read

Aya 1 – 9: Ametengeneza Vizuri Umbo La Kila Kitu

Maana

Alif Laam Miim.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1).

Ni uteremsho wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake, kinachotoka kwa Mola wa walimwengu wote.

Ushahidi wa hilo tumeuleza kwenye Aya kadhaa; kama vile Juz. 1 ( 2:23 – 25), Juz. 5 (4:80 – 82) na Juz. 18 (24:55 – 57).

Au wanasema amekizua? Bali hicho ni haki itokayo kwa Mola wako, ili uwaonye watu wasiofikiwa na mwonyaji kabla yako, huenda wakaongoka.

Wapenda anasa wanaojitia kwenye upotevu, katika vigogo wa kikuraishi, walisema: “Qur’an ni utungo wa Muhammad.” Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akasema, kuwarudi, kuwa hapana bali ni wahyi wa Mwenyezi Mungu na Muhammad amewajia na yale ambayo hajawaletea yeyote kabla yake wala hatawaletea yeyote baada yake.

Amewajia na kheri ya dunia na akhera akawakataza dhulma na ufisadi mlio nao, ili mpate mawaidha na muache kabla hayajawafikia majanga. Ilitakiwa mumshukuru Muhammad kwa fadhila hii badala ya kumpangia njama za kiuadui na kumfanya ni mwongo mzushi.

Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika siku sita. Kisha akatawala kwenye arshi. Hamna walii wala mwombezi isipokuwa Yeye. Basi je hamkumbuki?

Siku sita ni kinaya cha mikupuo au mara. Makusdio ya Arshi ni utawala. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:54), Juz. 11 (10:3) na Juz. 19 (25:59). Katika Juz. 8 (54:56) tumeeleza kauli zilizosemwa kuhusu siku sita na rai yetu.

Hulipanga jambo kutoka mbinguni hadi ardhini, kisha linapanda kwake katika siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyohisabu.

Makusudio ya kupanga jambo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameumba ulimwengu, kila kiumbe akakipa sifa kwa namna inavyotaka hekima yake. Akamwajibishia kiumbe ambaye amempa uweza na utambuzi kulazimiana na njia aliyomwongoza.

Makusudio ya ‘kupanda kwake katika siku’ ni kuwa matendo ya viumbe yatakwenda kwake Siku ya Kiyama. Miaka elfu ni kinaya cha kurefuka zama.

Maana ni kuwa viumbe wote wamezungukwa na mipangilio ya Mungu na ulinzi wake. Yeye ndiye aliyewaleta na akawapangilia vizuri: “ambaye amekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza” Juz. 16 (20:50). Ni Yeye atakayekimaliza na kukirudisha, na matendo yatapelekwa kwake siku ambayo itakuwa ndefu na nzito kwa waasi na wakosefu.

Huyo ndiye Mjuzi wa mambo ya ghaibu na ya dhahiri, Mwenye uwezo Mwenye kurehemu.

Muumba wa kila kitu na msimamizi wa kila kitu. Ni Mjuzi wa ya lililokuwa na litakalokuwa, liwe dogo au kubwa, la dhahiri au la kujificha. Ni Mwenye nguvu kwa uweza wake na ufalme wake na Mwenye huruma kwa viumbe wake na waja wake.

Ambaye ametengenza vizuri umbo la kila kitu.

Kila kiumbe kilichopatikana kwa nidhamu kamili basi ni kizuri na kimepangika, kikifahamisha uwezo wa mtengenezaji na utukufu wake. Hakuna kitu chochote kilichopo ila utaona nidhamu na uwiano unaofahamisha kuweko mjuzi mwenye hekima:

مَا تَرَىٰ فِي خَلْقِ الرَّحْمَٰنِ مِنْ تَفَاوُتٍ ۖ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَىٰ مِنْ فُطُورٍ {3}

“Hutaona tofauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa rehema. Hebu rudisha jicho, je unaona kosa lolote” (67:3).

Na akaanzisha umbo la mtu kwa udongo.

Makusudio ya mtu hapa ni baba wa watu, Adam.

Kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji hafifu ambayo ni manii. Kisha akamlimganisha sawa katika umbile zuri na akampulizia roho yake.

Hiki ni kinaya cha uhai. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:2) na Juz. 18 (23:12 – 14).

Amewajaalia kusikia na kuona na nyoyo. Ni uchache mnavyoshukuru.

Neema ya ubainifu inatokana na neema ya usikizi uoni na utambuzi. Ama matamanio ya chakula ni kwa ajili ya kuishi na matamanio ya jinsia ni kwa ajli ya kubakia. Hakuna matamanio yoyote kwa mtu isipokuwa yana faida na hekima.

وَقَالُوا أَإِذَا ضَلَلْنَا فِي الْأَرْضِ أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ ۚ بَلْ هُمْ بِلِقَاءِ رَبِّهِمْ كَافِرُونَ {10}

Na husema: Ati tutakapopotea ardhini, kweli tutakuwa kwenye umbo jipya? Bali wao wanakanusha kukutana na Mola wao.

قُلْ يَتَوَفَّاكُمْ مَلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ {11}

Sema, atawafisha malaika wa mauti aliyewakilishwa kwenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu.

وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الْمُجْرِمُونَ نَاكِسُو رُءُوسِهِمْ عِنْدَ رَبِّهِمْ رَبَّنَا أَبْصَرْنَا وَسَمِعْنَا فَارْجِعْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا إِنَّا مُوقِنُونَ {12}

Na ungeliwaona wakosefu wanavyoinamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao. Mola wetu! Tumeona na tumesikia, turejeshe tutatenda mema, kwani hakika sisi tuna yakini.

وَلَوْ شِئْنَا لَآتَيْنَا كُلَّ نَفْسٍ هُدَاهَا وَلَٰكِنْ حَقَّ الْقَوْلُ مِنِّي لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ {13}

Na lau tungelitaka tungeipa kila nafsi muongozo wake. Lakini imehakikika kauli kutoka kwangu: Kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa wote majini na watu.

فَذُوقُوا بِمَا نَسِيتُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَٰذَا إِنَّا نَسِينَاكُمْ ۖ وَذُوقُوا عَذَابَ الْخُلْدِ بِمَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {14}

Basi onjeni kwa sababu ya kusahau mkutano wa siku yenu hii, hakika sisi tumewasahau. Na onjeni adhabu yenye kudumu kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.