao ili watuombee kwa Mwenyezi Mungu na watuwekee karibu naye, sasa je, mmeona? Wamejitenga nanyi na wamewakana mnayoyasema na mambo yenu ya ubatilifu. Adhabu ndio hii sasa inawashukia hakuna wa kuwakinga nayo wala kuwasaidia.

Na atakayedhulumu miongoni mwenu tutamuonjesha adhabu kubwa.

Hakuna kitu kikubwa na adhimu kuliko moto wa Jahannam, na ndiyo malipo ya kila dhalimu na mwenye hatia.

Na hatukuwatuma kabla yako mitume ila kwa hakika walikuwa wakila chakula na wakitembea masokoni.

Washirikina walimkana Muhammad (s.a.w.) kwa kuwa anakula chakula na kutembea sokoni. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawarudi kwa kuwaambia kuwa kuna ajabu gani ya hilo? Mitume wote waliokuwa kabla yake walikuwa wakila chakula na kutembea kwenye masoko, wakiwemo wale mnaoitakidi utume wao; kama Ibrahim na Ismail (a.s.). Rudia Aya 8 ya Sura hii.

Na tumewajaalia badhi yenu wawe mtihani kwa wengine.

Mwenyezi Mungu anawatahini waja wake, akiwa anawajua zaidi, ili visidhihirike vitendo vinavyostahiki thawabu na adhabu; kama alivyosema Imam Ali (a.s.). “Miongoni mwa mambo anayowatahini nayo waja wake na yaliyo wazi zaidi ni kuwapelekea Mitume, kuwabashiria na kuwaonya. Atakayewaamini, kuwasikiliza na kutii, basi atastahiki thawabu na atakayekufuru na kufanya inadi basi atastahiki adhabu.”

Kwa hiyo kupatikana mitume, kama wabashiri na waonyaji ni mtihani kwa waumini na makafiri na ni sababu ya kudhihiri hakika ya makundi hayo mawili.

Vile vile kupatikana makafiri na wanafiki ni mtihani kwa manabii. Kwa vile washari na wafisadi hawawachi wakombozi, bali wanajaribu kuwaudhi kwa kila njia, bali wanawazushia mambo, kuleta uvumi na njama; sawa na washirikina walivyomfanyia Mtume (s.a.w.) na hivi sasa vibaraka wanaolipwa wanavyowafanyia wakombozi wenye ikhlasi.

Historia ya mapambano baina ya haki na batili inaanzia na mwanzo wa binadamu. Qabil alimuua Habil pamoja na kuwa walitokana na tone moja la manii na mfuko mmoja wa uzazi, si kwa lolote ila ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikubali amali ya Habil kwa wema wake na hakuikubali ya Qabil kwa ufisadi wake.

Je, mtakuwa na subira?

Yaani enyi waumini kuweni na uthabiti kwenye haki wala msiwajali wabatilifu na uongo wao.
Na Mola wako ni Mwenye kuona yule anayewazulia wema na yule anayethibiti kwenye haki kwa matokeo yoyote yatakayokuwa na atamlipa kila mmoja stahiki yake.