read

Aya 46 – 49: Mjadala Kwa Njia Nzuri

Maana

Njia Ya Mjadala Katika Qur’an

Wala usjadiliane na watu wa Kitabu isipokuwa kwa njia iliyo nzuri kabisa.

Makusudio ya watu wa Kitabu ni mayahudi na manaswara (wakristo). Kujadiliana kwa njia nzuri ni kuwa hoja na dalili ziwe kwa mfumo wa kuvutia sio wa kufukuza, ziwe wazi na sio kufungwa fungwa na kuweko na insafu ya kuusikiliza upande wa pili na kukubaliana nao kwenye lile la haki; ni sawa awe ni katika watu wa Kitabu au wengineo.

Mfano ulio wazi zaidi juu ya hilo ni kauli ya Mwenyezi Mungu kwa washirikina waliosema: “Hakika sisi tuliwakuta baba zetu juu ya desturi; na hakika sisi tunafuata nyayo zao.” Akasema:

أَوَلَوْ جِئْتُكُمْ بِأَهْدَىٰ مِمَّا وَجَدْتُمْ عَلَيْهِ آبَاءَكُمْ ۖ {24}

“Hata nikiwaletea yenye muongozo bora kuliko mliyowakuta nayo baba zenu?” (43:24).

Upole huu wa kusema: ‘Hata nikiwaletea yenye muongozo bora’ unavunja hoja na unaingia katika moyo wa mwenye kusikiliza vizuri.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amehusisha kuwataja watu wa Kitabu, kwa sabubu wao ndio wanaotakiwa kukubali haki haraka kuliko washirikina, kwa vile wao wanamwamini Mungu, malaika wake, vitabu vyake na mitume wake.

Isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao, ambao ni wale walioifanyia inadi haki na wakang’ang’ania upotevu wala hawajitolei kwa hali yoyote. Basi aina hii ya watu wa kitabu muachane nao wala msijadiliane nao katika dini kabisa.

Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an, yenye hekima, ambazo zinawajadili wapinzani na wabatilifu ataona kuwa njia ya mjadala wa kiqur’ani inakuwa kwenye uhuru wa kiakili katika nyanja zote. Uhuru huu unajitokeza pale Qur’an inapoleta dalili mkataa ya usahihi wa madai yake na wajibu wa kuyaamini:

سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنْفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ {53}

Tutawaonyesha ishara Zetu zilizo katika upeo wa mbali, na katika nafsi zao, mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli.” (41:53).

Vile vile uhuru huu unadhihiri pale Qur’an inapomtaka mpinzani atoe dalili za kuutetea msimamo wake:

قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {111}

“Sema: Leteni dalili zenu, kama nyinyi ni wasema kweli” Juz. 1 (2:111).

ائْتُونِي بِكِتَابٍ مِنْ قَبْلِ هَٰذَا أَوْ أَثَارَةٍ مِنْ عِلْمٍ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {4}

“Nileteeni Kitabu kilicho kabla ya hiki au alama yoyote ya ilimu ikiwa mnasema kweli.” (46:4).

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا {33}

Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyo nzuri.”
Juz.21 (25:33).

Huu ndio mjadala wa kiqur’ani ulivyo hasa; kusimamisha hoja kwenye madai yanayohitajia akili, kumtaka hoja anayepinga na kumjibu kwa nguvu ya hoja na fasaha zaidi akiwa ana athari yoyote ya shaka au dalili.

Mtindo huu wa Qur’an umejitokeza kwa mifumo mbali mbali; miongoni mwayo ni hii ifuatayo:

Kutosheka na ubainifu wa jambo na kuchambua maana yake. Qur’an imetumia mfumo huu kuwarudi waabudu masanamu na kuupinga uungu wake; pale ilipoweka wazi kuwa yanashindwa na kitu kidogo:

إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ لَنْ يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ ۖ وَإِنْ يَسْلُبْهُمُ الذُّبَابُ شَيْئًا لَا يَسْتَنْقِذُوهُ مِنْهُ ۚ ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ {73}

“Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu hawatoumba nzi wajapojumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika atakaye na anayetakiwa.” Juz. 17 (22:73).

Yaani vipi mtu anaabudu ambacho hakiwezi kuumba hata nzi?

