Aya 56 – 63: Wanyama Wangapi Hawabebi Riziki Zao
Maana
Enyi waja wangu mlioamini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa, basi niabuduni mimi tu.
Wameafikiana mafaqihi kuwa haijuzu kwa Mwislamu kukaa katika mji ambao itakuwa uzito kwake kutekeleza wajibu wa kidini; kama vile Swala na mfano wake; hata kama mji huo ndio nyumbani kwake; na kwamba ni lazima ahame kwenda mahali pengine atakapoweza kutekeleza hayo. Tumezungumzia kwa ufafanuzi zaidi maudhui haya katika Juz. 5 (4:97) kifungu ‘Mafaqihi na wajibu wa hijra’.
Kila nafsi itaonja mauti, kisha mtarudishwa kwetu.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwajibisha kuhama mji uliotajwa, alisema kuwa anayehofia kufa uhamishoni, basi hawezi kuokoka na mauti popote pale alipo, nyumbani au ugenini. Na baada ya kufa ataulizwa wajibu aliouacha na mambo ya haramu aliyoyafanya; yakiwemo kukaa kwenye mji anaolazimika kuacha ibada na kunywa pombe.
Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, bila shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yapitiwayo na mito chini yake wadumu humo.
Atakayetoka nyumbani kwake kwa kufanya Hijra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi Mungu atampa badali bora zaidi yake – ghorofa, miti, na mito katika nyumba na makazi ya amani.
Ni neema iliyoje kwa malipo ya watendaji. Ambao walisubiri na kwa Mola wao wanategemea.
Kuna malipo gani zaidi ya Pepo? Kwa vile ni adhimu basi nayo thamani yake iko ghali na adhimu. Thamani yenyewe ni: kukataa kujisalimisha kwa maadui wa Mwenyezi Mungu, kutomhofia yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake na kuwa na subira kwa ajili yake katika matukio yote, vyovyote yatakavyokuwa.
Riziki Na Kumtegemea Muumba Na Si Kiumbe
Wanyama wangapi hawabebi riziki zao. Mwenyezi Mungu anawaruzuku wao na nyinyi. Na Yeye ni Msikizi, Mjuzi.
Watu wengi wanamwamini Mwenyezi Mungu kinadharia; kwamba riziki za viumbe ziko mikononi mwake Yeye peke yake, kwamba hazina yake haishi wala haina ukomo na kwamba Yeye ni mkarimu, hakosi kitu anayemwamini na kumtegemea Yeye.
Wanaamini haya yote kinadharia, lakini wanamkana Mungu kimatendo; wanamtegea kumbe badala ya Muumba na wanajikurubisha kwa kimbe kwa mambo yanayoiondoa dini yao na dhamiri yao kwa kuwa na tamaa ya vilivyo mikononi mwake na wanajiweka mbali na Mwenyezi Mungu wakikata tamaa naye na hazina yake.
Aya hii inamkemea mumin huyu aliye kafiri.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni Muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake, aina zote za sababu za riziki zinakomea kwake; nazo ziko tayari kwa kila mwenye kuzitaka na kuzihangaikia. Ikiwa zitakuwa nzito basi zinajiandaa kwa mhitaji kwa ubora zaidi bila ya kutambua; bali viumbe hai vingi haviifanyii kazi riziki wala kuibeba, lakini inawajia pale wanapoihitajia.
Hapa kuna mazingatio kwa vibaraka wahaini na kila mwenye kuiuza dini yake kwa shetani na akayafanya maasi ndio nyenzo ya kupata tonge.
Hasha! Haiwezekeni kwa Mwenyezi Mungu kukataza kitu na azuie sababu za riziki. Vipi iwe hivyo na hali dini yake ni dini ya maisha? Imam Ali (a.s.) anasema: “Hakika lile mliloamrishwa lina wasaa zaidi kuliko lile mlilokatazwa na mliyohalalishiwa ni mengi zaidi ya mliyoharamishiwa. Basi acheni yaliyo machache kwa ajili ya yaliyo mengi. Na yaliyo dhiki kwa ajili ya yaliyo na wasaa.”
