read

Aya 33 – 34: Ujuzi Wa Saa Uko Kwa Mwenyezi Mungu

Maana

Enyi watu! Mcheni Mola wenu na iogopeni siku ambayo mzazi hatamfaa mwanawe wala mwana hatamfaa mzaziwe kwa lolote. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Basi yasiwadanganye maisha ya dunia wala asiwadanganye na Mwenyezi Mungu mdanganyifu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameamrisha takua kwa sababu ni njia ya kuokoka na siku ambayo mtu atawakimbia wanawe na mama yake na baba yake. Siku hii itakuja bila ya shaka yoyote. Mwenye kuhadaika ni yule anayeghurika na mambo ya batili na uwongo.

Kwa Nini Mungu Akamuumba Mtu?

Nilisoma mwandishi mmoja akisema: “Miongoni mwa maswali ambayo hayana majibu ni swali hili: Kwa nini Mungu amemuumba mtu?”

Bila shaka kila mmoja anatamani lau angelijua jawabu la swali hili, kwa sababu linafungamana na kuweko mtu na hakika yake moja kwa moja. Sio siri kwamba mimi nimesoma majibu mengi sana ya swali hili kutoka kwa wataalamu, wanafalsafa na wengineo katika waliopita na wa sasa, lakini sikukinai kabisa; igawaje mimi nilipoulizwa swali hili mara nyingi nilijibu kama walivyojibu, kwa vile sina jibu jingine zaidi ya hayo waliyoyasema.

Nilipoingilia kufasiri Aya za Qur’an yenye hekima, nilisahau swali hili na sikuyahifadhi majibu ya wataalamu. Kwa sababu Tafsir Al-Kashif imeninyang’anya kila kitu; hata kumbukumbu yangu pia. Hakuna kitu isipokuwa busara inayoniongoza kwenye maana ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na malengo yake na mfungamano wake na maisha.

Nilipoendela kidogo tu na tafsiri nilipata jawabu lilio wazi wazi, katika KitabuchaMwenyeziMungu,lisilokubalishakawalataawili.Siuzushi kwamba Muumba wa kitu ndiye anayejua zaidi analolitaka kwa alichokiumba.
Basi nikapata katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu Aya zinazofahamisha kwa uwazi kuwa mtu ameumbiwa akhera sio dunia ili akaishi maisha yasiyokuwa na tabu wala matatizo yoyote.

Lakini hekima ya Muumba imetaka kuwe na mfungamano baina ya maisha mema ya akhera aliyoumbiwa mtu na kuisadiki imani kwa haki na ikhlasi na kuihami; kama ambavyo hekima yake Mtukufu imetaka kuwa asiyeamini mfungamano huu au akauamini kinadhariya bila ya kuufanyia kazi, kuwa atahisabiwa hisabu nyepesi na ataadhibiwa adhabu chungu.

Kwa sababu yeye hakujua au alijitia kutojua lengo aliloumbiwa na akaiacha njia ya sawa kwa uchaguzi wake mbaya baada ya kuongozwa na Mwenyezi Mungu na kuamrishwa kuifuata.

Kwa maneno mengine ni kuwa, ilivyo hasa maisha ya mtu yanabaki kwa kubakia muumba wake na kwamba Yeye amemuweka kwenye nyumba ya dunia kwa muda tu, mpaka wakati maalum kisha agure kwenye nyumba ya kudumu. Naye amemwamrisha kuzishughulikia nyumba zote mbili pamoja, na afanye ihtiyat ya lile linalowezekana kumtokea katika nyumba ya kwanza na lile litakalotokea katika nyumba ya pili ambalo halina shaka.

Ikiwa atafuata amri na akatii basi atakuwa amejichagulia amani na kufaulu; sawa na msafiri mwenye maandalizi kamili ya safari yake. Na atakyepinga na kuasi basi atakuwa amejichagulia mwisho mbaya; sawa na anayesafiri mji wa mbali ugenini bila ya maandalizi yoyote. Tazama Juz. 20 (28:77).

Hebu sasa tutaje baadhi ya Aya zinazofahamisha kuwa lengo la kumbwa mtu ni maisha ya pili; kama ifuatavyo:

1. Kuna zile zinazoisifia dunia kuwa ni upuuzi, mchezo, starehe zinazodanganya na mahali pa kujifaharisha na kujigamba na kwamba dunia itaondoka na kuisha; na kuisifia akhera kuwa ni nyumba ya Mwenyezi Mungu, ya kheri, ya maisha na kuridhiwa.

Vipi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amuumbe mtu na ampe siri, ugunduzi na uwezo wa kuleta maendeleo kuweza kuigeuza historia ya mtu, mbingu na ardhi kwa ajili ya mchezo na starehe zenye ghururi na maisha yanayofanana na ndoto; na hali Yeye amesema: “Hakika tumewatukuza wanaadamu.”?