Vile vile Qur’an imetumia mfumo huu katika kuwarudi wale waliodai kuwa Bwana Masih ni mungu:

مَا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ ۖ كَانَا يَأْكُلَانِ الطَّعَامَ ۗ انْظُرْ كَيْفَ نُبَيِّنُ لَهُمُ الْآيَاتِ ثُمَّ انْظُرْ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ {75}

“Masih mwana wa Maryam hakuwa ila ni Mtume. Wamepita kabla yake Mitume. Na mama yake ni mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyowabainishia ishara, kisha angalia jinsi wanavyogeuzwa.” Juz. 6 (5:75).

Yaani anayekula chakula ni muhitaji na Mungu huwa hahitaji kitu isipokuwa yeye ndiye anayehitajiwa. Tazama Juz. 6 (5:76 – 81).

Kutoa dalili ya kuweko kitu kwa kuweko msabibashaji: Qur’an imeutumia mfumo huu kufahamisha kuweko Mwenyezi Mungu, katika Aya kadhaa zikiwemo hizi:

أَفَلَمْ يَنْظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِنْ فُرُوجٍ {6}

“Je, hawaangalii mbingu zilizo juu yao, vipi tulivyozijenga na tuakazipamba wala hazina nyufa.” (50:6).

Haiwezekani jengo hili lilopangiliwa vizuri na kupambwa na nyota liwe limekuja kwa sadfa. Kwa hiyo imewajibisha kuweko mpangiliaji mwenye hekima. Pia Qur’an imetumia mfumo huu kujulisha umoja wa Mungu pale iliposema:

لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّهُ لَفَسَدَتَا ۚ{22}

“Lau wangelikuwemo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu basi zingefisidika.” Juz. 17 (21:22).

Kwamba kuweko wengi kungeleta ufisadi; na kwa kuwa hakuna ufisadi basi sio wengi. Kwa ibara ya watu wa mantiki ni kuwa kutokuweko linalolazimiana, ambalo ni ufisadi, kunafahamisha kutokuweko linalolazimiwa, ambalo ni kuweko na waungu wengi.

Kutoa dalili kwa umwanzo: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametumia mfumo huu kutoa dalili ya kuweko marejeo ya ufufo katika Aya 27 ya Sura Ar-Rum kwenye Juzuu hii tuliyo nayo: “Naye ndiye ambaye anaanzisha uumbaji kisha ataurudisha na jambo hili ni jepesi zaidi kwake.” Kwamba mwenye kuweza kukifanya kitu bila ya kuweko kitu kingine, basi ana uwezo zaidi kukikusanya tena baada ya kutawanyika.

Mifumo hii yote ni dalili mkataa kwamba mjadala wa kiqur’ani uko kwenye msingi wa kiakili na uhuru wake; na kwamba lengo ni kuidhi- hirisha haki kwa ajili ya kuiamini na kuitumia au kumjibu mwenye kupinga kwa mfumo wa kumkinaisha mwenye kuitafuta haki kwa ajili ya haki.

Na semeni: Tumeamini yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni mmoja na sisi ni wenye kusilimu kwake.

Maneno yanaelekezwa kwa waislamu. Maana ni kuwa enyi waislamu! Kama ilivyokuwa wajibu kwenu kujadiliana vizuri na yule mnayemtarajia katika watu wa Kitabu, vile vile msiwaonyeshe uadui; bali mchanganyike nao na muwaambie tunayemwabudu sisi ndiye mnayemwabudu nyinyi. Sisi tunamwamini yeye na tunaamini Tawrat iliyoteremshwa kwa Musa na Injil iliyotermshwa kwa Isa; sawa na tunavyoiamini Qur’an iliyoteremshwa kwa Muhammad. Kwa maneno mengine ni: kuweni kwa uislmu ni pambo wala msiwe ni fedheha.

Na hivyo ndio tumekuteremshia Kitabu.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.). Makusudio ya Kitabu ni Qur’an. Maana ni kuwa, kama tulivyomteremshia Musa Tawrat na Isa tukamtermshia Injil, kabla yako, vile vile nawe tumekuteremshia Qur’an.

Basi wale ambao tumewapa Kitabu wanakiamini.

Hii ni kuwaishiria wale waliosilimu katika mayahudi na manaswara.

Na miongoni mwa hao wako wanaokiamini.

Ni ishara ya wale waliosilimu katika washirikina wa kiarabu.

Na hawazikatai ishara zetu isipokuwa makafiri.

Unaweza kuuliza kuwa kukataa ndio kukufuru; hapo basi maana yatakuwa hawazikatai ila wakataaji; sawa na kusema: Hakai ila mkaaji. Na Qur’an haiko hivi?

