Aya 76 – 85: Qur’an Inasimulia
Maana
Nembo Ya Israil Ni: ‘Tumesikia Na Tumeasi’
Hakika hii Qur’an inawasimulia wana wa Israil mengi wanayohitalifiana.
Qur’an imezungumzia na kuyakariri mambo ya kushangaza ya wana wa Israil. Imezungumzia mambo yanayohusiana nao, nembo yao na yale waliyohitalifiana wakati wa Nabii Musa na baadaye.
Nembo yao wanayoifuata bila ya kuicha ni: ‘Tumesikia na tumekataa,’ kama ilivyoelezwa katika Juz. 1(2:93) na Juz. 5 (4:46). Yaani tumemsikia Mwenyezi Mungu na mtume wake na tumemuasi Mwenyezi Mungu na mitume wote. Waliendelea na nembo hii wakati wa Nabii Musa (a.s.) mpaka akawashtakia kwa Mola wake na akawapa sifa ya ufuska, akisema kwa masikitiko:
رَبِّ إِنِّي لَا أَمْلِكُ إِلَّا نَفْسِي وَأَخِي ۖ فَافْرُقْ بَيْنَنَا وَبَيْنَ الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ {25}
Katika Aya nyingine amewapa sifa ya upumbavu:
قَالَ رَبِّ لَوْ شِئْتَ أَهْلَكْتَهُمْ مِنْ قَبْلُ وَإِيَّايَ ۖ أَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ السُّفَهَاءُ مِنَّا ۖ {155}
Bado wanaendelea na nembo yao hii hadi leo. Mnamo mwaka 1967, Umoja wa Mataifa, unaowakilisha mataifa yote duniani, kuanzia mashariki hadi magharibi, ulipitisha azimio la kuitaka Israil ijiondoe katika ardhi ya Quds.
Jibu la mjumbe wake lilikuwa ni: “Umoja wa Mataifa ni debe la takataka,” kama ilivyonukuliwa katika magazeti.
Ama yale ambayo walihitilafiana ni walivyoifanyia Tawrat wakati wa Musa mpaka Mwenyezi Mungu akawainulia jabali na kuwatishia kuwaangamiza:
وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَكُمْ وَرَفَعْنَا فَوْقَكُمُ الطُّورَ خُذُوا مَا آتَيْنَاكُمْ بِقُوَّةٍ وَاسْمَعُوا ۖ قَالُوا سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا {93}
Walihitalifiana katika mitume waliokuja baada ya Musa (a.s.). Miongoni mwao ni Bwana Masih (a.s.), kundi moja lilimkadhibisha na kundi moja likataka kumuua; kama ilivyoelezwa katika Juz. 1 (2:87).
Vilevile walihitalifiana kuhusu utume wa Muhammad. Hawakumwamini isipokuwa wachache. Kama wangelikuwa ni watafutaji kweli wa haki wangeliafikiana kuichukua Qur’an ambayo imesimama kwa dalili na hoja juu ya ukweli wake.
Nayo hakika ni uongofu na rehema kwa waumini.
Ni uongofu kwa mwenye kutaka kuongoka na rehema kwa kutumia hukumu zake na mafunzo yake.
Hakika Mola wako atakata baina yao hukumu yake naye ni mwenye nguvu, Mjuzi.
Siku ya Kiyama batili zitaondoka na Mwenyezi Mungu atawahukumu waisrail na wengineo katika yale waliyohitalifiana katika mambo ya dini na dunia.
Basi mtegemee Mwenyezi Mungu.
Mwenye kukimbilia kwake basi yuko katika ngome imara na kizuizi cha nguvu.
Hakika wewe uko kwenye haki iliyo wazi.
Na mwenye haki hajali yanayosemwa juu yake.
Kwa hakika wewe huwezi kuwasikilizisha wafu wala kuwasikilizisha viziwi wanapogeuka kurudi nyuma. Wala huwezi kuwaongoza vipofu na upotevu wao.
Jumla hizi zina lengo moja, kwamba kuna sifa zinazoua moyo na kumfanya mtu anga’ang’anie ukafiri, unafiki na upotevu. Zinamfanya yeye na maiti ni sawasawa; hafaidiki na mawaidha wala maonyo. Miongoni mwa sifa kuu hizo ni tamaa na pupa ya chumo na cheo.
Maana haya yamekaririka kwa mifumo mbalimbali; miongoni mwayo ni Aya hizi zifuatazo:-
Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi. Hao ndio walioghafilika. Juz. 9 (7:179).
Je, wewe unaweza kuwasikilizisha viziwi ingawa hawafahamu? ... Je, wewe unaweza kuwaogoza vipofu ingawa hawaoni? Juz.11 (10 42–43).
Huwezi kuwasikilizisha ila wale wanaoziamini ishara zetu, basi hao ndio watiifu.
Anayekusikiliza na kukutii wewe Muhammad ni yule anayeitafuta haki kwa ajili ya haki, kiasi ambacho akipata dalili na hoja anaiamini na kuifuata. Ama watu wa masilahi na tamaa wanakupa mgongo.
Na itakapowaangukia kauli juu yao, tutawatolea mnyama katika ardhi atakayewasemeza, kwamba watu walikuwa hawana yakini na ishara zetu.
Kuwaangukia, ni kuwathibitikia. Makusudio ya kauli hapa ni yale aliyoyaahidi Mwenyezi Mungu ya kutokea Kiyama. Makusudio ya watu ni makafiri.
