read

Aya 1-3: Ewe Nabii, Mche Mwenyezi Mungu

Maana

Ewe Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwatii makafiri na wanafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hekima. Na fuata uliyoletewa wahyi kutoka kwa Mola wako. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda. Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa.

Katika Aya hizi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemwamrisha Nabii wake mtukufu, kuwa na takua, kumtegemea Yeye, kuutumia wahyi wake na kutowatii makafiri na wanafiki.
Wafasiri wamejiuliza kuwa Nabii ni maasumu, sasa kuna haja gani ya amri zote hizi na kukatazwa uasi?

Kuna waliojibu kuwa hii ni kusisitiza utiifu na unyenyekevu alio nao Nabii (s.a.w.). Wengine wakasema kuwa Abu Sufyan alimtaka Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kutoyatukana masanamu wanayoyaubudu makauraishi. Abu Sufyani wakati huo alikuwa pamoja na kundi la makafiri na wanafiki.

Sisi huko nyuma tumesema mara kwa mara kuwa aliye juu ana uwezo wa kumwamrisha aliye chini na kumkataza maasi hata kama ni maasumu. Hivi sasa tunayaunganisha hayo na haya yafutayo:

Hakuna kitu kizito kwa yule asiyemuogopa Mwenyezi Mungu kuliko tamko la ‘mche Mungu;’ wala hakuna adui mkubwa kuliko atakayelisema tamko hilo kwake. Imenukuliwa kutoka kutoka kwa Abdul-Malik bin Marwani kwamba yeye alipotawala alisema katika hotuba: “Kuanzia leo, atakayeniambia: mche Mungu, nitamkata shingo yake.”

Ama yule mwenye kuhofia kukutana na Mola wake na akaikanya nafsi na matamanio, basi kwake yeye hilo ni tamko la mapenzi na huruma na hutamani lau angelisikia mara kwa mara; hata kama ni maasumu wa makosa na madhambi; bali huko kulipenda na kulisikilza kumetokana na umaasumu na utiifu wake. Mtu adhimu huwa anajituhumu kwa upunguvu kadiri atakavyoweza kujitahidi.

Kwa hiyo basi hakuna haja ya kuleta taawili na tafsiri nyingine. Kuongezea kuwa amri ya takuwa kwa bwana wa watu na majini ni hekima na somo kubwa kwa wenye vyeo na watawala, kwamba kwa vyovyote watakavyokuwa wakubwa, lakini hawako zaidi ya kuamrishwa uadilifu na takua.

Kwenye Nahjul balagha imeelezwa: “Ambaye itakuwa uzito kwake kuambiwa neno la haki au kuelezwa uadilifu basi itakuwa kuyafanya mawili hayo ni uzito zaidi.”

مَا جَعَلَ اللَّهُ لِرَجُلٍ مِنْ قَلْبَيْنِ فِي جَوْفِهِ ۚ وَمَا جَعَلَ أَزْوَاجَكُمُ اللَّائِي تُظَاهِرُونَ مِنْهُنَّ أُمَّهَاتِكُمْ ۚ وَمَا جَعَلَ أَدْعِيَاءَكُمْ أَبْنَاءَكُمْ ۚ ذَٰلِكُمْ قَوْلُكُمْ بِأَفْوَاهِكُمْ ۖ وَاللَّهُ يَقُولُ الْحَقَّ وَهُوَ يَهْدِي السَّبِيلَ {4}

Mwenyezi Mungu hakumwekea mwanamume nyoyo mbili ndani yake. Wala hakuwafanya wake zenu – mnaowalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu – kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu. Hiyo ni kauli yenu kwa vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu anasema haki, naye huongoza njia.

ادْعُوهُمْ لِآبَائِهِمْ هُوَ أَقْسَطُ عِنْدَ اللَّهِ ۚ فَإِنْ لَمْ تَعْلَمُوا آبَاءَهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ وَمَوَالِيكُمْ ۚ وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُمْ بِهِ وَلَٰكِنْ مَا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ ۚ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِيمًا {5}

Waiteni kwa baba zao. Hilo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Kama hamuwajui mababa zao basi ni ndugu zenu katika dini na rafiki zenu. Si vibaya kwenu kwa mlivyokosea, lakini kwa yale ziliyoyakusudia nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.