Juz. 15 (17:70). Hakuna kitu kinachooafikiana na kutukuzwa watu na hekima ya Mungu isipokuwa maisha yatakayobakia kwa kubakia muumbaji wake.

2. Aya zinazofahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamjaribu na kumtahini mtu – pamoja na kuwa anamjua zaidi – ili ifichuke siri yake na hakika yake na vijitokeze vitendo vyake vitakavyomfanya astahiki thawabu au adhabu huko mwisho, akhera. Miongoni mwa Aya hizo ni: “Hakika tumevifanya vilivyo katika ardhi kuwa ni pambo lake ili tumjaribu ni nani kati yao mwenye vitendo vizuri zaidi” Juz. 15 (18:7)

وَمَا كَانَ لَهُ عَلَيْهِمْ مِنْ سُلْطَانٍ إِلَّا لِنَعْلَمَ مَنْ يُؤْمِنُ بِالْآخِرَةِ مِمَّنْ هُوَ مِنْهَا فِي شَكٍّ ۗ{21}

“Naye – Iblisi – hakuwa na mamlaka juu yao ila ni kwa sababu ya (kuwajaribu) tumjue ni nani mwenye kuamini akhera na ni nani anayetilia shaka” (34:21).

3. Lengo sio kutangaza na kuweka wazi tu bali ni “ili awalipe waliotenda ubaya kwa waliyoyatenda na waliotenda mema awalipe kwa memea” (53:31).

Kwa vile malipo haya hayathibiti duniani, basi lazima kuweko na siku nyingine; vinginevyo itakuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kukuza mambo tu. Mwenyezi Mungu ametakata na wayasemayo wajinga.

4. Aya zinazofahamisha kubakia Peponi kwa mwenye kuamini na kufanya wema na kubaki motoni mwenye kukufuru na kufanya uovu.

Unaweza kuuliza: Utaichukulia vipi kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: “Sikuumba majini na watu ila waniabudu” (51:56); ambapo inafahamisha waziwazi kuwa lengo la kuumbwa mtu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu katika maisha haya ya dunia na wala sio kupewa maisha bora akhera?

Jibu: Makusudio ya ibada hapa ni kila tendo linalomridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujikurubisha kwake. Hakuna mwenye shaka kwamba kumridhisha Mwenyezi Mungu ni njia pekee ya maisha mema ya kudumu. Kwa hiyo maana yanakuwa, sikuumba majini na watu ila wafanye matendo mema yatakayowasababishia kuishi maisha mema ya milele huko akhera. Kwa maneno mengine ni kuwa Aya hii inarudufu kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ {23}

“Na Mola wako amepitisha kuwa msimwabudu yoyote ila Yeye tu” Juz. 15 (17:23)

na pia kaulu Yake:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ {5}

“Na hawakuamrishwa ila wamwabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafia dini” (98:5).

Na natija ya usafi wa dini ni maisha ya kudumu na pepo.

Zaidi ya hayo kuna Aya kadhaa amabazo zimeifunga pepo kwa kutenda matendo mema na ya kheri duniani na kuufunga moto na kufanya shari na ufisadi duniani.

Miongoni mwa Aya hizo ni: “Na aliyekuwa kipofu katika dunia hii, basi Akhera atakuwa kipofu na aliyepotea zaidi njia.” Juz. 15 (17:72).

“Je, mwadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira?” Juz. 4 (3:142). Makusudio ya jihadi hapa ni jihadi ya kuihami haki na watu wake na kufa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu na makusudio ya subira ni uthabiti dhidi ya wabatilifu na wapetuka mipaka; na wala sio subira ya kujisalimisha kwenye nguvu ya shari na uovu na kuwa dhalili na ufukara.

Baada ya kutubainikia kuwa lengo la kuumbwa mtu ni maisha yatakayobaki na kwamba kupata neema zake ni mpaka mtu afanye heri na wema hapa duniani; na kupata moto ni mpaka mtu afanye shari na ufisadi, tutakuwa tumejua kwamba tafsiri yoyote ya kuelezea lengo la kuumbwa mtu itakayokwenda kinyume na hakika hii basi hiyo itakuwa mbali na usawa na uhalisi wa mambo.

Inatosha kuwa ni dalili ya yote hayo kauli yake Mwenyezi Mungu: “Je, mnadhani kuwa tuliwaumba bure na kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?” Juz. 18 (23:115).

Yaani lau Mwenyezi Mungu asingelimuumba mtu kwa ajili ya akhera basi ingelikuwa Mwenyezi Mungu, ambaye imetukuka hekima yake, anafanya mambo bure tu.

