read

Aya 15 – 22: Muumin Anaweza Kuwa Sawa Na Fasiki?

Hakika wanaoziamni Aya zetu ni wale tu ambao wanapokumbushwa hizo huanguka kusujudu na humsabihi kwa kumsifu Mola wao.

Makusudio ya waumini hapa ni wale wanaoijua haki na kuitumia na kujitolea muhanga kwa ajaili yake; wanamwabudu Mwenyezi Mungu usiku na mchana kwa kumtegemea Yeye na kumfanyia ikhlasi peke yake, asiyekuwa na mshirika. Ama tasbihi, rukui na sujudi kwa msukumo wa chumo na kibiashara kwa dini, yote hayo ni unafiki sio ibada na ni uzandiki sio imani.

Nao hawatakabari; yaani waumini wanaikaribisha haki na kuacha masilahi yao binafsi kwa ajili ya haki; kwa sabu hiyo ndiyo dini yao na masilahi yao.

Ni wajibu kusujudi kwa mwenye kuisoma Aya hii au kuisikiliza na imesemekana hata mwenye kuisikia pia bila ya kukusudia.

Mbavu zao zinaachana na vitanda kumwomba Mola wao kwa hofu na tumaini.

Vitanda ni kinaya cha usingizi. Tukiunganisha Aya hii na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu.” Juz. 18 (24:37), maana yatakuwa: Hakika waumini haiwashughulishi biashara wala usingizi kuacha ibada ya Mwenyezi Mungu, jambo ambalo linaelezea kuhofia kwao adhabu yake na kutumai kwao thawabu zake.

Ibada hiyo ndiyo aliyoikusudia Mwenyezi Mungu aliposema: “Na usi- mamishe Swala, hakika Swala inakataza machafu na maovu.” Kuna Hadith isemayo: Kisimamo cha mja kinamkurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kinamkataza dhambi, kinafuta maovu na kufukuza ugonjwa mwilini.” Ama Swala ya kibiashara huwa inaamrisha uovu na ubaya. Kwa sababu ubaya unaelekeza kwenye mfano wake na vile vile wema.

Na hutoa katika yale tuliyowaruzuku.

Wamemwabudu Mwenyezi Mungu kwa nyoyo, miili na mali.

Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika yanayofurahisha maisha. Ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda.

Makusudio ya nafsi ni nafsi yoyote, iliyokuwa na itakayokuwa katika ardhi au mbingu. Maana ni kuwa hakuna yeyote anayejua uhakika wa thawabu za kufurahisha ambazo Mwenyezi Mungu amewaandalia waumini, wenye kufanya matendo. Mtume anasema katika Hadith: “Mwenyezi Mungu anasema: “Nimewaandalia waja wangu wema ambayo hakuna jicho liliyaona wala sikio lililoyoyasikia, wala moyo uliyoyawazia.”

Je, aliye mumin ni sawa na aliye fasiki? Hawawi sawa.

Tafsri nyingi; ikiwemo Jamiu ya Tabariy, Bahrul-muhit ya Andalusi,Ruhul-bayan ya Haqi, zimesema kuwa Aya hii ilishuka Madina kuhusiana na Ali bin Abi Twalib na Walid bin U’qba bin Abi Mu’it. Tutanukuu yale ya Tabariy: “Kulipita maneno baina ya Walid na Ali. Walid akasema: “Mimi nina ulimi mpana kuliko wewe, nina meno makali kuliko wewe na ninafaa zaidi kwenye jeshi kuliko wewe.” Ali akamwambia, nyamaza wewe ni fasiki, ndipo ikashuka: ‘Je, aliye mumin ni sawa na aliye fasiki? Hawawi sawa.’

Hapana wallah hawawi sawa duniani wala kwenye mauti na akhera pia.

Ama wale ambao wameamini na wakatenda mema watakuwa na bustani za makao. Ndipo pa kufikia kwa waliyokuwa wakiyatenda.

