Aya 1 – 11: Huu Ni Uumbaji Wa Mwenyezi Mungu
Maana
Alif Laam Miam.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1).
‘Hizo’ ni Aya za Kitabu chenye hekima.
Hizo ni ishara ya Aya za Sura hii, na kwamba hizo zinatokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amekisifu kuwa kina hekima kwa sababu ndani yake mna hekima ya hali ya juu.
Ni uongofu na rehema kwa wafanyao wema ambao wanaitafuta haki na kuitumia kwa sababu ni haki; wala hawana shaka kwamba Qur’an ni uongofu na rehema kwa kila mwenye kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na haki. Ama wale ambao tamaa zimepofusha nyoyo zao, basi hao ni ugonjwa usiokuwa na dawa isipokuwa kun’golewa.
Ambao wanasimamisha Swala; yaani wanadumu nayo na wanatoa Zaka kwa anayestahiki na wana yakini na akhera, wala hawana shaka kwamba wao wataulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu kuhusu kauli zao na vitendo vyao.
Hao ndio walio na uwongofu utokao kwa Mola wao na hao ndio wenye kufanikiwa.
Kipimo cha uongofu na kufanikiwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kuifanyia ikhlasi haki kwa kauli na vitendo na kutomwabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu wala usifanyie ubakhili fadhila alizokupa Mwenyezi Mungu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 mwanzo wa sura ya pili.
Kuifanyia Biashara Dini Na Dhamiri
Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipokujua na wanaichukulia ni mzaha.
Mwenye Majmaul-bayan anasema: “Wafasiri wengi wamesema kuwa makusdio ya maneno ya upuuzi ni nyimbo. Na kutoka kwa Imam Ja’far Sadiq (a.s.) imepokewa kuwa ni kuitusi haki na kuifanyia mzaha.”
Tafsiri hii ya Imam ndiyo iliyo karibu zaidi na hali halisi ya mamabo na inaenda na mfumo wa maneno. Kwani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kutaja waumini waliofaulu, sasa anawataja wakosefu ambao wananunua shutuma kutoka kwa wale wanoifanyia biashara dini na dhamiri, ili wawapoteze watu na haki na kuwavungavunga na mambo ya batili.
Mfano ulio wazi wa hayo ni vile, siku hizi, nguvu ya shari inavyokimbilia kueneza propaganda zake kwa kutoa mamilioni ya pesa kwenye vyombo vya habari ili yaeneze uwongo na uzushi na kuwapa mapesa wahaini na vibaraka ili wawatie shaka wenye wema wenye ikhlasi.
Zaidi ya hayo vyombo hivyo vya kishari vimewavisha vibaraka wake nguo ya dini ili wapandikize bid’a na waifasiri vile watakavyo; kuweza kueneza fitna na mipasuko baina ya mataifa na watu wa dini.
Baada ya vita vya mashariki ya kati vya mwaka 1967, tumeshuhudia aina kwa aina ya propaganda za uwongo na vita vya maneno katika magazeti ya kulipwa. Ama harakati za vibaraka zimefikia kiwango cha kumfanyia ujeuri Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Lakini kila siku zinavyopita zinafichuka njama zao na kufedheheka vibaraka. Wakati wa kuwang’oa utafika tu.
Hao watapata adhabu ya kufedhehesha kwa asababu wameiuza dini yao kwa shetani na wakala njama naye dhidi ya haki na watu wake.
Na anaposomewa Aya zetu huzipa mgongo wa kujivuna, kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni kwake mna uziwi. Basi mbashirie adhabu chungu.
Mumin mwenye ikhlasi anaisikliliza haki na anaizibia masikio batili, lakini habithi mkosefu mwenye malengo ya tamaa anaisikiliza batili na kuiiz- ibia masiko haki. Hana malipo huyu isipokuwa adhabu chungu.
Razi amesema: “Mwenye akili anaitafuta hekima kwa thamani yoyote, lakini wao hawakuitafuta na ilipowajia bure hawakuisikiza.”
Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema watakuwa na bustani zenye neema.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipobainisha malipo ya mwenye kuzipinga Aya zake kuwa ni adhabu chungu, sasa anabainisha malipo ya mwenye kuamini kuwa ni Pepo yenye neema.
Watadumu humo na watapata kila wanachokitamani. Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli kwa sababu itatokea tu.
Na Yeye ndiye mwenye uwezo mwenye hekima.
Ni mwenye nguvu kwa uweza wake, usioshindwa, ni mwenye hekima kwa mipangilio yake ambayo haipingi ila jahili au mwenye kiburi.
Ameumba mbingu bila ya nguzo mnazoziona na ameweka katika ardhi milima ili ardhi isiwayumbishe na amewatawanya humo kila namna ya wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:2).
Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasiokuwa Yeye!
Kila kilichomo mbinguni ni ushahidi wa kuweko Mwenyezi Mungu na uweza na umoja wake. Basi mna dalili gani nyinyi washirikiana kuwa mnaowaabudu ni washirika wa Mwenyezi Mungu kwenye sifa moja tu katika sifa zake.
Lakini madhalimu wamo katika upotevu ulio dhahiri.
Kila anayeipinga haki yoyote, baada ya kumdhihirikia dalili yake, basi huyo ni dhalimu mwenye dhambi.
Unaweza kuuliza: Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an tukufu ataona kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) mara nyingi anapobatilisha ushirikina huwa anasisitiza kwa kueleza vitu vilivyo dhahiri na vinavyoonekana; mfano kauli yake hii: ‘Basi nionyesheni wameumba nini hao wasiokuwa Yeye!’ au ‘Hawawezi kuumba hata nzi,’ Je, kuna siri gani katika hilo?
Siri ya hilo ni kufichua kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwa kikundi kiovu hakiamini hakika yoyote hata kama iko wazi kama mwangaza wa jua, isipokuwa masilahi yake tu. Sifa hii ni mbaya zaidi ya nyingine na ni hatari zaidi; haina dawa isipokuwa nguvu kuu ya upinzani.
وَلَقَدْ آتَيْنَا لُقْمَانَ الْحِكْمَةَ أَنِ اشْكُرْ لِلَّهِ ۚ وَمَنْ يَشْكُرْ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ كَفَرَ فَإِنَّ اللَّهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ {12}
وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ {13}
وَوَصَّيْنَا الْإِنْسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ {14}
وَإِنْ جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَنْ تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ۚ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُمْ بِمَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {15}
يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِنْ تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِنْ خَرْدَلٍ فَتَكُنْ فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّهُ ۚ إِنَّ اللَّهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ {16}
يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ ۖ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ {17}
وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ {18}
وَاقْصِدْ فِي مَشْيِكَ وَاغْضُضْ مِنْ صَوْتِكَ ۚ إِنَّ أَنْكَرَ الْأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ {19}