Akasema tena: “Kuamrisha mema na kukataza mabaya ni maumbile mawili katika viumbe vya Mwenyezi Mungu na kwamba hayo hayakarubishi ajali wala hayapunguzi riziki.”
Huko nyuma tumeweka wazi tofauti baina ya imani ya kweli na imani ya mawazo. Kwamba imani ya kweli ni ile iliyothibiti kwenye moyo na ikaleta kumhofia Mwenyezi Mungu na kujihimu na twaa yake na radhi yake kwa kauli na vitendo.
Lakini imani ya kuwazia haithibiti moyoni; isipokuwa imerambwa na ulimi, na inakuwa ni ya kuwazia tu, sawa na njozi. Ushahidi mkubwa wa imani hii ya kombokombo ni kuwa mtu anamwamini Mwenyezi Mungu kwa kauli na huku anamtarajia kiumbe na kumhofia badala ya Mwenyezi Mungu.
Na ukiwauliza ni nani aliyemba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi, bila shaka watasema ni Mwenyezi Mungu.
Wanaoulizwa ni wapenda anasa waliokaidi risala ya Muhammad (s.a.w.).
Unaweza kuuliza ikiwa wanakubali waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye muumba wa ulimwengu, basi iko wapi sababu ya kupin- gana kwao na mitume?
Jibu: Kimsingi wao wanamkubali Mwenyezi Mungu na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyewahusu wao kwa mali na utawala na akawachagulia wengine ufukara na utumwa.
Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu na akaamini kuwa watu wana anayostahiki juu yake na yeye ana anayostahiki juu ya watu, basi huyu ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko huyo anayeamini bila ya matendo
Dalili ya kuwa wao wanamkubali Mwenyezi Mungu kwenye msingi huu ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na wanapoambiwa: Toeni katika yale aliyowapa Mwenyezi Mungu, wale waliokufuru huwambia walioamini: Je, tumlishe ambaye Mwenyezi Mungu akipenda atamlisha? Nyinyi hammo ila katika upotevu dhahiri” (36:47).
Basi wanageuzwa wapi?
Wanaigeuka haki kwa kuzua kuwa Mwenyezi Mungu amewahusu wao tu kuwa na mali kuliko wengine wote.
Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake na humdhikisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:26).
Na ukiwauliza ni nani aliyeteremsha maji kutoka mbinguni na akahuisha kwayo ardhi baada ya kufa kwake, bila shaka watasema ni Mwenyezi Mungu.
Wakiulizwa kuhusu mumbaji wa ulimwengu wanajibu kwa kukabali kuwa ni Mwenyezi Mungu lakini kwa masharti yao. Na wakiulizwa aliyeteremsha maji na akahuisha ardhi, ambayo ndiyo sababu ya moja kwa moja ya riziki na utajiri ulio mikononi mwao, pia wanasema na kukubali kuwa ni Mwenyezi Mungu peke yake.
Hapo wanajipinga wao wenyewe. Ikiwa sababu za riziki ziko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na si mikononi mwao, itakuwaje iwe yao tu peke yao na wengine wasipate? Ikiwa Mwenyezi Mungu ni wa wote, vipi heri zake na baraka zake?
Sema: Alhamdulillah (sifa njema ni za Mwenyezi Mungu), ambaye ameidhihirisha haki hata kupitia mdomoni mwa maadui zake wazushi.
Bali wengi wao hawafahamu kwamba wao ni waongo na wazushi wakijipinga wao wenyewe kwa wenyewe.
وَمَا هَٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَهْوٌ وَلَعِبٌ ۚ وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ {64}
فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ {65}
لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ وَلِيَتَمَتَّعُوا ۖ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ {66}
أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا حَرَمًا آمِنًا وَيُتَخَطَّفُ النَّاسُ مِنْ حَوْلِهِمْ ۚ أَفَبِالْبَاطِلِ يُؤْمِنُونَ وَبِنِعْمَةِ اللَّهِ يَكْفُرُونَ {67}
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّهِ كَذِبًا أَوْ كَذَّبَ بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِلْكَافِرِينَ {68}
وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا ۚ وَإِنَّ اللَّهَ لَمَعَ الْمُحْسِنِينَ {69}