Aya 17 – 25.: Ushahidi Wa Ulimwengu Na Kuumbwa Mtu
Maana
Basi mtakaseni Mwenyezi Mungu mnapofikia jioni na mnapofikia asubuhi. Na sifa njema zote ni zake katika mbingu na ardhi na jioni na na mnapofikia mchana.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja watu wa Peponi na watu wa Motoni, anatoa amri ya kutukuzwa kwake asubuhi, jioni, mchana na usiku pia. Kwani Hakika Yeye Mwenyezi Mungu ni msifiwa mbinguni na ardhini.
Kuna riwaya moja inayosema kuwa Suleiman Bin Daud, siku moja alimpi- tia mkulima akasema: “Hakika Bin Daud amepewa ufalme mkubwa.”
Suleiman akamwambia: “Tasbih moja tu anayoikubali Mwenyezi Mungu ni bora kuliko waliyopewa ukoo wa Daud.”
Kwenye Nahjul-balagha, imeelezwa: “Mwenyezi Mungu Amejaalia Alhamdu (kusifiwa na sifa njema) ni ufunguo wa utajo wake na ni sababu ya kuzidi fadhila zake na ni dalili ya uungu wake na utukufu wake.
Hukitoa kilicho hai kutokana na kilichokufa, na hukitoa kilichokufa kutokana na kilicho hai. Na huhuisha ardhi baada ya kufa kwake.
Wanaoamini mada wanasema kuwa mada ndiyo iliyoleta uhai, usikikizi, nyoyo n.k. Kama yangekuwa sahihi haya, basi ingelikuwa kila mada inaona, kusikia na kuwa na akili. Kwa sababu vinavyohusiana na kitu ni lazima viwe navyo wakati wowote. Na kwa kuwa tunaona mada nyingine zina uhai na nyingine hazina, basi tumejua kwamba kuna nguvu nyuma ya mada inayompa uhai amtakaye na kutompa amtakaye.
Na kama hivyo ndivyo mtakavyotolewa.
Yaani kufufuliwa. Kama ambavyo Mwenyezi Mungu ameitoa mimea hai kutokana na ardhi iliyokufa, atamtoa mtu hai kutoka kaburini kwake. Kwa maneno mengine ni kuwa; kama ambavyo alimpa uhai baada ya kuwa si chochote, vilevile atampa uhai mara nyingine baada ya kuwa ni mchanga na mifupa. Basi je, kuna ajabu gani?
Tazama Juz. 7 (6:95 – 99) na Juz. 13 (13:5 – 7) kifungu cha ‘Waanaoamini mada na maisha baada ya mauti.’
Na katika ishara zake ni kuwa amewaumba kwa udongo; kisha mmekuwa watu mnaoenea.
Mwenyezi Mungu amemuumba mtu wa kwanza kutokana na udongo na watu wote wametokana na yeye. Vile vile chakula chao kinachowafanya waishi kinatokana na udongo.
Kwa hiyo, udongo ndio sababu ya kupatikana mtu na kubakia kwake na kuendelea kwake. Vipi mchanga umekuwa mtu mwenye usikizi, uoni, akili, ubainifu, utashi na nguvu zinazofanya maajabu mengi na kuleta maendeleo?
Je, haya ni matengenezo ya sadfa au mada? Na waseme wapinzani watakavyo, lakini akili haiamini isipokuwa kuweko ambaye hana mfano na kitu chochote na ni Mjuzi, Mwenye hekima.
Ndoa Ya Ki-Qur’an
Na katika ishara zake ni kuwaumbia wake zenu kutokana na nafsi zenu. Ili mpate utulivu kwao. Na akajaalia mapenzi na huruma baina yenu.
