read

Aya 29 – 32: Musa Anamaliza Muda

Baada ya kutimia muda walioafikana Musa na baba mkwe, alifungasha virago vyake na akelekea Misri pamoja na ahli zake. Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu, imeandikwa: “Musa alikwenda Misri pamoja na mkewe na wanawe wawili.”

Basi alipofika jangwani alipotea njia kwenye giza la usiku wenye baridi; kama inavyofahamisha kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Mpate kuota.” Wakati akiwa hajui la kufanya, mara akaona moto unawaka, ndipo akawaaambia watu wake, ningojeni niende kwenye ule moto niwaletee habari za njia au angalau niwaletee moto wa kuota. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:10) na Juz. 19 (27:7).

Basi alpoufikia aliitwa kutoka upande wa kulia wa bonde. Yaani upande wa kulia wa Musa. Katika eneo lilobarikiwa, kutokana na Mitume wengi kutokea huko na heri zake nyingi, kutoka mtini, kwamba ewe Musa! Hakika mimi ndiye Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “kutoka mtini,” inafahamisha kwamba Mwenyezi Mungu aliumba maneno kwenye mti.

Wale wanaosema kuwa maneno ya Mwenyezi Mungu ni ya kuzuka na wala siyo ya tangu zamani, wametoa dalili kwa Aya hii. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (19: 52) na (20: 12).

Na kwamba, itupe fimbo yako! Alipoiona inatingishika, kama kwamba ni nyoka aligeuka kurudi nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Njoo mbele wala usihofu! Hakika wewe ni miongoni mwa waliosalimika.

Umetangulia mfano wake katika Juz. Juz. 19 (27:10).

Na ingiza mkono wako katika mfuko wako utatoka mweupe pasipo ubaya na vutia mkono wako kwako kutuliza hofu. Basi hizo ni dalili mbili kutoka kwa Mola wako kwa ajili ya Firauni na wakuu wake. Hakika wao ni watu mafasiki.

Kuvutia mkono ni kuuweka kifuani;yaani hilo linatuliza hofu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:108), Juz. 16 (20:22) na Juz. 19 (26:33) na (16:12).

قَالَ رَبِّ إِنِّي قَتَلْتُ مِنْهُمْ نَفْسًا فَأَخَافُ أَنْ يَقْتُلُونِ {33}

Akasema: Mola wangu! Hakika mimi nilimuua mtu katika wao, kwa hiyo nahofia wataniua.

وَأَخِي هَارُونُ هُوَ أَفْصَحُ مِنِّي لِسَانًا فَأَرْسِلْهُ مَعِيَ رِدْءًا يُصَدِّقُنِي ۖ إِنِّي أَخَافُ أَنْ يُكَذِّبُونِ {34}

Na ndugu yangu Harun ni fasaha zaidi kwa ulimi kuliko mimi, basi mtume pamoja nami awe msaidizi. Hakika mimi nahofia watanikadhibisha.

قَالَ سَنَشُدُّ عَضُدَكَ بِأَخِيكَ وَنَجْعَلُ لَكُمَا سُلْطَانًا فَلَا يَصِلُونَ إِلَيْكُمَا ۚ بِآيَاتِنَا أَنْتُمَا وَمَنِ اتَّبَعَكُمَا الْغَالِبُونَ {35}

Akasema: Tutautia nguvu mkono wako kwa ndugu yako. Na tutawapa madaraka hawatawafikia. Kwa sababu ya ishara zetu, nyinyi na watakaowafuata mtashinda.

فَلَمَّا جَاءَهُمْ مُوسَىٰ بِآيَاتِنَا بَيِّنَاتٍ قَالُوا مَا هَٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُفْتَرًى وَمَا سَمِعْنَا بِهَٰذَا فِي آبَائِنَا الْأَوَّلِينَ {36}

Basi alipowafikia Musa na ishara zetu zilizo wazi wazi, walisema: Haya si chochote ila ni uchawi uliotungwa. Na hatukuyasikia haya kwa baba zetu wa zamani.

وَقَالَ مُوسَىٰ رَبِّي أَعْلَمُ بِمَنْ جَاءَ بِالْهُدَىٰ مِنْ عِنْدِهِ وَمَنْ تَكُونُ لَهُ عَاقِبَةُ الدَّارِ ۖ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ {37}

Na akasema Musa: Mola wangu ndiye anayemjua kabisa nani anayekuja na uwongofu kutoka kwake na ni nani atakayekuwa na mwisho mwema wa makazi. Hakika wenye kudhulumu hawatafanikiwa.