read

Aya 7 – 13: Mama Wa Musa

Maana

Na tulimpa wahyi mama wa Musa kuwa mnyonyeshe.
Makusudio ya wahyi hapa ni ilhamu; ni mfano kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na Mola wako akampa wahyi nyuki.” Juz. 14 (16:68). Katika Juz. 9 (7: 103 -112).

Tumenukuu kutoka kitabu Qisasul-qur’an, kwamba jina la mama yake Musa ni Yukabid (Jochebed). Kisha tukasoma katika Tawrat kuwa hilo ndilo jina lake na kwamba aliolewa na Amram, mtoto wa kaka yake. Musa ndiye mdogo katika watoto wa baba yake, akiwa ni watatu, baada ya Maryam na Harun.

Na utakapomhofia basi mtie mtoni.

Makusudio ya mto hapa ni mto Nile. Maana ni akimhofia kuchinjwa amtie mtoni kwa mkono wake! Itakuwaje, mwenye akili aweze kujitupa motoni?

Lakini akaambiwa: Na usihofu wala usihuzunike. Hakika sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa mitume.

Usimhofie, hakika Mwenyezi Mungu ndiye mhifadhi na mlinzi. Yule ambaye ameujaalia moto kuwa baridi na salama kwa Ibrahim, ataijalia bahari kuwa amani kwa Musa. Alimpa habari ya usalama wa mtoto wake na kwamba yeye atamlea na pia akampa habari njema kuwa amemchagua kwa risala yake na kumhusu kwa rehema yake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:38).

Basi wakamwokota watu wa Firauni aje kuwa adui kwao na huzuni.

Walimwokota na kumlea kwa kumfanya mtoto wao, lakini akaja akawa ni adui wa itikadi yao na desturi yao. Akaingiza huzuni nyoyoni mwao na mwisho wa ufalme wao ukawa mikononi mwake.

Hakika Firauni na Hamana na majeshi yao walikuwa wenye makosa, wapotevu katika vitendo vyao vyote; hasa kuua maelefu ya vijana ili kujiepusha na Musa, lakini ikawa wao wanamwepusha Musa na mauti ili aje awamalize. Katika kamusi ya Kitabu kitakatifu1, imeelezwa kuwa maisha ya Musa katika nyumba ya Firauni hayakujulikana kwa ufafanuzi na kwamba wanahistoria wametofautiana kuhusu wakati wake alioishi. Wengine wakasema ni wakati wa Firauni Amenophis (Amenhotep II) (1411 – 1436 Bc), wengine wakasema ni Ramesses II (1223 – 1290 Bc). Pia kuna waliosema ni wakati wa Mernptsh ( 1211 – 1223 Bc)

Akasema mke wa Firaun: Ni kiburudisho cha macho kwangu na kwako. Msimuue! Huenda akatufaa au tumfanye kuwa mtoto wetu. Wala wao hawakutambua.

Kuburudika macho ni furaha. Mke wa Firauni ni Asiya bint Muzahim. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemsifu pale aliposema:

وَضَرَبَ اللَّهُ مَثَلًا لِلَّذِينَ آمَنُوا امْرَأَتَ فِرْعَوْنَ إِذْ قَالَتْ رَبِّ ابْنِ لِي عِنْدَكَ بَيْتًا فِي الْجَنَّةِ وَنَجِّنِي مِنْ فِرْعَوْنَ وَعَمَلِهِ وَنَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ {11}

“Na Mwenyezi Mungu amewapiga mfano walioamini – mke wa Firauni, aliposema: “Mola wangu! Nijengee kwako nyumba Peponi na uniokoe na Firauni na vitendo vyake na uniokoe na watu madhalimu.” (66:11).

Na katika Hadith imesemwa kuwa wanawake bora ni wane: Maryam binti Imran, Asiya binti Muzahim, Khadija bint Khuwaylid na Fatima bint Muhammad. Firauni alipomwangalia mtoto alishtuka na kusema, imekuaje huyu mtoto wa ki Hebrew amepona kuchinjwa? Majasusi hawakumuona au wamenificha?

Mkewe akamtuliza na akamfanya ampende mtoto ili awe kiburudisho cha macho yao, lakini akawa ni kero ya macho yao na huzuni ya nyoyo zao.
Moyo wa mamake Musa ukawa mtupu. Alikuwa karibu kudhihirisha, lau tusingeliuimarisha moyo wake ili awe miongoni mwa waumini.

Alimtupa mtoto wake baharini akiwa na matumaini ya kuukotwa na ambaye atamwepusha na Firauni. Mara kadari ikamtoa baharini hadi nyumbani kwa Firauni!

Alipopata habari kuwa ameanguka mikononi mwa mchinjaji, alijua mtoto wake amekwisha.

Akafazaika sana na akajisahau na ahadi aliyoahidiwa na Mungu kuwa atamrudisha kwake; akawa karibu adhihirishe fazaa yake kwa kutamka jina la kipenzi chake, lakini Mwenyezi Mungu akampa utuvu, akaufanya thabiti moyo wake ili awe miongoni mwa wanaoamini ahadi yake. Kwa hiyo akawa na subira na akatulia.

