Aya 64 – 69: Dunia Ni Upuuzi Na Mchezo
Maana
Na maisha haya ya dunia si chochote ila ni upuuzi na mchezo.
Makusudio ya dunia hapa ni dunia ya uzembe, uovu, kujifaharisha na israfu kwa hisabu ya wanyonge. Vile vile dunia ya wakoloni na wazayuni waundaji wa mauti, njama za kiuadui na mapinduzi ya kijinga. Dunia ya mashirika ya ulanguzi, unyonyaji, na kuifanyia biashara dini.
Dunia ya vyombo vya habari vya kulipwa ili kutia sumu kwenye fikra na kuvungavunga kuuficha ukweli na propaganda za uwongo.
Hii ndio dunia ya mchezo, ufisadi shari na upotevu, inayomchukiza Mwenyezi Mungu na kuwaandalia wakazi wake adhabu ya kuunguza. Ama dunia ya watu wema, walio huru, waungwana ambao wanaleta masilahi katika nchi na sio ufisadi. Hii ndio dunia ya haki, heri, uongofu na kufaulu ambayo wakazi wake watapata radhi za Mwenyezi Mungu na kufuzu kwa neema yake na Pepo yake.
Na nyumba ya akhera ndiyo maisha hasa, lau wangelikuwa wanajua.
Tunaifasiri kwa kauli yake Imam Ali (a.s.): “Kila neema isiyokuwa Pepo ni upuzi na kila balaa isiyokuwa moto ni faraja.” Na kauli yake katika wasifa wa Pepo “Haikatiki neema yake, haondoki mkazi wake, hazeeki anayedumu humo, wala kukata tamaa anayekaa humo.”
Na wanapopanda katika jahazi, humwomba kwa kumsafia utiifu, lakini anapowavua wakafika nchi kavu mara wanamshirikisha.
Inasemekana kuwa watu wa wakati wa jahiliya walikuwa wanaposafiri baharini huchukua masanamu yao. Dhoruba ikawakumba wanayatupa masanamu na kusema: Yarabi yarabi! (Ewe Mola ewe Mola!). Hili si ajabu. Wengine walikuwa wakitengeneza sanamu ya tende, wakishikwa na njaa wanaila.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:22). Ni vizuri kurudia tuliyoyaandika huko kwenye kifungu ‘Mwenyezi Mungu na maumbile.’
Ili wapate kuyakana tuliyowapa na wapate kustarehe, punde watajua.
Yaani wapate kuacha kushukuru kwa neema ya kuokoka aliyoaneemesha Mwenyezi Mungu kwa ukarimu wake na upole. Basi wataona hizaya ya adhabu itakayowapata kesho.
Je, hawaoni kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani na hali watu wa pambizoni mwake wananyakuliwa.
Wanaambiwa washirikina wa Makka ambao wamempiga vita Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Hiyo ni kutokana na neno ‘Nchi takatifu ina amani.’ Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawakumbusha yale aliyowahusu nayo kuliko watu wengine; kwa kukaa katika mji wenye amani ya nafsi na mali; na jirani zao wanaishi na hofu na wasiwasi wa maisha yao na vitu vyao.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:125), Juz. 4 (3:97) na Juz. 20 (28:57).
Je, wataamini batili na kuzikataa neema za Mwenyezi Mungu?
Kila anayenyenyekea batili na akaridhia yasiyokuwa haki kwa tamaa ya dunia, basi yeye ni katika anayeamini batili na kuzikana fadhila za Mwenyezi Mungu na hisani yake.
Na ni nani dhalimu zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uwongo. Au akadhibishaye haki inapomjia? Je, si katika Jahannam ndio yatakuwa makazi ya makafiri?
Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:21).
Na wale wanaofanya juhudi kwa ajili yetu, hakika tutawongoza kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wema.
Juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni mambo mengi; miongoni mwayo ni: kutafuta ilimu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kutafuta maisha kwa jasho, kuamrisha mema na kukataza maovu. Ilivyeo bora kabisa kuliko yote ni kuisafisha ardhi na madhalimu na wafisadi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamwongoza kwenye haki kila Mwenye kum- fanyia ikhlasi katika nia yake na akafanya uzuri katika matendo yake, wala hamuongozi Mwenye kufanya israfu aliye muongo.