Ama kuhusu mnyama, maneno yamekuwa mengi kumuhusu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakutubainishia ni yupi. Pia Hadith kutoka kwa maasum hazikuthibiti; hata kama mapokezi yake yatasihi hatuwezi kuitumia, kwa sababu itakuwa imekuja kwa njia moja (Khabarul-waahid) ambayo inakuwa hoja katika hukumu tanzu, si katika maudhui na misingi ya kiitikadi. Na kusema bila ya elimu ni haramu.
Kwa hiyo hakuna kilichobakia isipokuwa kuchukulia dhahiri ya Aya ambayo inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atakapowafufua watu kwa ajili ya hisabu atamtoa kiumbe kutoka ardhini atakayetangaza kuwa makafiri walizikana dalili wazi wazi na hoja mkataa za kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na mitume wake.
Unaweza kuuliza, kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakubainisha hakika ya mnyama huyu akawaacha watu wameduwaa, mpaka wengine wakasema bila ya elimu na kuwazia tu?
Jibu: Lengo la kutajwa ni kuwatangaza makafiri na kwamba wao watafufuliwa kesho wakiwa madhalili wamefedheheka mbele ya ushahidi. Lengo hili linapatikana kiasi cha kudokeza tu kuwa kutakuwa na mnyama hata kama jina lake halijulikani wala hakika yake. Aya hii inafanana na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Siku ambayo nyuso zitang’aa na nyuso (nyingine) zitasawijika.” Juz. 4 (3:106).
Na siku tutakapowakusanya watu kutoka kila umma, kundi katika wanaokadhibisha ishara zetu.
Neno‘katika’nilakubainishasiolabaadhi;nikamamfanowakauliyake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Jiepusheni na uchafu katika mizimu.” akimaanisha mizimu yote sio baadhi.
Maana ni kuwa katika kila umma kuna wanaosadikisha ishara za Mwenyezi Mungu na wenye kuzikadhibisha. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kesho atawakusanya wakadhibishaji wote kwa ajili ya hisabu na malipo. Inajulikana wazi kuwa Mwenyezi Mungu atawakusanya wasadikishaji na wakadhibishaji, lakini lengo la kutajwa wakadhibishaji ni ukemeo na kiaga.
Nao watagawanywa mafungu mafungu.
Malaika watawazuia kuumeni na kushotoni na watawachunga kwenda kwenye kisimamo, kama wanyama wakipelekwa machinjioni.
Hata watakapofika, atasema: Je, nyinyi si mlizikanusha ishara zangu pasipokuzijua vyema, au mlikuwa mkifanya nini?
Watakaposimama wakanushaji mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu atawaambia kwa kuwatahayariza, kwa nini mmewakadhibisha mitume wangu na kuacha kuitikia mwito wao? Ikiwa hamkujua ukweli wao kwanini mlipinga dalili za kuwajulisha na msiziangalie kwa mtazamo wa mwenye kutafuta haki kwa njia ya haki? Ni lipi lilo muhimu zaidi ya hilo?
Maulamaa wameafikiana, kwa kauli moja, kuwa akili inahukumiwa kwa wajibu wa kuangalia muujiza wa mwenye kudai utume. Wakasema: Akili haisamehewi kwa lile ambalo ni wajibu ikiwa inaweza kufanya utafiti na kupata maarifa. Kuna Hadith isemayo: “Mja ataambiwa siku ya Kiyama, je ulijua? Akisema, ndio, Ataulizwa tena, je ulifanya? Akisema sikujua (namna ya kufanya), ataulizwa, je ulijifundisha?
Na kauli itawaangukia juu yao kwa vile walivyodhulumu.
Ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu itawapata kwa sababu ya kufuru yao na uzembe wao wa kufanya utafiti na kuuliza.
Basi hao hawatasema lolote, kwa sababu ya kukatikiwa na hoja na mshangao wao kutokana na vituko vya siku ya Kiyama.
أَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا اللَّيْلَ لِيَسْكُنُوا فِيهِ وَالنَّهَارَ مُبْصِرًا ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ {86}
وَيَوْمَ يُنْفَخُ فِي الصُّورِ فَفَزِعَ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَمَنْ فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَنْ شَاءَ اللَّهُ ۚ وَكُلٌّ أَتَوْهُ دَاخِرِينَ {87}
وَتَرَى الْجِبَالَ تَحْسَبُهَا جَامِدَةً وَهِيَ تَمُرُّ مَرَّ السَّحَابِ ۚ صُنْعَ اللَّهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ ۚ إِنَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَفْعَلُونَ {88}
مَنْ جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِنْهَا وَهُمْ مِنْ فَزَعٍ يَوْمَئِذٍ آمِنُونَ {89}
وَمَنْ جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَكُبَّتْ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ هَلْ تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {90}
إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ رَبَّ هَٰذِهِ الْبَلْدَةِ الَّذِي حَرَّمَهَا وَلَهُ كُلُّ شَيْءٍ ۖ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ {91}
وَأَنْ أَتْلُوَ الْقُرْآنَ ۖ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ ضَلَّ فَقُلْ إِنَّمَا أَنَا مِنَ الْمُنْذِرِينَ {92}
وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ سَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ فَتَعْرِفُونَهَا ۚ وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ {93}
- 1. Yakushangaza ni yale niliyoyasoma yaliyonukuliwa kutoka katika Kitabu Talmud, ambacho kwa Mayahudi wengi wanakiona ni kitabu kilichoteremshwa kama Tawrat: “Hakika Mwenyezi Mungu akiteremsha suala gumu huwashauri marabi wakuu kulitatua. Siku moja Mwenyezi Mungu alitoa rai kimakosa, mmoja wa marabi wakuu akagundua kosa hilo na Mungu akakubali.”