Aya 1 – 9: Imani, Jihadi Na Subira
Maana
Alif Laam Miim.
Umepita mfano wake katika Juz. 1 (2:1).
Wasidhani watu wataachwa waseme tumeamini nao wasijaribiwe?
Imani sio tamko la kusemwa, bali hapana budi liamambatane na mitihani na majaribu ya aina ya raha na tabu. Mwenye kuvumilia tabu na asitoke kwenye dini yake na akashukuru raha na kunyenyekea, wala cheo na mali isimfanye jeuri na kupetuka mipaka, huyo ndiye mumin wa kweli. Vinginevyo atakuwa sio mumin chochote.
Hivi ndivyo inavyofahamisha dhahiri ya Aya. Tukiiunganisha na Aya nyingine zinazohusiana na maudhui haya, tunapata muhtasari wa kuwa kuna jambo ambalo haliepukani na imani kwa hali yoyote. Nalo ni kuitikia muumini mwito wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kimatendo sio kimatamshi; yaani afanye bidii yake yote kutii amri ya Mungu na makatazo yake na kuambatana hayo na tabia yake na matendo yake. Anapopata mtihani na msukosuko wowote, basi umzidishe imani na unyenyekevu, kwa sababu anamfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu.
Tazama Juz. 2 (2: 153 – 157), kifungu cha ‘Thamani ya Pepo,’ Juz. 2 (2:211 – 212), kifungu cha ‘Hakuna imani bila ya takua’ na Juz. 5 (4: 135 – 136) kifungu cha ‘Baina ya dini na watu wa dini.’
Hakika tuliwajaribu waliokuwa kabla yao.
WafuasiwaMitumewaliotanguliatuliwajaribukwashida,wakavumiliana wakawa na subira ya uungwana na wakazidi kushikamana na dini yao na ikhlasi kwa Mola wao na mitume yao.
Tafsiri inayofafanua zaidi Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Ni manabii wangapi waliopigana pamoja nao waumin wengi, nao hawakulegea kwa yale yaliyowasibu katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika, wala hawakudhalilika. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaosubiri.” Juz. 4 (3:146).
Kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wa kweli na kwa yakini atawatambulisha waongo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamtahini mja wake kwa kumpa mbele ya dunia na nyuma yake, ili vidhihiri vitendo vyake vitakavyomfanya astahiki thawabu na adhabu. Kwa sababu yeye ambaye, imetukuka hekima yake, hamhisabu mtu kutokana na maandalizi yake ya kheri au ya shari; isipokuwa anamhisabu kwa matendo yake ambayo yanadhihirika.
Au wanadhani wanaotenda maovu kwamba watatushinda?
Waovu wanafikiria kuwa Mwenyezi Mungu hawezi kuwapata? Itakuwaje naye ni muweza wa kila kitu? Ni nani atakayeweza kuwazuia naye na hali yeye hana mpinzani wala mshirika aliye sawa naye?
Ni mabaya wanayohukumu kwamba wao wataponyoka na utawala wa Mwenyezi Mungu na hukumu yake.
Mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyezi Mungu itafika.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja wenye kukufuru siku ya mwisho sasa anataja mwenye kumwamini. Akamwambia mumin huyu:
Thibiti kwenye imani yako, kwani saa itafika tu hakuna shaka, basi ifanyie kazi.
Naye ni mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Anasikia unayoyasema na anajua unayoyadhamiria na kuyafanya na atakulipa yaliyopita.
Na anayefanya juhudi basi hakika anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi yake.
Tafsiri ya Aya hii ni ile Aya isemayo:
فَمَنْ أَبْصَرَ فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ عَمِيَ فَعَلَيْهَا ۚ {104}
Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu, haumnufaishi utiifu wa mwenye kutii, wala haumdhuru uasi wa mwenye kuasi.
Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, kwa hakika tutawaondolea maovu yao, na tutawalipa mazuri ya waliyokuwa wakiyatenda.
Mwenye kuamini baada ya kukufuru, akawa mwema baada ya kuwa mfisadi, basi Mwenyezi Mungu atamsamehe na kumghufiria yaliyopita. Zaidi ya hayo atapata thawabu kutokana na imani yake na wema wake; sawa na ambaye hana dhambi.
