read

Aya 23 – 30: Usiwe Na Shaka Ya Kuipokea Kwake

Maana

Hakika tulimpa Musa Kitabu basi usiwe na shaka ya kukipokea kwake, na tukakifanya ni mwongozo kwa wana wa Israil.

Wafasiri wengi wamesema kuwa ‘Kwake’ inarudi kwa Musa; kwa maana ya kuwa Muhammad atakutana na Musa usiku wa Miraji. Ilivyo hasa ni kuwa dhamiri hiyo inarudia kwenye Qur’an; kwa maana ya kuwa, ewe Muhammad! Tumekutermshia Qur’an kama tulivyomteremshia Musa Tawrat. Wala haitakikani kutia shaka katika hilo wewe wala mwingine.

Kuhusu kukatazwa Mtume kutia shaka tumekuelezea mara nyingi. Tazama Juz. 3 (3:59-63).

Na tukawafanya miongoni mwao maimamu wanaoongoza kwa amri yetu waliposubiri, na wakawa na yakini na ishara zetu.

Makusudio ya maimamu hapa ni mitume wa Kiisrail; kama vile Musa, na Isa ambaye nasaba ya upande wa mama yake inafikia kwa Daud. Kila Mtume wa kiisraili alipata aina kwa aina ya adhabu na mateso; bali waisrail waliwaua manabii wao kadhaa:

وَيَقْتُلُونَ النَّبِيِّينَ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۗ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوْا وَكَانُوا يَعْتَدُونَ {61}

“Na wakiwaua Manabii pasipo haki. Basi haya ni kwa sababu ya kuasi kwao na kupituka mipaka.” Juz. 1 (2:61).

Pamoja na yote hayo, waliweza kuvumilia wakawa na subira na wakaendelea kutekeleza risala yao. Kwa hiyo nawe Muhammad vumilia maudhui ya watu wako na uendelee na risala yako.

Hakika Mola wako ndiye atakayefafanua baina yao Siku ya Kiyama katika lile walilohitalifiana.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:113), Juz. 11(10:93) na Juz. 14 (16:124).

Je, haikuwabainikia, ni vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao nao wanatembea katika maskani zao. Hakika katika hayo kuna Ishara, basi je, hawasikii.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20).

Je, hawaoni kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kame, kisha kwayo tunaitoa mimea wanayokula wanyama wao.

Je, hawapati busara kwa jinsi Mwenyezi Mungu alivyoipa uhai ardhi baada ya kufa kwake na akaotesha humo kila aina za mimea wanayokula watu na wanyama? Kama hivyo atawafufua wafu baada ya kuwa ni mchanga na mifupa

Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; kama Juz. 17: (22:5).

Na wanasema: ushindi huu utatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
Aya hii ni mfano wa ile isemayo: “Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?” Juz. 17 (21:38). Kwa sababu makusudio ya ushindi hapa ni siku itakayohukumiwa kwa haki. Hilo linatiliwa nguvu na kauli inayofuatia:

Sema: Siku ya ushindi wale ambao wamekufuru, na wakaifanyia inadi haki katika maisha ya dunia, haitafaa imani yao huko akhera wakati watakapoiona adhabu. Kwa sababu imani hiyo itakuwa ni kuukimbia moto sio imani ya kweli na yakini.

Wala hawatapewa muda.

Mwenyezi Mungu hawezi kuwapa muda siku ya Kiyama, kwa sababu ali- wapa muda mrefu duniani, lakini hawakuitumia fursa hiyo.

Basi achana nao na ungoje; hakika wao wanangoja.

Wao wanangoja ufikwe na majanga, basi achana nao na ungoje kidogo tu, utaona hukumu ya Mwenyezi Mungu kwako na kwao. Yeye atakunusuru na atawafedhehsha wao:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ {33}

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wamechukia.” Juz. 10 (9:33).