Maana ya ‘Kutokana na nafsi zenu’ ni jinsi yenu na maumbo yenu; mkibadilishana upendo kwa upendo na utulivu kwa utulivu. Wakale walisema: “Kila shepu inazoena na shepu inayofanana nayo.” Lau mke angelikuwa wa jinsi nyingine inayotofautiana na jinsi ya mume, ingelikuwa vigumu kufahamiana na kushirikiana. Kila mmoja angejiona ni mgeni kwa mwenzake na yuko mbali na tabia yake na hulka yake. Tazama Juz. 4 (4:19 – 21) kifungu cha ‘Ndoa ni kubadilishana roho kwa roho.’
Ya kushangaza ni kauli ya baadhi ya wafasiri waliosema kuwa makusudio ya mapenzi ni kujamiiana; na huruma ni mtoto. Hii inafahamisha tu kuwa wafasiri hao wameelemea zaidi upande wa mambo ya kijinsiya na kumuona mwanamke kuwa ni chombo cha kuzaa watoto tu.
Qur’an Tukufu imeabainisha lengo la ndoa kuwa ni kuzoeana, kuhurumiana, uadilifu na usawa; sio baina ya mume na mke tu, bali familia nzima kwa ujumla. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Enyi watu! Mcheni Mwenyezi Mungu ambaye amewaumba kutokana na nafsi moja.
Na akamuumba mkewe katika nafsi hiyo na akaeneza, kutokana na hao wawili, wanaume wengi na wanawake. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana na ndugu wa damu; hakika Mwenyezi Mungu anawachunga.” Juz. 4 (4:1).
Lengo la kumcha Mwenyezi Mungu katika Aya hii ni kila mmoja katika familia atekeleze haki ya mwenzake, ili familia iwe na maisha mazuri yasiyokuwa na misukosuko wala vikwazo. Inajulikana wazi kuwa familia njema ndio msingi wa jamii njema.
Si vibaya kudokeza kuwa ni Sunna kusoma khutuba ya ndoa wakati wa kutaka kuoa, na wakati wa kusomwa tamko la ndoa kwa kumwiga Mtume (s.a.w.) na kizazi chake. Khutba yenyewe inakuwa ni kumhimidi Mwenyezi Mungu Mtukufu, shahada mbili, kumswalia Mtume na kizazi chake, kuwausia watu takua na kuwaombea Mungu wana ndoa. Imepokewa Hadith kutoka kwa Imam Zainul-abidin: “Mwenye kumhimidi Mwenyezi Mungu amehutubia.”
Vile vile ni Sunna kutabaruku kwa kusoma Aya za Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume wake Mtukufu. Hii imekuwa ni desturi ya wahenga na wa sasa.
Huwa kabla ya kufungisha ndoa wanasoma Aya hii tuliyo nayo. Na katika Hadith wanasoma “Owaneni mtapata kizazi na kuwa wengi. Kwani mimi nitajifaharisha kwa umma nyingine siku ya Kiyama hata kwa mimba iliyoharibika.”
Tumesema kuwa Aya na Hadith hizi zinasomwa kwa kutabaruku tu. Ni makosa kudhaniwa kuwa tabia njema na adabu za Qur’an zitapatikana kwa kusoma Hadith na Aya. Hapana! Tabia njema na adabu zitakuwa kwa malezi tu ya kumlea mtoto ki-qur’ani tangu udogoni; jambo ambalo litampelekea kufahamu lengo alilolikusudia Mwenyezi Mungu katika ndoa.
Ama kuwalea watoto juu ya kupenda mali na kujifharisha na mambo ya kujionyesha ya upuuzi; kama mama kumwambia binti yake: Mungu akujalie upate mume tajiri au baba kumpa nasaha mwanawe kuoa binti wa waziri au wa mfanya biashara mkubwa, malezi haya hayafaidiwi chochote na kusoma Qur’an wala Hadithi.
Hadithi ya owaneni mtapata kizazi, haina shaka yoyote katika usahihi wake, lakini Bwana wa Mitume (s.a.w.) atajifaharisha kwa waumini wenye takua na wapigania jihadi waungwana na vile vile kwa mimba iliyoharibika. Na atajitenga na waovu wenye ufuska katika vijana wa kike na wa kiume, ambao dini haiwakanyi na lolote.
