Aya 4 – 5: Mwenyezi Mungu Hakumweka Mtu Mmoja Nyoyo Mbili
Maana
Mwenyezi Mungu hakumwekea mwanamume nyoyo mbili ndani yake.
Hata mwanamke pia ni kama mwanamume. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemuhusu mwanmume hapa kwa sababu amemwamrisha Mtume (s.a.w.) wake mtukufu kuwa na takua, kwa hiyo ikanasibiana kufuatishia amri hii kuwa mwanamume hawezi kuwa na moyo mmoja wa kumcha Mwenyezi Mungu na mwingine wa kucha watu.
Lengo ni Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anabainisha kuwa mtu hawezi kuamini mambo mawili yanayopingana kwa wakati mmoja; kwa mfano aamini dini inayokataza dhulma na uchokozi, Uislamu na Ukiristo, na wakati huo huo ahalalishe dhulma na uchokozi.
Ila ikiwa ana nyoyo mbili na nyuso mbili; kama waamerika ambao wameleta kununi mpya, kwamba mmarekani anaweza kuwa ni mwisrail na kupigana na mwarabu kwa jina la Israil na wakati huo bado ni raia wa Marekani.
Au itabidi tuseme kuwa Israil ni kambi ya jeshi la uchokozi la marekani na kwamba urai wa Israil ni jina tu; hata watawala pia; kwa vile ni kikosi tu cha kulinda masilahi ya ukoloni na unyonyaji.
Mtu mmoja alimwambia Imam Ali (a.s.): “Mimi nakupenda wewe na ninampenda Muawiya.” Imam akamwambia: “Wewe ni chongo, sasa chagua ama uwe kipofu au upone chongo.”
Unaweza kuuliza: Utasemaje kuhusiana na anayesema; mimi ni mwislamu au mkristo kiitikadi, lakini kisiasa ninafuata siasa za mashariki au magharibi. Je inawezekana kuchanganya mawili haya?
Jibu: Mtu yoyote anayeamini haki kwa ukweli na usafi wa nia, inafaa, bali ni wajibu kumuunga mkono kila kwenye msimamo wa kuinusuru haki na uadilifu; awe ni wa mashariki au magharibi. Wala haijuzu kumuunga mkono tu, hivi hivi, bila ya msingi wowote. Kwa maana hiyo basi haiwezekeni kuchanganya baina ya itikadi ya kiislamu na kuunga mkono tu hivi hivi kwa hali yoyote.
Hii ni katika yanayohusiana na Uislamu. Ama yanayohusiana na itikadi ya kikiristo tunawaachia makasisi walio huru waliotangaza hasira zao kwa baba mtakatifu aliyekataa kukutana nao, lakini wakati huo huo akakutana na viongozi wa kimarekani.
Wakasema katika mateta yao: “Mkutano huu wa Baba mtakatifu na viongozi hawa unaonyesha wazi uhusiano wa nguvu ulioko baina ya kanisa kama tasisi ya dini na siasa za kiuchumi zinazosimamia ukandamizaji na dhulma dhidi ya watu wengi.” Makasisi hawa walitangaza kuwa wangejaribu kuuangamiza uhusiano huu.1
Wala hakuwafanya wake zenu – mnaowalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu – kuwa ni mama zenu.
Wakati wa ujahiliya mtu alikuwa akimwacha mkewe kwa kumwambia: Wewe kwangu ni kama mgongo wa mama yangu (Dhihar). Uislamu ukalikataza hilo, kwa sabau mke hawezi kuwa mama kwa kauli hii, na ukawajibisha kafara kwa atakayesema kauli hiyo, yakipatikana masharti yake, ambayo yatabainishwa mwanzoni mwa Juzuu ya 28. (inshaallah).
Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu.
Wakati wa ujahiliya mtu alikuwa akimchukua mtoto wa mwingine kumfanya mwanawe hasa na kumwingiza kwenye ukoo wake, anakuwa na hukumu ya mtoto wake halisi katika kila kitu na watu wakimwita kwa jina la baba aliyemchukua badala ya baba yake. Ndipo Uislamu ukakataza mtindo huu.2
Hiyo ni kauli yenu kwa vinwywa vyenu tu.
Na kauli haibadilishi uhalisi wa mambo.
Na Mwenyezi Mungu anasema haki naye huongoza njia.
Kauli ya haki na njia ya sawa ni kuwa mtoto wa kupanga sio mtoto wa kiuhakika; wala mke hawi ni mama kwa dhihari.
Waiteni kwa baba zao waliowazaa sio waliowapanga. Hilo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. yaani hilo la kuwaita kwa ubini wa baba zao.
Kama hamuwajui mababa zao basi ni ndugu zenu katika dini na rafiki zenu.
Neno rafiki limefasiriwa kutokana na neno mawla, pia lina maana ya huria; mtumwa aliyeachwa huru. Mtu alikuwa anaweza kuitwa huria wa fulani.
Wafsiri na watu wa sera wanasema kuwa Zayd Bin Haritha alitekwa nyara akiwa mdogo. Hakim bin Huzam akamnunua kwa ajili ya kumpatia shangazi yake Khadija Bint Khuwalid. Mtume (s.a.w.) alipomuoa akapewa zawadi na mkewe. Baada ya kushuka wahyi kwa Nabii, akamlingania kwenye Uisalamu na akasilimu. Akamfanya ndugu na ami yake Hamza bin Abu Twalib.
Haritha, Baba yake Zayd, akaja siku moja kwa Mtume (s.a.w.) na kumwambia, ama uniuzie mwanangu, au mwache huru. Mtume akamwacha huru na kumwambia nenda upendako. Basi akakataa kuachana na Mtume. Ndipo watu wakawa wanamwita Zayd bin Muhammad mpaka iliposhuka Qur’an kubatilisha hilo.
Si vibaya kwenu kwa mlivyokosea, lakini kwa yale ziliyoyakusudia nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Anayemwita mtu asiyekuwa baba yake kwa kufikiria kuwa ni baba yake, hana lawama; isipokuwa mwenye dhambi ni yule aliyejua na akakusudia: Mtume (s.a.w.) anasema: “Umma wangu umeondolewa kukosea na kusahau na yale waliyolazimishwa na wasiyoyajua na wasiyoyaweza na wanayokuwa na dharura nayo,” kwa sharti la kutotokea hayo kwa uzembe na kupuuza.
النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنْفُسِهِمْ ۖ وَأَزْوَاجُهُ أُمَّهَاتُهُمْ ۗ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّهِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ إِلَّا أَنْ تَفْعَلُوا إِلَىٰ أَوْلِيَائِكُمْ مَعْرُوفًا ۚ كَانَ ذَٰلِكَ فِي الْكِتَابِ مَسْطُورًا {6}
وَإِذْ أَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنْكَ وَمِنْ نُوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۖ وَأَخَذْنَا مِنْهُمْ مِيثَاقًا غَلِيظًا {7}
لِيَسْأَلَ الصَّادِقِينَ عَنْ صِدْقِهِمْ ۚ وَأَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا أَلِيمًا {8}