Huwezi Kumuongoa Umtakaye Aya 56 - 61
Maana
Abu Twalib Na Uislamu
Kwa hakika wewe humuongoi umtakaye, lakini Mwenyezi Mungu humuongoa amtakaye, naye ndiye anayewajua zaidi waongokao.
Wametofautiana katika sababu ya kushuka Aya hii. Wakasema wafisri wengi katika Sunni kuwa ilishuka kwa ajili ya ami wa Mtume, Abu Twalib. Shia wakasema Aya haikumuhusu yeye wala mwinginewe. Mtume (s.a.w.) anapenda kila mmoja aongoke, awe ni wa karibu naye au wa mbali naye. Herufi man, katika Aya ni ya kuenea.
Kuitumia Aya kwa kumhusu Abu Twalib peke yake, hiyo itakuwa ni kuyatumia maneno ya Mwenyezi Mungu bila ya dalili. Ama riyawa inayosema kuwa Aya imeshuka kwa Abu Twalib peke yake, hiyo haikuthibiti kwetu.
Kwa hiyo basi Aya hii itakuwa inarudufu Aya nyingine isemayo: “Je, wewe unaweza kuwaongoza vipofu ingawa hawaoni? Juz. 13 (10:43).
Mwenye Tafsiri Fii dhilal amerefusha maneno, kisha akaishia kwenye madhehebu ya mababa na mababu, akategemea dalili za wakale ingawaje zinapingana na maumbile ya kiakili.
Naye amekariri mara kadhaa kuwa Qur’an inazungumza na umbile la akili kwa undani. Nasi tutayahukumu maneno yake kwa mahakama ya maumbile ya kiakili na ya kimaudhui, sio ya kimadhehebu wala ya kiupendeleo. Tunamtarajia msomaji aangalie kauli yetu kwa mtazamo wa kielimu usiokuwa na upendeleo.
Anasema mwenye Fii dhilal, ninamnukuu: “Huyu ami wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), mlezi wake muhami wake na mgombezi wake, Mwenyezi Mungu hamwandikii imani, ingawaje anampenda sana Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mtume wa Mwenyezi Mungu naye anampenda sana, Mwenyezi Mungu hamwandikii kuamini.
Maana ya kauli hii ni kuwa Mwenyezi Mungu alichukia Abu Twalib kusema: Lailaha illa llah, Muhammadu rrasulullah (Hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu), lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu alipenda na kung’ang’ani aseme kauli hii.
Tunauliza: Inaingilika akilini kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu apende jambo ambalo Mwenyezi Mungu analichukia? Basi kwa nini Mwenyezi Mungu ameilinganisha sawa twaa yake na ya Mtume, kwenye Aya kadhaa? Ikiwa Mwenyezi Mungu amechukia Abu Twalib asilimu na wala hakumwandikia kusilimu, basi kwanini amwadhibu na amuweke kwenye moto wa ‘juu juu’ kama walivyopokea wazushi? Je, inafaa mwenye nguvu kumwadhibu mnyonge kwa jambo ambalo hakulifanya? Itakuwaje na hali yeye ndiye alisema: “Na mimi si mwenye kuwadhulumu waja?”
Kwa nini Mwenyezi Mungu apende Abu Sufyani asilimu, lakini achukie kwa Abu Twalib? Ni kwa sababu Abu Sufyan alikuwa akimchukia sana Mtume, na kumkusanyia majeshi ya kumpiga vita, akapenda awe mwislamu, lakini Abu Twalib aliyempenda sana Mtume na kumuhami ndio akachukia kuwa mwislamu? Au ni kwa sababu Abu Sufyan ni mzazi wa Muawiya na Abu Twalib ni mzazi wa Ali?
Majibu ya maswali yote haya ni ndio kwa wale wanaodai kuwa Abu Twalib ni kafiri. Kwa sababu wao wanaamini kuwa Mwenyezi Mungu hawajibikiwi na lolote na wala kwake hakuna jambo baya, na kwamba inafaa kwake kuwaadhibu wema; na wale wanaomwaga damu za watu kuwafanya ni wema.
Je, mwenye Fii dhilal alikusudia kuwa maana haya ndiyo yametokana na umbile la akili la ndani?
Zaidi ya hayo, kuandika tafsiri na isiyokuwa tafsiri kunaathirika na itikadi, mazingira, utamuduni na hali ya mwandishi. Na hili halimwachi mdogo wala mkubwa. Lakini hii haina maana kwamba itikadi na mapondokeo yote hayaafikiani na haki na hali halisi. Vinginevyo ingelikuwa muhali kauli ya haki na uadilifu. Ni wajibu kwa mtu kujitahidi kuitafuta haki kutokana na chimbuko lake, si kutokana na itikadi au mazingira. Na haya ndiyo tunayojaribu na kuyakusudia.
Misitari hii tunaiunganisha na tuliyoyaandika kuhusiana na maudhui haya katika Juz. 11 (9:113).
Na wakasema: Tukifuata muongozo huu pamoja nawe, tutanyakuliwa kutoka nchi yetu.
Kuna riwaya isemayo kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alisema: “Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake! Jambo hili nitalitolea mwito kwa mweusi na mweupe, kwa aliye juu ya kilele cha mlima na aliye kwenye kilindi cha maji na nitawatolea mwito watu wa Fursi na Roma.”
Basi vigogo wa kikuraishi waliposikia maneno haya wakayakuza na kumwambia Mtume (s.a.w.); “Vipi tukufuate na wewe nia yako ni hii. Kama tutakuitikia, basi kutakuwa na watu wengi wakiwemo wafursi na waroma na watachukua mali zetu na miji yetu na wataivunja Al-Kaa’ba vipande vipande.”