Vile vile atajitenga na wahaini na vibaraka walio maadui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu. Kuna Hadith isemayo: “Kwa hakika watu watafikiwa na wakati ambao mtu hatasalimika na dini ila kwa kukimbia kutoka kilele kimoja hadi kingine.” Wakasema: “Yatakuwa lini hayo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema: ”Itakapokuwa mtu hapati maisha ila kwa kumuasi Mwenyezi Mungu, basi wakati huo itakuwa halali useja.”
Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaofikiri.
Lengo la ndoa ni utulivu, mapenzi na kuhurumiana; na kwamba ndoa za kibiashara na kisiasa mara nyingi zinaishia kwenye maisha mabaya ya kifamilia na hatimaye kuvunjika na watoto kutangatanga.
Na katika ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi.
Mwenyezi Mungu anakariri ishara ya kuumbwa ulimwengu, kwa sababu huo pamoja na maajabu na siri zilizomo ndani yake ni katika dalili zilizo dhahiri zaidi za kuweko Mwenyezi Mungu. Vile vile kukumbusha fadhila zake Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na kutofautiana ndimi zenu na rangi zenu.
Yaani kutofautiana lugha na rangi za watu. Pia kuna watu wanatofautiana kwa sura, sauti, alama za vidole n.k. Hekima ya hilo ni kujuana watu na kuwatofautisha. Mzazi amjue mwanawe, mume amjue mkewe, mdai amjue anayemdai n.k. Haiwezekani kabisa kuwa hekima hii ya hali ya juu iwe imepatikana kwa sadfa.
Hakika katika hayo kuna ishara kwa wenye elimu.
Yaanikunadaliliwazizakuwekomkadiriajinampangiliajimambo.
Na katika ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake.
Mtu anaweza kulala mchana wakati wa adhuhuri (qaylula) na pia anaweza kutafuta riziki usiku. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu
وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا {10}
وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا {11}
Vyovyote iwavyo, lengo ni kukumbusha hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kuyagawanya maisha ya mtu kwenye mateso na raha, ambapo maisha hayawezi kupangika bila ya mawili hayo.
Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaosikia mwito wa Mwenyezi Mungu wakauitikia na mawaidha wakawaidhika nayo.
Na katika Ishara zake ni kuwaonyesha umeme kwa hofu na tamaa na kuwateremshia maji kutoka mbinguni na kwayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wenye akili.
Umepita mfano wake katika Juz. 13 (13:12).
Na katika Ishara zake ni kusimama mbingu kwa amri yake.
Kila kitu kinamhitajia Mwenyezi Mungu katika kubaki kwake na kuendelea kwake; sawa na kilivyomuhitajia katika kuumbwa kwake. Kikikosa ulinzi wake, basi kitakuwa ni bure tu kisicho na maana yoyote.
Kisha atakapowaita mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye ardhi.
Wito wa Mwenyezi Mungu duniani ni wito wa nasaha na mwongozo, wanauitikia wenye takua na kuupinga wakosefu. Ama mwito wake huko akhera ni wakiutekelezaji, asioweza kuukimbia yoyote. Umetukuka uweza wake.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:52).
وَلَهُ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ كُلٌّ لَهُ قَانِتُونَ {26}
وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ ۚ وَلَهُ الْمَثَلُ الْأَعْلَىٰ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ {27}
ضَرَبَ لَكُمْ مَثَلًا مِنْ أَنْفُسِكُمْ ۖ هَلْ لَكُمْ مِنْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ مِنْ شُرَكَاءَ فِي مَا رَزَقْنَاكُمْ فَأَنْتُمْ فِيهِ سَوَاءٌ تَخَافُونَهُمْ كَخِيفَتِكُمْ أَنْفُسَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ {28}
بَلِ اتَّبَعَ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَهْوَاءَهُمْ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۖ فَمَنْ يَهْدِي مَنْ أَضَلَّ اللَّهُ ۖ وَمَا لَهُمْ مِنْ نَاصِرِينَ {29}