read

Aya 86 – 93: Milima Inakwenda Mwendo Wa Mawingu

Maana

Je, hawaoni kwamba tumeufanya usiku ili watulie na mchana wa kuangaza. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wenye kuamini.

Imetangulia pamoja na tafsiri yake katika Juz. 11 (10:67).
Na siku itakapopuziwa parapanda, watafazaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila amtakaye Mwenyezi Mungu.

Parapanda itapuziwa kutangaza Kiyama, nyoyo za viumbe zitashtuka, kutokana na mpuzio huo, kwa hofu kuu; isipokuwa nyoyo za Mitume wasadikishaji, mashahidi na watu wema ambao Mwenyezi Mungu amewavua kwa kusema: ‘Ila amtakaye Mwenyezi Mungu.’ Hao aliowavua amewashiria katika kauli yake:

وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ مِنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ ۚ وَحَسُنَ أُولَٰئِكَ رَفِيقًا {69}

“Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, basi hao (watakuwa) pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii na wasadikishaji na mashahidi na watu wema. Na hao ndio marafiki wema.” Juz. 5 (4:69).

Katika baadhi ya tafsiri imeelezwa kuwa Parapanda itapulizwa mara tatu; Mpulizo wa fazaa, wa kufa watu wote na ule wa ufufuo. Ufufuo wa kwanza unafahamishwa na Aya tuliyo nayo, wa pili na wa tatu unafahamishwa na Aya isemayo: “Na itapulizwa parapanda, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhini, ila aliyemtaka Mwenyezi Mungu. Kisha itapulizwa mara nyingine. Hapo watainuka wawe wanangojea.”

Na wote watamfikia nao ni wanyonge.

Yaani hao wanaohofia watafufuliwa kwa Mola wao wakiwa dhalili.

Milima Na Harakati Za Ardhi

Na unaiona milima unaidhania imetulia nayo inakwenda mwendo wa mawingu.

Maudhui ya Aya hii na iliyo kabla yake ni mamoja, kuzungumzia Kiyama na vishindo vyake. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ataing’oa milima kutoka sehemu zake na kuiendesha angani, sawa na yanavyopita mawingu, lakini mtu atafikiria kuwa imetulia.

Hiyo inatokana na kuwa umbo kubwa likitembea kwenye mwelekeo mmoja ulionyooka, basi macho hayaoni harakati zake kutoka na ukubwa wake na umbali wa pembe zake; hasa ikiwa mtazamaji yuko mbalia nalo.

Hapa yanatubainikia makosa ya mwenye kuitumia aya hii katika kuthibitisha harakati ya ardhi. Kuna Aya nyingi zinazofahamisha kuwa makusudio ya kutembea milima, katika Aya hii, kutakuwa siku ya Kiyama; miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:-

وَيَوْمَ نُسَيِّرُ الْجِبَالَ وَتَرَى الْأَرْضَ بَارِزَةً وَحَشَرْنَاهُمْ فَلَمْ نُغَادِرْ مِنْهُمْ أَحَدًا {47}

“Na siku tutakayoipitisha milima na utaiona ardhi iwazi. Na tutawafufua..” Juz. 15 (18:47).

وَسُيِّرَتِ الْجِبَالُ فَكَانَتْ سَرَابًا {20}

“Na ikaendeshwa milima ikawa sarabi.” (78:20).

يَوْمَ تَمُورُ السَّمَاءُ مَوْرًا {9}

وَتَسِيرُ الْجِبَالُ سَيْرًا {10}

“Siku itakapotikisika mbingu mtikisiko. Na milima iwe inakwenda mwendo.” (52: 9 10).