Iwe ni sahihi riwaya au la, lakini madhumuni yake yanendana na Aya hii. Kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alimlingani mweusi na mweupe, akaendelea na mwito wake. Vigogo wa kikuraishi wakampiga vita.
Zaidi ya hayo pia riwaya inaafikiana na kauli yake Mwenyezi Mungu inayofuatia:
Je, kwani hatukuwaweka imara mahali patakatifu pa amani, panapoletwa matunda ya kila aina kuwa ni riziki itokayo kwetu?
Vipi nyinyi watu wa Makka mnawahofia watu na hali Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameulinda mji wenu huu na mauaji na uporaji tangu siku ya kwanza? Na akajaalia nyoyo za watu zinauelekea mji huu wakileta kila aina ya matunda na mambo mazuri?
Lakini wengi wao hawajui kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameuhusisha mji huu na sifa hizi kuliko miji mingine.
Na ni miji mingapi iliyojifaharisha maisha yake tumeiangamiza! Na hayo maskani yao hayakukaliwa tena baada yao ila kwa uchache tu. Na sisi ndio tumekuwa warithi.
Walimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu kuwa tunawahofia watu kama tutakufuata wewe, akawajibu Mwenyezi Mungu, katika Aya iliyotangulia, kuwa mnahofia watu na hali Mwenyezi Mungu ameujalia mji wenu huu ni mtakatifu na wa amani?
Kisha katika Aya hii anawauliza, mnawahofia watu badala ya kumhofia Mwenyezi Mungu? Je, hampati mazingatio kwa umma zilizopita ambazo zilifanya jeuri na kuzikufuru neema za Mwenyezi Mungu, ndipo Mwenyezi Mungu akaziangamiza kwa sababu ya kuzikufuru neema zake, wakaacha miji yao ni magofu isipokuwa michache tu, lakini mingi ikawa haina warithi ila yule atakayeirithi ardhi na waliomo juu yake na kwake ndio marejeo.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:128).
Na Mola wako haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume katika mji wao mkuu awasomee Aya zetu. Wala hatuiangamizi miji mpaka watu wake wawe madhalimu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni mwadilifu na ni hakimu hamwadhibu yoyote ila baada ya mawaidha na kuhadharishwa.
Unaweza kuuliza: Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu hatumi Mtume katika miji midogo au kama akituma mtume basi watu wake hatawaadhibu kama hawatamsikiliza. Na hii haielekiani na misingi ya usawa katika taklifa na wajibu. Sasa itakuwaje?
Jibu: Aya imekuja kwenye mfumo wa aghlab. Kwani mitume wengi walitumwa kwenye miji mikubwa na kila Mtume alikuwa akituma muongoza- ji kwenye miji midogo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:6) na Juz. 12 (11:118).
Na chochote mlichopewa ni matumizi ya maisha ya dunia na pambo lake. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio bora na yatakayobaki zaidi. Basi je, hamfahamu?
Matumizi mabaya ya maisha ya dunia ni yale yanayomfanya mtu kuwa jeuri na kueneza ufisadi. Vingenevyo hakuna uharamu wa mapambo ya Mwenyezi Mungu na riziki njema isipokuwa kwa asiyejua dini ya Mwenyezi Mungu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2: 103) na Juz.5 (4:77).
Je yule tuliyemuahidi ahadi nzuri tena naye akaipata, ni kama tuliyemstarehesha kwa starehe za maisha ya duniani na kisha siku ya Kiyama akawa miongoni mwa wanaohudhurishwa?
Mwenyezi Mungu aliwaahidi wale ambao wameamini na wakatenda mema Pepo ambazo hupita mito chini yake. Mwenyezi Mungu atatekeleza ahadi yake tu. Hakuna shaka kwamba mwenye kuneemeka na pepo ya milele hawezi kufananishwa na mwenye kustarehe hapa duniani kisha apelekwe Jahannam.
وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ فَيَقُولُ أَيْنَ شُرَكَائِيَ الَّذِينَ كُنْتُمْ تَزْعُمُونَ {62}
قَالَ الَّذِينَ حَقَّ عَلَيْهِمُ الْقَوْلُ رَبَّنَا هَٰؤُلَاءِ الَّذِينَ أَغْوَيْنَا أَغْوَيْنَاهُمْ كَمَا غَوَيْنَا ۖ تَبَرَّأْنَا إِلَيْكَ ۖ مَا كَانُوا إِيَّانَا يَعْبُدُونَ {63}
وَقِيلَ ادْعُوا شُرَكَاءَكُمْ فَدَعَوْهُمْ فَلَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُمْ وَرَأَوُا الْعَذَابَ ۚ لَوْ أَنَّهُمْ كَانُوا يَهْتَدُونَ {64}
وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ فَيَقُولُ مَاذَا أَجَبْتُمُ الْمُرْسَلِينَ {65}
فَعَمِيَتْ عَلَيْهِمُ الْأَنْبَاءُ يَوْمَئِذٍ فَهُمْ لَا يَتَسَاءَلُونَ {66}
فَأَمَّا مَنْ تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَعَسَىٰ أَنْ يَكُونَ مِنَ الْمُفْلِحِينَ {67}
وَرَبُّكَ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ وَيَخْتَارُ ۗ مَا كَانَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ ۚ سُبْحَانَ اللَّهِ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ {68}
وَرَبُّكَ يَعْلَمُ مَا تُكِنُّ صُدُورُهُمْ وَمَا يُعْلِنُونَ {69}
وَهُوَ اللَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ لَهُ الْحَمْدُ فِي الْأُولَىٰ وَالْآخِرَةِ ۖ وَلَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ {70}