Hii ni kutofautisha baina ya mumin mwenye takua na kafiri muovu; ni sawa na kutofautisha wema na uovu, heri na shari na Pepo iliyoandaliwa wenye takua na moto ulioandaliwa wakosefu.
Na ama wale ambao wamefanya ufuska, basi makazi yao ni motoni; kila wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni adhabu ya moto ambayo mlikuwa mkiikadhibisha.

Waumini watapata Pepo zenye neema na mafasiki watapata moto unaowaka. Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:22).

Na kwa hakika tutawaonjesha adhabu hafifu kabla ya adhabu kubwa, labda watarejea.

Makusudio ya adhabu hafifu ni adhabu ya duniani; kama vile kahati, balaa n.k. Anawaonya kwayo na kwa nguvu za hoja, wale walioghafilika na wanaojishughulisha na mambo ya batili na kuiacha haki, ili waonyeke na wapate mawaidha.

Vinginevyo watafikiwa na adhabu kubwa: “Moto wa Jahanam hali ya kudumu humo. Ni tosha yao. Na Mwenyezi Mungu amewalaani. Na wana wao adhabu ya kudumu.” Juz. 10 (9:68).

Kwa hakika ilivyo ni kuwa viongozi na watawala ndio chimbuko la kwanza la ufisadi na uovu. Kuna Hadith zinayosema: “Watawala wakiwa waongo huzuiliwa mvua, na mtawala akiwa jeuri dola inakuwa dhalili.”

Ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayekumbushwa kwa ishara za Mola wake kisha akazikataa. Hakika sisi ni wenye kuwachukulia kisasi wakosefu.

Mwenye kupata mawaidha kisha asiwaidhike nayo basi huyo ni katika wakosefu wakubwa. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewaonya kwa ulimi wa mitume wake na kwa madhara na shida, lakini nyoyo zao zikasusuwaa na wakaendelea na dhulma na ufisadi. Ndio Mwenyezi Mungu akawalipiza kisasi na Yeye ni mwenye nguvu Mwenye kulipiza kisasi.

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَلَا تَكُنْ فِي مِرْيَةٍ مِنْ لِقَائِهِ ۖ وَجَعَلْنَاهُ هُدًى لِبَنِي إِسْرَائِيلَ {23}

Hakika tulimpa Musa Kitabu basi usiwe na shaka ya kukipokea kwake, na tukakifanya ni mwongozo kwa wana wa Israil.

وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ {24}

Na tukawafanya miongoni mwao maimamu wanaoongoza kwa amri yetu waliposubiri, na wakawa na yakini na ishara zetu.

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ يَفْصِلُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ {25}

Hakika Mola wako ndiye atakayefafanua baina yao Siku ya Kiyama katika lile walilohitalifiana.

أَوَلَمْ يَهْدِ لَهُمْ كَمْ أَهْلَكْنَا مِنْ قَبْلِهِمْ مِنَ الْقُرُونِ يَمْشُونَ فِي مَسَاكِنِهِمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ ۖ أَفَلَا يَسْمَعُونَ {26}

Je, haikuwabainikia, ni vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao nao wanatembea katika maskani zao. Hakika katika hayo kuna ishara, basi je, hawasikii.

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا نَسُوقُ الْمَاءَ إِلَى الْأَرْضِ الْجُرُزِ فَنُخْرِجُ بِهِ زَرْعًا تَأْكُلُ مِنْهُ أَنْعَامُهُمْ وَأَنْفُسُهُمْ ۖ أَفَلَا يُبْصِرُونَ {27}

Je, hawaoni kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kame, kisha kwayo tunaitoa mimea wanayokula wanyama wao. Je, hawapati busara.

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَٰذَا الْفَتْحُ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {28}

Na wanasema: Ushindi huu utatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?

قُلْ يَوْمَ الْفَتْحِ لَا يَنْفَعُ الَّذِينَ كَفَرُوا إِيمَانُهُمْ وَلَا هُمْ يُنْظَرُونَ {29}

Sema: Siku ya ushindi wale ambao wamekufuru haitafaa imani yao, wala hawatapewa muda.

فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَانْتَظِرْ إِنَّهُمْ مُنْتَظِرُونَ {30}

Basi achana nao na ungoje; hakika wao wanangoja.