Ujuzi Wa Saa, Mvua Na Vilivyo Matumboni

Hakika ujuzi wa saa uko kwa Mwenyezi Mungu na huiteremsha mvua na anavijua vilivyo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho, wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, mwenye habari.

Unaweza kuuliza: Ujuzi wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hauna kikomo; kama alivyosema: “Hakifichikani kwake kilicho na uzito wa chembe katika mbingu wala aradhini” (34:3) Na akasema tena “Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye; anajua kilichomo nchi kavu na kilichomo baharini; na halianguki jani ila analijua wala punje katika giza la ardhi; wala kibichi au kikavu, ila kimo katika Kitabu kinachobainisha.” Juz. 7 (6:59).
Imam Ali (a.s.) naye anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu anajua kudondoka kwa tone na kutulia kwake, kusogea kwa chembe na kupita kwake na chakula kinachomtosha mbu.” Sasa kwanini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akahusisha kutaja vitu hivi hapa?

Imesemekana kuwa muulizaji alimuuliza Mtume (s.a.w.): kuhusu vitu hivi ndipo ikashuka Aya. Razi anasema: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipotaja saa ya Kiyama alinasibisha kutaja vitu hivi.

Sisi tumesema mara nyingi kuwa Qur’an ni Kitabu cha uongofu kinampeleka mtu kwenye jambo moja hadi jingine. Imam Ja’far Sadiq (a.s.) amesema: “Hakika Aya inakuwa mwanzo ni jambo jingine na mwisho wake ni jengine; ni maneno yanayoungana yakinyumbuka kwenye njia mabalimbali…” Kwa vyovyote iwavyo nikuwa Aya imekusanya mambo matano:

1. Hakika ujuzi wa Saa uko kwa Mwenyezi Mungu

“Hakuna wa kuidhihirisha kwa wakati wake ila yeye tu.” Juz. 9 (7:187). Hekima katika hilo ni kuwa watu wawe kwenye hadhari, wakitazamia kutokea wakati wowote.

2. Na huiteremsha mvua.

Wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio ya kuteremsha mvua ni kuwa ujuzi wa kushuka kwake unahusika na Mwenyezi Mungu tu peke yake.

Usawa ni kulichukulia neno kuteremsha kama lilivyo; kuwa ujuzi wa kuiteremsha unahusika na Mwenyezi Mungu, kwa vile sababu za kushuka kwake zinakomea kwake.

Hii haimzui mtu kujua wakati wa kushuka mvua kutokana na dalili zake. Hata kama tukichukulia kuwa makusudio ya kujua ni kujua wakati wa kushuka kwake.

Kwa sababu mtu anajua wakati wa kushuka kwake baada ya kujitoikeza dalili na alama zake. Lakini hakuna ajuae kuwa dalili na alama hizo zitatokea lini isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake.

Unaweza kuuliza: Wataalamu wanaweza kushusha mvua ya kutengenezwa, sasa itakuwaje kuwa anahusika nayo Mungu tu?

Jibu: Wataalamu wanageuza mawingu kuwa mvua na Mwenyezi Mungu ndiye aliyetengeneza mawingu kisha anayasukuma kutoka mji mmoja hadi mwingine anavyotaka. Tofauti ni kubwa baina ya kukifanya kitu na kukigeuza.

3. Na anavijua vilivyo ndani ya matumbo ya uzazi.

Unaweza kuuliza: Elimu ya kisasa inajua vilevile inajua aliyemo tumboni, kupitia vipimo kuwa ni mume au ni mke?

Jibu: Kipimo kinajua ambacho kimekwishakuwa, lakini hakijui sifa zake na utashi wa aliyemo tumboni; kama vile uzuri na ubaya, werevu na ujinga n.k. Lakini haya yote kwa Mwenyezi Mungu yanajulikana.

Imam Ali (a.s.) anasema: “Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anajua kilicho katika matumbo ya uzazi kuwa kitakuwa mume au mke, mbaya au mzuri, mkarimu au bakhili, mwema au muovu na ambaye atakuwa kuni kwenye moto wa Jahannam au atakayekuwa Peponi pamoja na mitume.”

4. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho kwa sababu kila siku ina mambo mengine.

Baada ya kupita siku nyingi imethibitika nadharia ya mwanafalsafa wa kigiriki, Heraclitus aliyesema: “Wewe huwezi kuingia mto mmoja mara mbili.” akiashiria kuwa mambo ya dhahiri ya kilimwengu na ya kijamii hubadilika mara kwa mara kutoka hali moja hadi nyingine. Kwa hiyo elimu haiwezi kujua litakalomtokea mtu baadaye.
5. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani wala wakati gani pia.

Kwa sababu mauti hayazuiliki, yanamchuka mtoto mchanga na kijana mwenye afya na kumwacha mgonjwa na kikongwe.