read

Aya 33 – 37: Nahofia Wasije Wakaniua

Maana

Akasema: “Mola wangu! Hakika mimi nilimuua mtu katika wao, kwa hiyo nahofia wataniua.”

Umetangulia mfano wake katika Juz. 19 (26:14).

Na ndugu yangu Harun ni fasaha zaidi kwa ulimi kuliko mimi, basi mtume pamoja nami awe msaidizi. Hakika mimi nahofia watanikadhibisha.

Hii inaashiria kuwa mwito wowote hauna budi uwe na wasaidizi. Na kwamba ilimu peke yake haitoshi kuitetea haki ikiwa haikwenda pamoja na ufasaha wa ulimi na ubainifu.

Vile vile Aya inafahamisha kuwa Qur’an inaunga mkono nyenzo za uenezaji habari; kama vile idhaa, magazeti n.k., lakini kwa sharti ya kuwa na mwelekeo wa kuithibitisha haki na kuwatetea watu wake na kuibatilisha batili na kuwatangaza wasaidizi wake; sawa na alivyoitumia Harun elimu yake na ufasaha wake dhidi ya utaghuti wa Firaun.

Imesemekana kuwa Harun ni mkubwa wa Musa kwa miaka mitatu. Sijui aliokoka vipi na kuchinjwa. Sio mbali kuwa Harun alizaliwa kabla ya Firauni kuamuru achinjwe kila mwana wa Israili atakayezaliwa. Katika Tawrat, kitabu cha Kutoka 32 imeelezwa kuwa Harun ndiye aliyewatengenezea wana wa israil ndama na kuwajengea dhabihu na wala sio Msamaria, kama ilivyoelezwa katika Qur’an Juz. 16 (20:95).

Akasema: Tutautia nguvu mkono wako kwa ndugu yako.

Mwenyezi Mungu alimwitikia Musa maombi yake, kama alivyotaka. Kauli ya Musa ya kuhofia kuuawa ameijibu Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kusema:

Na tutawapa madaraka hawatawafikia. Kwa sababu ya ishara zetu, nyinyi na watakaowafuata mtashinda.

Katika Juz. 16, amesema: “Msiogope! Hakika mimi niko pamoja nanyi. Nasikia na ninaona,” na hapa akasema kuwa nitawapa silaha itakayomtisha Firauni na jeshi lake na mtaneemeka kwayo nyinyi na wale watakaowaamini. Silaha hii au madaraka hayo ni ishara na miujiza; kama vile fimbo kugeuka nyoka, mkono kuwa mweupe, nzige, chawa, vyura n.k.

Basi alipowafikia Musa na ishara zetu zilizo wazi wazi, walisema: Haya si chochote ila ni uchawi uliotungwa. Na hatukuyasikia haya kwa baba zetu wa zamani.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:109) na Juz. 16 (20:63).

Na akasema Musa: Mola wangu ndiye anayemjua kabisa nani anayekuja na uwongofu kutoka kwake na ni nani atakayekuwa na mwisho mwema wa makazi. Hakika wenye kudhulumu hawatafanikiwa.

Walimkadhibisha Musa wakamwambia ni mchawi, akawajibu kwa jawabu la asiyejali kukadhibisha kwao na inadi yao, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na ahadi yake.

Kwa ufupi, jawabu ni kuwa Mwenyezi Mungu anajua kuwa mimi niko katika haki na uongofu na kwamba nyinyi mko kwenye batili na upotevu. Vile vile anajua kwamba mwisho mwema ni wangu na wanonifuata, nanyi mtapata mwisho wa maangamizi duniani na adhabu ya moto huko akhera.

وَقَالَ فِرْعَوْنُ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ مَا عَلِمْتُ لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرِي فَأَوْقِدْ لِي يَا هَامَانُ عَلَى الطِّينِ فَاجْعَلْ لِي صَرْحًا لَعَلِّي أَطَّلِعُ إِلَىٰ إِلَٰهِ مُوسَىٰ وَإِنِّي لَأَظُنُّهُ مِنَ الْكَاذِبِينَ {38}

Na akasema Firauni: Enyi waheshimiwa! Sijui kama mnaye Mungu asiyekuwa mimi. Ewe Haman! Niwashie moto unichomee udongo, unijengee mnara nipate kumchungulia Mungu wa Musa na hakika mimi namuona yeye ni katika waongo.

وَاسْتَكْبَرَ هُوَ وَجُنُودُهُ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ إِلَيْنَا لَا يُرْجَعُونَ {39}

Na akawa na kiburi yeye na majeshi yake katika nchi bila ya haki. Na wakadhani kuwa hawatarudishwa kwetu.

فَأَخَذْنَاهُ وَجُنُودَهُ فَنَبَذْنَاهُمْ فِي الْيَمِّ ۖ فَانْظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الظَّالِمِينَ {40}

Basi tukamshika yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini. Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa wenye kudhulumu.

وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ لَا يُنْصَرُونَ {41}

Na tukawafanya ni maimamu waitao kwenye moto. Na siku ya Kiyama hawatanusuriwa.

وَأَتْبَعْنَاهُمْ فِي هَٰذِهِ الدُّنْيَا لَعْنَةً ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ هُمْ مِنَ الْمَقْبُوحِينَ {42}

Na tukawafuatishia laana katika dunia hii. Na siku ya Kiyama watakuwa miongoni mwa wanaokebehiwa.

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ مِنْ بَعْدِ مَا أَهْلَكْنَا الْقُرُونَ الْأُولَىٰ بَصَائِرَ لِلنَّاسِ وَهُدًى وَرَحْمَةً لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ {43}

Na hakika tulimpa Musa Kitabu, baada ya kuziangamiza karne za kwanza, ili kiwafumbue macho watu na kiwe uongofu na rehema ili wapate kukumbuka.