Jibu: Makusudio ni kuwa dalili za ukweli wa Qur’an ziko wazi kiasi ambacho hawezi kuzipinga, isipokuwa aliyeifanya batili ndio dini. Na ukafiri ni itikadi, mwenye nayo haiachi hata kama ubatilifu wake utadhihiri kama jua; sawa na mayahudi walioambiana: “Wala msimwamini ila yule anayefuata dini yenu.” Juz. 3 (3:73).

Na hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kuume. Ingelikuwa hivyo wangelifanya shaka wabatilifu.

Wameafikiana wana historia kuwa Muhammad (s.a.w.) hakusoma kwa mwalimu yoyote, mkubwa wala mdogo. Lakini pamoja na hivyo ameleta Qur’an iliyo muujiza wa miujiza katika itiakadi yake, sharia yake, mafunzo yake, misingi yake yote, kuwatolea habari mitume waliotangulia na mengineyo.

Hii ni dalili tosha kuwa hiyo ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, haikutengenezwa na mtu.

Lau Mtume (s.a.w.) angeliandika na kusoma au akawa amesoma kwa mwalimu, wazushi wangesema kuwa Qur’an imetungwa na Muhammad, si wahyi wa Mwenyezi Mungu.

Kuna mmoja alisema Muhammad (s.a.w.) amechukua Qur’an kutoka kwa mtawa wa kinaswara huko Sham. Hatujui ameyatoa wapi haya? Sijui atasemaje kuhusu Aya hizi:

لَقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّهَ ثَالِثُ ثَلَاثَةٍ ۘ {73}

“Kwa hakika wamekufuru wale waliosema, Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa utatu.” Juz.6 (5:73).

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِنْ دُونِ اللَّهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَٰهًا وَاحِدًا ۖ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ {31}

Wamefanya makuhani wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu na Masih mwana wa Maryam. Wala hawakuamrishwa isipokuwa wamwambudu Mungu mmoja hakuna Mungu ila yeye. Ametakata na wanayomshirikisha nayo.” Juz. 10 (9:31).

Tazama kifungu cha ‘Qur’an na wanaohubiri utatu’ katika Juz. 6 (4:171 – 173).

Bali hicho ni ishara zilizo wazi katika vifua vya waliopewa ilimu; na hawazikatai ishara zetu isipokuwa madhalimu.

Hapana! Qur’an haikutengenezwa na Muhammad (s.a.w.), bali ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu wanaiamini na kuitegemea wale wanaotafuta ilimu kwa imani ya haki na kuitumia.

Ama wale ambao wameifanya ilimu ni duka la biashara, basi wataipinga, kwa sababu inapiga vita unafiki na ukandamizaji.

وَقَالُوا لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ آيَاتٌ مِنْ رَبِّهِ ۖ قُلْ إِنَّمَا الْآيَاتُ عِنْدَ اللَّهِ وَإِنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُبِينٌ {50}

Na walisema: Mbona hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake? Sema: Hakika ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; na mimi kwa hakika ni muonyaji mwenye kubain- isha tu.

أَوَلَمْ يَكْفِهِمْ أَنَّا أَنْزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَرَحْمَةً وَذِكْرَىٰ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ {51}

Je, kwani hayakuwatosha kwamba tumekuteremshia Kitabu wanachosomewa? Hakika katika hiyo kuna rehema na mawaidha kwa watu wanaoamini.

قُلْ كَفَىٰ بِاللَّهِ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ شَهِيدًا ۖ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَالَّذِينَ آمَنُوا بِالْبَاطِلِ وَكَفَرُوا بِاللَّهِ أُولَٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ {52}

Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni shahidi baina yangu na nyinyi, anajua yaliyomo mbinguni na ardhini. Na wale ambao wameamini batili na wakamkufuru, hao ndio waliopata hasara.

وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ ۚ وَلَوْلَا أَجَلٌ مُسَمًّى لَجَاءَهُمُ الْعَذَابُ وَلَيَأْتِيَنَّهُمْ بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ {53}

Na wanakuhimiza adhabu. Na lau si wakati maalum uliowekwa, basi adhabu ingeliwajia na hakika ingeliwatokea ghafla na hali wao hawatambui.

يَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ {54}

Wanakuhimiza adhabu na hali Jahannam kwa hakika imewazunguka makafiri.

يَوْمَ يَغْشَاهُمُ الْعَذَابُ مِنْ فَوْقِهِمْ وَمِنْ تَحْتِ أَرْجُلِهِمْ وَيَقُولُ ذُوقُوا مَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {55}

Siku itakayowafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu yao na atasema: Onjeni mliyokuwa mkiyatenda.