Katika msingi huu wa heri kuna heri zote za utu. Kwa sababu unafungua mlango wa matumaini ya wenye dhambi na makosa na kupata msukumo wa kutubia na kujing’oa kwenye uovu. Hakuna njia nzuri kuliko hii ya kuisafisha jamii na dhulma na ufisadi.
Tena Kuwatendea Wema Wazazi Wawili
Na tumemuusia mtu kuwatendea wema wazazi wake wawili. Na wakikushikilia unishirikishe mimi na yale usiyokuwa na ujuzi nayo, basi usiwatii. Kwangu mimi ndio marejeo yenu, na nitawaambia mnayoyatenda.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameamrisha kuwatendea wema wazazi wawili na kuwatii katika kila kitu isipokuwa katika lile ambalo haliridhii Mwenyezi Mungu Mtukufu; kwani hakuna kumtii kiumbe kwa kumuasia muumba.
Tumelizungumzia kwa ufafanuzi hilo katika Juz. 15 (17:23). Na katika vitabu vya Hadith, kuna kisa kinachofahamisha kuwa kuwatendea wema wazazi wawili kunanufaisha wakati wa shida na pia kwamba dua bora ya kumwelekea Mwenyezi Mungu wakati wa shida ni matendo mema.
Imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.) kwamba watu watatu walingia kwenye pango lililokuwa njiani, wakalala humo. Likaanguka jiwe kubwa kutoka mlimani likawazibia mlango. Baada ya kufikiria sana hawakupata njia isipokuwa kuelekea kwenye dua kumuomba Mwenyezi Mungu peke yake awaokoe na maangamizi haya.
Kisha akakumbuka kila mmoja tendo jema alilolitenda: Wa kwanza, akakumbuka jinsi alivyowatendea wema wazazi wake wawili na kuwapatia raha. Basi jiwe likasogea kidogo. Wa pili akakumbuka kumtekelezea haja mwanamke aliyekuwa na dharura bila ya kufanya naye tendo chafu. Jiwe likasogea tena. Wa tatu akasema kuwa alikuwa na mfanyakazi aliyeondoka bila ya kuchukua mshahara wake. Ule mshahara akauhifadhi na ukazaa, ukawa na wanyama wengi sana, basi akampa mshahara wake na ile ziyada. Hapo jiwe likamalizika kufunguka na wakatoka kwenye pango.
Riwaya hii iwe ni sahihi au la, lakini kisa kinauelezea Uislamu na uhakika wake, kwa sababu unadhibiti njia ya uokovu duniani na akhera kwa matendo mema, sio kwa kauli na kujionyesha.
Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, kwa hakika tutawaingiza katika wema.
Unaweza kuuliza: Kuna tofauti gani kati ya Aya hii na ile iliyotangulia, isemayo: Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, kwa hakika tutawaondolea maovu yao, na tutawalipa mazuri ya waliyokuwa wakiyatenda?
Jibu: Kuingizwa katika kundi la watu wema; kama vile mashahidi na mawalii, ni daraja ya juu zaidi sana kuliko kusamehewa na kulipwa. Ni sawa na kumwambia aliyefanya uovu kisha akatengenea na kuwa mwenye ikhlasi: Nimekusamehe na nitakufanyia wema fulani. Zaidi ya hayo nitakuweka kwenye idadi ya wateuliwa walio bora.
وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّهِ فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّهِ جَعَلَ فِتْنَةَ النَّاسِ كَعَذَابِ اللَّهِ وَلَئِنْ جَاءَ نَصْرٌ مِنْ رَبِّكَ لَيَقُولُنَّ إِنَّا كُنَّا مَعَكُمْ ۚ أَوَلَيْسَ اللَّهُ بِأَعْلَمَ بِمَا فِي صُدُورِ الْعَالَمِينَ {10}
وَلَيَعْلَمَنَّ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْمُنَافِقِينَ {11}
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا اتَّبِعُوا سَبِيلَنَا وَلْنَحْمِلْ خَطَايَاكُمْ وَمَا هُمْ بِحَامِلِينَ مِنْ خَطَايَاهُمْ مِنْ شَيْءٍ ۖ إِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ {12}
وَلَيَحْمِلُنَّ أَثْقَالَهُمْ وَأَثْقَالًا مَعَ أَثْقَالِهِمْ ۖ وَلَيُسْأَلُنَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَمَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ {13}