Akamwambia dadake (Musa), mfuatie na uchunguze habari yake.

Akaenda na akamkuta kwa Firauni.

Basi akawa anamwangalia kiupande upande na wao hawatambui.

Wengine wamefasiri alimwangalia kwa mbali.

Maana ni kuwa alimwangalia kama vile hataki wala hamkusudii yeye, huku watu wa Firauni hawajui lengo lake au kuwa yeye ni dada wa mtoto waliyemuokota ufukweni.

Na tukamharamishia wanyonyeshaji tangu mwanzo.

Firauni alimsikiliza mkewe, akamwacha mtoto baada ya Mwenyezi Mungu kutia mahaba moyoni mwake na akaamrisha atafutwe mnyonyeshaji atakayemlea na kumtunza.

Wakaletwa wanyonyeshaji kutoka huku na huko, kila mmoja anapendelea akubali matiti yake ili apate hadhi mbele ya Firauni. Lakini mtoto aliwakataa wote.

Akasema (dadake): Je, niwaonyeshe watu wa nyumba watakaowalelea na watakuwa wema kwake.

Dadake Musa alipoona kuduwaa kwa watu wa Firauni kuhusu mtoto alijitokeza kuwaelekeza atakayekubali matiti yake na kumshughulikia bila ya kuzembea. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:40).

Basi tukamrudisha kwa mama yake ili yaburudike macho yake.

Vile vile umetangulia mfano wake katika Juzuu hiyo hiyo.

Na ajue kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli.

Yaani mamake Musa ajue kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kurudishiwa mwanawe na kuwa miongoni mwa mitume, ni kweli.

Lakini watu wengi hawajui, mipangilio yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na undani wa hekima yake.

وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَاسْتَوَىٰ آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ {14}

Na alipofikilia kukomaa kwake na akastawi, tulimpa hukmu na elimu. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.

وَدَخَلَ الْمَدِينَةَ عَلَىٰ حِينِ غَفْلَةٍ مِنْ أَهْلِهَا فَوَجَدَ فِيهَا رَجُلَيْنِ يَقْتَتِلَانِ هَٰذَا مِنْ شِيعَتِهِ وَهَٰذَا مِنْ عَدُوِّهِ ۖ فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِنْ شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ ۖ قَالَ هَٰذَا مِنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ ۖ إِنَّهُ عَدُوٌّ مُضِلٌّ مُبِينٌ {15}

Na akaingia mjini wakati wenyeji wake wako kwenye mghafala. Akakuta humo watu wawili wanapigana – huyu ni katika kundi lake na huyu ni katika adui zake. Yule aliye katika kundi lake alimtaka msaada dhidi ya yule aliye katika adui zake. Musa akampiga, akammaliza. Akasema: Hiki ni kitendo cha shetani; hakika yeye ni adui mpotezaji dhahiri.

قَالَ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي فَاغْفِرْ لِي فَغَفَرَ لَهُ ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ {16}

Akasema: Mola wangu! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu, basi nisamehe. Akamsamehe; hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

قَالَ رَبِّ بِمَا أَنْعَمْتَ عَلَيَّ فَلَنْ أَكُونَ ظَهِيرًا لِلْمُجْرِمِينَ {17}

Akasema: Mola wangu! Kwa ulivyonineemesha, sitakuwa msaidizi wa wakosefu.

فَأَصْبَحَ فِي الْمَدِينَةِ خَائِفًا يَتَرَقَّبُ فَإِذَا الَّذِي اسْتَنْصَرَهُ بِالْأَمْسِ يَسْتَصْرِخُهُ ۚ قَالَ لَهُ مُوسَىٰ إِنَّكَ لَغَوِيٌّ مُبِينٌ {18}

Akapambaukia mjini akiwa na hofu na hadhari, mara yule aliyemtaka msaada jana anampigia kelele. Musa akamwambia: Hakika wewe ni mpotevu dhahiri.

فَلَمَّا أَنْ أَرَادَ أَنْ يَبْطِشَ بِالَّذِي هُوَ عَدُوٌّ لَهُمَا قَالَ يَا مُوسَىٰ أَتُرِيدُ أَنْ تَقْتُلَنِي كَمَا قَتَلْتَ نَفْسًا بِالْأَمْسِ ۖ إِنْ تُرِيدُ إِلَّا أَنْ تَكُونَ جَبَّارًا فِي الْأَرْضِ وَمَا تُرِيدُ أَنْ تَكُونَ مِنَ الْمُصْلِحِينَ {19}

Basi Musa alipotaka kumkamata kwa nguvu, yule aliye adui yao akasema: Ewe Musa! Unataka kuniua, kama ulivyomuua mtu jana? Hutaki ila kuwa jabari katika ardhi, wala hutaki kuwa miongoni mwa wema.
  • 1. Wakiristo wanaita Tawrat na Injili nne, Kitabu kitakatifu. Kamusi iliyotajwa inafafanua maana ya maneno yaliyo katika Kitabu Kitakatifu, na inadokeza historia, matukio, watu na mengineyo yanayoambatana na Tawrat na Injil