read

Aya 38 – 43: Sijui Kama Mna Mungu Mwingine

Maana

Na akasema Firauni: Enyi waheshimiwa! Sijui kama mnaye Mungu asiyekuwa mimi.

Alisema hivi kwa vile alipata wa kumsadiki. Nilihifadhi mithali tangu utotoni bado naikumbuka: “Firauni aliulizwa, ni nani Firauni wako? Akasema: Sijapata wa kunipinga”

Watu wengi wangelikuwa mafirauni lau kusingelikuweko upinzani. yatakuja maelezo katika Juz.30 (79:24).
Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu, imeelezwa kuwa neno Firauni ni la kimisri lenye maana ya nyumba kubwa nalo ni msimbo wa wafalme wa Misri.

Ewe Haman! Niwashie moto unichomee udongo, unijengee mnara nipate kumchungulia Mungu wa Musa na hakika mimi namuona yeye ni katika waongo.

Firauni alishindwa kuikabili hoja kwa hoja, akamuhofia Musa na fimbo yake. Akajaribu kuificha hofu yake hii na kushindwa kwake kwa kuwavun- ga watu wake kuhusu Musa, ndipo akadhihirisha shaka ya kuweko Mungu asiyekuwa yeye na kwamba yeye atamchunguza na kumtafuta. Akimpata atapambana naye; vinginevyo basi Musa atakuwa ni muongo.

Ili kusisitiza uvungaji huu machoni mwa wale walio bendera kufuata upepo, alimwambia Haman amwashie moto na atengeneze mnara mrefu utakaomwezesha kupanda mbinguni ili amtafute Mungu wa Musa.

Haman hakujenga mnara, kama tunavyodhani, kwa sababu ana yakini na vitimbi vya Firauni. Ni nani mwenye akili anayeweza kujaribu kujenga jengo lisilo na mwisho na kuwa na njozi za kuwa udongo na miti inaweza kufika kwenye mbingu za juu na kumjua aliyeko huko?

Na akawa na kiburi yeye na majeshi yake katika nchi bila ya haki. Na wakadhani kuwa hawatarudishwa kwetu.

Walijikweza juu ya watu, wakajivuna na wakaeneza ufisadi na shari. Sababu ya kwanza na ya mwisho ni kwamba wao hawamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, wala misingi na dhamiri. Hawaamini kitu chochote isipokuwa nafsi zao na manufaa yao. Kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu akawanyakua mnyakuo wa mwenye nguvu na uweza.

Basi tukamshika yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini. Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa wenye kudhulumu?

Mama yake Musa alimtupa mwanawe kwa kumhofia Firauni, lakini adui huyu wa Mungu na wa Musa akamuokota ili anufaike naye. Musa alipokuwa mkubwa alijaribu kwa juhudi zake kumnufaisha Firauni kwa kumuokoa na maangamizi na adhabu, lakini akakataa na kuwa na kiburi, ukawa mwisho wake ni kuangamia kwenye bahari ile ile aliyomuokota Musa. Katika hayo kuna mazingatio kwa wenye busara, lakini wako wapi?

Na tukawafanya ni maimamu waitao kwenye moto. Na siku ya Kiyama hawatanusuriwa.

Hao ni Firauni na majeshi yake. Maana ni kuwa wao, duniani wamepotea na kuwapoteza wengine na akhera ni wenye hasara.

Maana ya tumewajaalia ni kuwa Mwenyezi Mungu amepitisha kadari kuwa mwenye kufuata njia ya maangamizi basi ataangamia. Hilo tumelibainisha mara nyingi huko nyuma.

Imepokewa riwaya kutoka kwa Imam Jafar Assadiq (a.s.) kwamba maimamu katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni aina mbili: Maimamu wa uongofu ambao amewaashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kauli yake:

وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا {73}

“Na tukawafanya maimamu wakiongoza kwa amri yetu. ” Juz. 17 (21:73).

Hao wanatanguliza amri ya Mwenyezi Mungu kabla ya amri yao na hukumu yake kabla ya hukumu yao. Aina ya pili ni maimamu waitao kwenye moto, wakitanguliza amri yao kabla ya amri ya Mwenyezi Mungu na hukumu yao kabla ya hukumu ya Mwenyezi Mungu.

Vile vile wanachukua hawa zao kinyume na ilivyo katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Na tukawafuatishia laana katika dunia hii. Na siku ya Kiyama watakuwa miongoni mwa wanaokebehiwa.

Duniani wana laana ya dunia, ya Mwenyezi Mungu na ya wenye kulaani na Akhera watapata adhabu ya moto.

Na hakika tulimpa Musa Kitabu, baada ya kuziangamiza karne za kwanza, ili kiwafumbue macho watu na kiwe uongofu na rehema ili wapate kukumbuka.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimtermshia Musa Tawrat baada ya kuangamizwa kaumu ya Nuh, A’d na Thamud.