Maneno ya Qur’an ni mamoja, sehemu moja inaifafanulia nyingine.
Ndio! Watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.), ambao wana elimu ya Kitabu na Sunna, waliweka wazi kuwa ardhi ina harakati kabla ya Companicus, kwa miaka elfu moja. Imam Ali (a.s.) anasema katika Nahjul-balagha: Na akaiumba ardhi hewani na akiweka bila ya muhimili na akaiinua bila ya nguzo (khutba 186). Na mjukuu wake Imam Jafar Sadiq akasema: “Kufahamisha vitu kuzunguka na vilivyomo ndani yake zikiwamo sayari saba, ni kuwa ardhi ina harakati…”

Ni sanaa ya Mwenyezi Mungu aliyekitengeneza vizuri kila kitu, kuanzia kikubwa sana hadi kidogo sana. Ufundi, mpangilio na nidhamu ni ushahidi mkubwa wa kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na uwezo.

Hakika yeye ana habari za mnayoyatenda.

Ambaye amemuumba mtu kwa ufundi wa hali ya juu, anajua kila akitendacho kiumbe, kiwe cha heri au cha shari na yale yanayompitikia katika nafsi yake:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنْسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ {16}

“Na hakika tumemuumba mtu nasi tunayajua yanayoitia wasiwasi nafsi yake na sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wake wa shingo.” (50:16).

Watakaokuja na wema watapata bora kuliko hayo. Nao watasalimika na mfazaiko wa siku hiyo. Na wenye kuja na uovu, basi nyuzo zao zitatupwa motoni. Kwani mnalipwa isipokuwa yale mliyoyatenda?

Inayofafanua zaidi Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mwenye kufanya vizuri atalipwa mfano wake mara kumi. Na mwenye kufanya vibaya hatalipwa ila sawa na hivyo tu. Nao hawatadhulumiwa.” Juz. 7 (6:179).

Hakika nimeamrishwa kumwabudu tu Mola wa mji huu ambaye ameufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wenye kunyenyekea.

Makusudio ya mji hapa ni Makka Tukufu. amaeuhusisha kuutaja, pamoja na kuwa yeye ni Mola wa ulimwengu wote, ili kuwabainishia makuraishi neema yake kwao kwa sababu ya mji huo. Walikuwa wakitegemeza ubora wao kuliko waarabu wengine kwa taadhima ya mji huo na utakatifu wake na kuwa na amani, kwa kuharamishwa kuua, kupigana, kuwinda, kukata miti na mengine yanayofahamisha utukufu na cheo chake.

Pamoja na yote haya makuraishi waliabudu masanamu wakaichafua Al-ka’ba kwayo, wakimshirikisha nayo Mola wa mji huu mtukufu ambaye amewalisha kutokana na njaa na akawasalimisha na hofu.

Kauli ya Mtume (s.a.w.): ‘Nimeamrishwa kumwabudu …’ ni kuwapinga makuraishi na kwamba wajibu wao ni kuacha ibada ya ya masanamu ambayo hayamiliki chochote, na wamwabudu Mola wa mji huu ambaye ndiye muumba, mfalme na mwenye amri. Na yeye ni muweza wa kila kitu na akawafadhili makuraishi kwa vitu vingi.

Na kwamba nisome Qur’an.

Makusudio ya kusoma Qur’an hapa ni kutoa mwito wa kuiamini na kwenda na sera yake.

Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida ya nafsi yake tu na aliyepotea basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji tu.

Mtume (s.a.w.) ametoa mwito wa uongofu. Mwenye kusikia na akatii, basi amejifanyia uzuri mwenyewe na atakuwa amefuata njia ya kheri na uokovu. Na mwenye kupinga basi atakuwa amejifanyia ubaya yeye mwenyewe na kujiingiza kwenye shari na maangamizi. Mtume (s.a.w.) hana majukumu ya watu wa upotevu baada ya kuwanasihi na kuwafikishia risala ya Mola wake.

Na Sema: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdu lillah) kwa kuniwafikisha kufikisha risala yake kwa waja wake kama alivyopenda na kutaka.

Atawaonyesha ishara zake mtazijua.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaonyesha dalili za ishara zake kwenye nafsi zao na kwenye pambizo, lakini wakazikana. Ndio akawaambia, leo mnazikana na kesho mtazikubali, ambapo kukubali kwenu hakutawafaa kitu.

Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.

Haya ni makemeo na kiaga cha kupinga kwao na kukana ishara za MwenyeziMungunaubainifuwake.