Aya 41 – 44: Nyumba Dhaifu Zaidi Ni Ya Buibui
Maana
Mfano wa wale ambao wamewafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa buibui aliyejitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu zaidi ni nyumba ya buibui, lau wangelikuwa wanajua.
Kwanza ni lazima tuwajue ni akina nani hao waliowafanya wengine kuwa walinzi badala ya Mwenyezi Mungu? Je ni waabudu mawe na mizimu tu, au ni zaidi ya hao?
Kabla ya kulijibu swali hili, kwanza tukumbuke kauli mbili za Mwenyezi Mungu Mtukufu:
مَنْ كَانَ يُرِيدُ الْعِزَّةَ فَلِلَّهِ الْعِزَّةُ جَمِيعًا ۚ ِ{10}
أَيَبْتَغُونَ عِنْدَهُمُ الْعِزَّةَ فَإِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّهِ جَمِيعًا {139}
Maana ni kuwa hakuna utukufu wa nguvu ya mali, elimu, utawala wala kwa kitu chochote ila ikiwa utasimama kwa misingi ya kumcha Mungu (takua) na radhi yake na yakawa matokeo yake ni kumtii Yeye na matakwa yake.
Elimu ni nguvu, heri na imani ya Mwenyezi Mungu na ubinadamu, ikiwa inaunga mkono haki na uadilifu na nyenzo za kuendeleza maisha. Elimu ni udhaifu, shari na kumkufuru Mungu na ubinadamu, ikiwa ni nyenzo ya dhulma, uchokozi, uvunjaji na uharibifu. Pia mali, utawala n.k. Ni hivyo hivyo.
Baada ya utangulizi huu, tutakuwa tumejua kuwa wale waliowafanya walinzi wengine badala ya Mwenyezi Mungu, ni waabudu masanamu, wanaompinga Mwenyezi Mungu kwa kughurika na mali, elimu au utawala na wenye kufanya ufisadi katika ardhi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amezifananisha nguvu za hawa na nyumba ya buibui ambayo ni dhaifu, isiyoweza kuhimili chochote; hata upepo pia unaweza ukaibomoa.
Kwa maneno mengine ni kuwa kila mwenye kumpinga Mwenyezi Mungu kwa kutegemea mizimu, elimu, mali au utawala, huyo ni katika waliowafanya wengine ni walinzi badala ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kufanya hivyo huyo ni miongoni mwa waliopata hasara.
Anasema Jahidh, katika Kitabu lhayawan (kitabu cha wanyama): “Mtoto wa buibui anaweza kutanda utandabui pale tu anapozaliwa kwa kutumia vitu vya nje sio vinavyotoka ndani mwake na kwamba yeye hutumia utando wake kulitanda windo lake.”
Kila mwenye akili anapaswa kujiuliza nafsi yake na akili yake: Ni nani aliyemjulisha buibui malighafi ya kuweza kutengeneza utando mara tu anapozaliwa? Ni mhandisi gani aliyemchorea nyumba hii yenye umbo la mtego wa wadudu? Je, yote haya yamekuja kwa sadfa? Ikiwa sadfa inaweza kuja mara mbili au tatu, je inaweza kukaririka kwa kila buibui wasio na idadi wanaozaliwa?
Hapana! Hakika Yeye ameumba kila kitu akakilinganisha sawa na akakikadiria na akakiongoza. Ametakata Mwenyezi Mungu Mtukufu na hayo wayasemayo wazushi.
Hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu wanachokiomba badala yake.
Yaani katika mizimu na mengineyo wanayoyategemea badala ya Mwenyezi Mungu; kama vile mali na utawala. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua hakika ya vitu hivi wanavyojikuza navyo na kwamba hivyo haviwatoshi na chochote.
Na Yeye ndiye mwenye nguvu, mwenye hekima.
Mwenye nguvu kwa uweza wake na mwenye hekima katika mipangilio yake.
Na hiyo ni mifano tunawapigia watu na hawaitii akilini ila wenye elimu.
Mifano hiyo ni ile ya buibui na mfano wake na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu anawatanabahisha watu kwenye utukufu wake na umoja wake, lakini mifano hii na mingineyo, katika ishara za Mwenyezi Mungu hawaifahamu isipokuwa wenye akili na busara.
Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi kwa haki.
Yaani kwa njia ya hekima na masilahi; na wala hakuziumba burebure na kwa mchezo. Hekima ya kuumbwa kwake ni kukaliwa na viumbe, wanufaike nayo na wapate dalili, kutokana na usanii wake na maajabu yake juu ya umoja wa Mwenyezi Mungu na utukufu wake.
Hakika katika hayo kuna ishara kwa waumini.
Hayo ya mpangilio na nidhamu ya kuumbwa mbingu na ardhi. Mpangilio huu ni dalili mkataa juu ya umoja wa Mwenyezi Mungu na utukufu wake kwa wale wanaoitafuta haki na kuiamini haki kwa ajili ya haki.