Lengo la kuteremshwa kwake ni kuwapa mawaidha watu na kutumia hukumu yake. Kwa sababu Tawrat, kabla ya kupotoshwa ilikuwa ni nuru, mwongozo na rehema.

Lakini Tawrat ya leo inawambia Waisraili: “ Uweni wanaume, watoto na wanawake, isipokuwa bikra, wabakisheni kwa ajili ya kustarehe nao ... Na mpore wanyama na milki zote... Mchome miji makazi na makambi.” kama ilivyoelezwa Kitabu cha Hisabu 32.

Je, baada ya haya kuna haja ya kuuliza kwa nini Israil imeuchoma Msikiti wa Aqsa? Itikadi ya kiyahudi ni ya shari na uadui kwa dini zote, sharia na misimamo ya kiubinadamu.

وَمَا كُنْتَ بِجَانِبِ الْغَرْبِيِّ إِذْ قَضَيْنَا إِلَىٰ مُوسَى الْأَمْرَ وَمَا كُنْتَ مِنَ الشَّاهِدِينَ {44}

Wala wewe hukuwa upande wa magharibi tulipompa Musa amri wala hukuwa miongoni mwa walioshuhudia.

وَلَٰكِنَّا أَنْشَأْنَا قُرُونًا فَتَطَاوَلَ عَلَيْهِمُ الْعُمُرُ ۚ وَمَا كُنْتَ ثَاوِيًا فِي أَهْلِ مَدْيَنَ تَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا وَلَٰكِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ {45}

Lakini tuliziumba karne na umri ukawa mrefu juu yao. Wala hukuwa mkaazi wa watu wa Madyana ukiwasomea Aya zetu, lakini ni sisi tuliokuwa tukiwatuma Mitume.

وَمَا كُنْتَ بِجَانِبِ الطُّورِ إِذْ نَادَيْنَا وَلَٰكِنْ رَحْمَةً مِنْ رَبِّكَ لِتُنْذِرَ قَوْمًا مَا أَتَاهُمْ مِنْ نَذِيرٍ مِنْ قَبْلِكَ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ {46}

Wala hukuwa kando ya mlima tulipomuita. Lakini ni rehema itokayo kwa Mola wako ili uwaonye watu wasiofikiwa na muonyaji kabla yako, huenda wakakumbuka.

وَلَوْلَا أَنْ تُصِيبَهُمْ مُصِيبَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ فَيَقُولُوا رَبَّنَا لَوْلَا أَرْسَلْتَ إِلَيْنَا رَسُولًا فَنَتَّبِعَ آيَاتِكَ وَنَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ {47}

Na usije ukawasibu msiba kwa iliyoyatanguliza mikono yao, kisha waseme: Ewe Mola wetu! Mbona hukutuletea Mtume nasi tukafuata ishara zako na tukawa miongoni mwa waumini?

فَلَمَّا جَاءَهُمُ الْحَقُّ مِنْ عِنْدِنَا قَالُوا لَوْلَا أُوتِيَ مِثْلَ مَا أُوتِيَ مُوسَىٰ ۚ أَوَلَمْ يَكْفُرُوا بِمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ مِنْ قَبْلُ ۖ قَالُوا سِحْرَانِ تَظَاهَرَا وَقَالُوا إِنَّا بِكُلٍّ كَافِرُونَ {48}

Ilipowajia haki kutoka kwetu walisema: Mbona hakupewa kama aliyopewa Musa? Je, hawakuyakataa aliyopewa Musa zamani? Walisema: ni wachawi wawili wanaosaidiana. Hakika tunawakataa wote.

قُلْ فَأْتُوا بِكِتَابٍ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ هُوَ أَهْدَىٰ مِنْهُمَا أَتَّبِعْهُ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {49}

Sema: Basi leteni kitabu kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu chenye mwongozo zaidi kuliko viwili nikifuate, ikiwa nyinyi mnasema kweli.

فَإِنْ لَمْ يَسْتَجِيبُوا لَكَ فَاعْلَمْ أَنَّمَا يَتَّبِعُونَ أَهْوَاءَهُمْ ۚ وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّنِ اتَّبَعَ هَوَاهُ بِغَيْرِ هُدًى مِنَ اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ {50}

Na ikiwa hawakuitikii basi jua kuwa wamejifuatia tu hawaa zao. Na ni nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayefuata hawaa yake bila ya mwongozo utokao kwa Mwenyezi Mungu? Hakika Mwenyezi Mungu hawongozi watu madhalimu.

وَلَقَدْ وَصَّلْنَا لَهُمُ الْقَوْلَ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ {51}

Na kwa hakika tuliwafululizia maneno ili wapate kukumbuka.