read

Aya 30 – 32: Dini Ya Sawasawa

Maana

Dini Ya Mwenyezi Mungu Na Maumbile

Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye dini–ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo dini ya sawasawa, lakini watu wengi hawajui.

Aya hii, mara nyingi, inakuwa vinywani mwa mahatibu na kwenye kalamu za waandishi. Kuna wale wanaotosheka na kuitolea dalili tu. Wengine wanaipamba wakisema: Hii ndio dini iliyo sahihi iliyo kubwa n.k.

Bila shaka Aya hii inathibisha msingi unaotiliwa mkazo na itikadi ya Kiislamu na sharia yake. Na inafahamisha wazi kwamba mafunzo ya dini kuanzia alifu mpaka ye (a mpaka z) yanaongoza kwenye uongofu na utekelezaji wa matakwa ya maisha, ukuaji na maendeleo yake.

Kwanza tutanza kufasiri misamiati iliyo katika Aya hii, kisha tutaja maana kijumla.

Neno umbile kwa ujumla linamanisha tabia iliyo ndani ya mtu, inayoikubali kheri inapoijua kuwa ni kheri na kulazimiana nayo kwa vile tu kheri inakubalika. Na tabia hiyo inaikataa shari inapoijua kuwa ni shari, si kwa jingine ila ni kwamba shari inakataliwa na kuepukwa.

Hii ni itakapokuwa umbile la mtu ni safi, halina takataka za desturi na uuigizaji wala halikuchafuliwa na hawaa. Mwanchuoni mkuu Hilli (Allama Hilli) ameipigia mfano tabia hii kwa kusema: “Lau mwenye akili atahiyarishwa kusema ukweli na apewe pesa au aseme uwongo pia apewe pesa, basi atachagua ukweli.”

Tabia hii inayochagua ukweli kuliko uongo ndio ile aliyoizungumzia Mwenyezi Mungu pale aliposema: “Je, mimi si Mola wenu? Wakasema: Kwa nini!” Juz. 9 (7:152). Pia ndiyo iliyokusudiwa na Hadith mashuhuri iliyopokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.): “Kila anayezaliwa anazaliwa na umbile mpaka wazazi wake wamfanye Yahudi au Mnaswara.”

Ama neno ‘kwenye dini’ hapa linamanisha msimamo wa umbile ambalo Mwenyezi Mungu amewaumbia watu la kuwa mbali na hawaa za nafsi.

Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu,” ni kuwa dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuthibiti kwa msingi wa kimaumbile, hauepukani nayo.

Neno ‘Hiyo’ ni ishara ya yale aliyoyawajibisha Mwenyezi Mungu kwa waja kulazimiana nayo kwa kauli na vitendo. Kwa sababu ndiyo dini ya kisawasawa isiyokuwa na kombokombo.

Ama kwa ujumla wake inafahamisha kuwa dini inafungamana na maumbile ya mtu, lakini hii haimaanishi kuwa umbile ndilo muamrishaji na mkatazaji na dini ielezee hukumu zake, hapana! Mwenyezi Mungu ambaye ameumba dini na maumbile ndiye muweka sharia wa kwanza. Ni Yeye pekee mwenye kuamrisha na kukataza.

Hakika makusudio ya Aya ni kuelezea kipimo tunachopimia dini ya Mwenyezi Mungu na kwamba itikidi, sharia na maadili yake yanenda sambamba na umbile la watu na masilahi yao; na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuweka hukumu kwa waja wake kupingana na manufaa ya mtu binafsi au jamii.
Huu ndio udhibiti na tofauti iliyoko baina ya hukumu ya Mwenyezi Mungu na hukumu nyinginezo, tofauti baina ya sharia ya haki na sharia ya batili. Ama kauli za maulama wa fiqih, tafsir na falsafa sio msingi wa Uislamu, wala haifai kuwategemea kama dalili ya sharia. Kwa sabau kauli zao hizo zinaakisi tu juhudi na fahamu zao katika dini ya Mwenyezi Mungu na hukumu zake, wala haziakisi uhakika na uhalisi wa dini.

Kwa ufupi ni kuwa Uislamu haukatai yote yaliyo katika dini na madhehbu mengineyo; bali unaangalia kwa mtazamo wa undani na usanifu. Unakubaliana yale yanayoafikiana na umbile la Mwenyezi Mungu na kukataa yasiyokuwa hayo.

Muwe wenye kurejea kwake na mcheni. Rudini kwenye dini hii na mtii hukumu zake zote.

Na simamisheni Swala kwani inawakumbusha Mwenyezi Mungu; wala msiwe katika washirikina.

Mfanyieni ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake kwenye kauli zenu na vitendo vyenu.

Katika wale walioigawa dini yao na wakawa makundi makundi. Kila kundi hufurahia waliyo nayo.

UmepitamfanowakekatikaJuz.8(6:158)naJuz.18(23:53).

وَإِذَا مَسَّ النَّاسَ ضُرٌّ دَعَوْا رَبَّهُمْ مُنِيبِينَ إِلَيْهِ ثُمَّ إِذَا أَذَاقَهُمْ مِنْهُ رَحْمَةً إِذَا فَرِيقٌ مِنْهُمْ بِرَبِّهِمْ يُشْرِكُونَ {33}

Watu yakiwagusa madhara humwomba Mola wao wakiwa wanarejea kwake. Kisha akiwaonjesha rehema kutoka kwake, mara kikundi miongoni mwao humshirikisha Mola wao.

لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ ۚ فَتَمَتَّعُوا فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ {34}

Ili wapate kuyakana tuliyowapa. Basi stareheni. Mtakuja jua.

أَمْ أَنْزَلْنَا عَلَيْهِمْ سُلْطَانًا فَهُوَ يَتَكَلَّمُ بِمَا كَانُوا بِهِ يُشْرِكُونَ {35}

Au tumewateremshia hoja inayowaambia juu ya yale wamshirikishayo nayo?

وَإِذَا أَذَقْنَا النَّاسَ رَحْمَةً فَرِحُوا بِهَا ۖ وَإِنْ تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ إِذَا هُمْ يَقْنَطُونَ {36}

Na watu tunapowaonjesha rehema huifurahia. Na ukiwasibu uovu kwa iliyoyatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa.

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّهَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَنْ يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ {37}

Je, hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaoamini.

فَآتِ ذَا الْقُرْبَىٰ حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ لِلَّذِينَ يُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّهِ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ {38}

Basi mpe jamaa haki yake na masikini na mwananjia. Hayo ni kheri kwa wale watakao radhi ya Mwenyezi Mungu na hao ndio wenye kufanikiwa.

وَمَا آتَيْتُمْ مِنْ رِبًا لِيَرْبُوَ فِي أَمْوَالِ النَّاسِ فَلَا يَرْبُو عِنْدَ اللَّهِ ۖ وَمَا آتَيْتُمْ مِنْ زَكَاةٍ تُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّهِ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُضْعِفُونَ {39}

Na mnachokitoa katika riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mlichokitoa Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watakaozidishiwa.

اللَّهُ الَّذِي خَلَقَكُمْ ثُمَّ رَزَقَكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ۖ هَلْ مِنْ شُرَكَائِكُمْ مَنْ يَفْعَلُ مِنْ ذَٰلِكُمْ مِنْ شَيْءٍ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ {40}

Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba, kisha akawaruzuku, kisha atawafisha na kisha atawafufua. Je katika mnaowashirikisha yuko awezaye kufanya lolote katika hayo? Ametakasika na ametukuka na hayo wanayomshirikisha nayo.