read

Aya 6 – 8: Nabii Ni Aula Kwa Waumini Kuliko Nafsi Zao

Maana

Je, Nabii Ni Hakimu Kwa Amri Yake? Nabii Ni Aula Kwa Waumini Kuliko Nafsi Zao.

Neno aula tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu linalotamkwa hivyo hivyo awla lililonyumbuliwa kutokana na neno wilaya na walii, ambalo maana yake yanatofautiana kulingana na yule anayezungumziwa. Akizungumziwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) basi maana yake ni utawala na nguvu zisizoshindwa na yeyote. Akizungumziwa Nabii (s.a.w.) inakuwa maana ni utiifu usiopingwa. Haya ndiyo maana yaliyokusudiwa hapa.
Sasa unaweza kuuliza: Si itakuwa maana yake ni kuwa Nabii ni hakimu na mtoa amri tu, mwengine hana uhuru. Tutalinganisha vipi hili na lile la msingi wa uhuru ambao ni haki ya kiasili ya kila mtu?

Jibu: Tutalinganisha uhuru wa mtu na utiifu wa Mwenyezi Mungu. Nabii (s.a.w.) anamsemea na kumbainishia Mwenyezi Mungu:

وَمَا يَنْطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ {3}

إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ {4}

“Hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni wahyi uliofunuliwa” 53 (3 4).

Kuna Hadith sahihi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: “Haamini mmoja wenu mpaka matamanio yake yafuate yale niliyokuja nayo.” Kwa hiyo kufuata na kutii ni aliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu sio kutoka kwake.

Zaidi ya hayo uhuru ni kushikamana na njia ya usawa, kutumia haki na kubeba majukumu kwa utashi wake, huku akiipigania haki kwa nguvu zake zote. Lakini mwenye kuwa na msukumo wa mapendeleo bila ya kujali hisabu wala mchungaji, huyo ni mtumwa wa matamanio. Mwana falsafa mmoja mashuhuri alisema: “Uhuru sio kujifadhilisha kiundani kunakoruhusu tujifadhilishe sisi kuliko majukumu; isipokuwa ni uwezo wa kujenga mustakabali.”

Na wake zao ni mama zao.

Wake za mitume wana heshima na uharamu wa kuolewa baada yake sawa na mama, lakini kwenye mambo mengine ni watu kando kama wengine.

Na ndugu wa tumbo ni aula wenyewe kwa wenyewe, katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kuliko waumini wengine na wahajiri.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 10 (9:75).

Ila muwe mnafanya wema kwa marafiki zenu

Makusudio ya wema hapa ni wasia, na marafiki wanakuwa ni pamoja na walioachwa huru au ndugu wasiorithi. Maana ni kuwa mirathi ni ya ndugu wa karibu wa maiti, lakini wasia ni wa aliyeusiwa awe wa mbali au wa karibu.

Hayo yamekwishaandikwa kitabuni.

Yaani hukumu imekwishathibiti Kitabuni mbele ya Mwenyezi Mungu na mwenye kuiasi atakuwa miongoni mwa walioangamia.

Na tulipochukua kwa manabii agano lao na kwako wewe na Nuh na Ibrahim na Isa mwana wa Maryam, na tulichukua kwao ahadi ngumu.

‘Kwako wewe,’ anaambiwa Muhammad (s.a.w.). Makusudio ya agano ni kufikisha (Tabligh) risala ya Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu wake na kuwa na subira na yatakayowapata katika njia yake. Amehusisha kutaja Nuh, Ibrahim, Musa, Isa na Muhammad, baada ya kuwataja manabii kwa ujumla kwa vile wao ni bora ya manabii wote, na ametangulizwa Muhammad kwa vile yeye ni mbora wao hao watano.

Katika Juz. 26 (46:35) wameashiriwa mitume Ulul-azmi (wenye ustahamilivu). Sababu ya kuitwa hivyo, kama zilivyopokewa baadhi ya riwaya, ni kuwa kila Nabii baada ya Nuh alikwa akifuata sharia ya Nuh, kisha sharia yake ikafutwa na sharia ya Ibrahim nayo ikafutwa na sharia ya Musa, nayo ikafutwa na Isa, kisha ikafutwa na ya Muhammad (s.a.w.) ambayo haitafutwa hadi Kiyama, kwa vile hakuna Nabii mwingine baada yake.

Na tulichukua kwao agano madhubuti.

Hili ndilo agano la kwanza, na amerudia kulitaja ili alisifu kuwa ni imara na lenye nguvu. Mwenyezi Mungu ameyapa sifa ya maagano madhibuti katika sehemu tatu katika Kitabu chake kitukufu:

Kwanza, ni agano la ndoa aliposema: “Na hali wao wamechukua kwenu agano madhubuti?” Juz. 4 (4:21). Pili ni agano alilochukua na wana wa Israil aliposema: “Na tukachukua kwao agano madhubuti.” Juz. 6 (4:154). Agano la tatu ni hili la Manbii tunalolizungumzia.

Sheikh Mahmud Shaltut, alighafilika kidogo pale aliposema: “Wasifu wa agano madhubuti haukuja katika sehemu yoyote ile katika sehemu zake – yaani Qur’an - isipokuwa katika kufunga ndoa.” Kutokosea ni kwa Mungu.

Ili awaulize wakweli juu ya ukweli wao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewatuma Manabii na akachukua kwao agano la kufikisha ujumbe ili wakawaulize wakweli, walikusudia nini kwenye ukweli wao. Je, walikusudia radhi ya Mwenyezi Mungu au ni kwa ajili ya kuwaambia watu kuwa wao ni wakweli na mengineyo ya kibinafsi.

Imam Ja’far Sadiq (a.s.) anasema: “Mwenyezi Mungu akimuuliza mtu kuhusu ukweli wake ni kwa njia gani aliusema, basi atamlipa kulingana nao, je vipi hali ya muongo?”

Na amewandalia makafiri adhabu chungu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipowataja mitume sasa anawataja makafiri kwa mkabala wa kuwataja wema.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ إِذْ جَاءَتْكُمْ جُنُودٌ فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا وَجُنُودًا لَمْ تَرَوْهَا ۚ وَكَانَ اللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرًا {9}

Enyi ambao mmeamini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu; pale yalipowafikia majeshi, tukayapelekea upepo na majeshi msiyoyaona na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

إِذْ جَاءُوكُمْ مِنْ فَوْقِكُمْ وَمِنْ أَسْفَلَ مِنْكُمْ وَإِذْ زَاغَتِ الْأَبْصَارُ وَبَلَغَتِ الْقُلُوبُ الْحَنَاجِرَ وَتَظُنُّونَ بِاللَّهِ الظُّنُونَا {10}

Walipowajia kutoka juu yenu na kutoka chini yenu; na macho yakakodoka na nyoyo zikapanda kooni. na mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbali mbali.

هُنَالِكَ ابْتُلِيَ الْمُؤْمِنُونَ وَزُلْزِلُوا زِلْزَالًا شَدِيدًا {11}

Hapo waumini walijaribiwa na wakatikiswa mtikiso mkali.

وَإِذْ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ مَا وَعَدَنَا اللَّهُ وَرَسُولُهُ إِلَّا غُرُورًا {12}

Na waliposema wanafiki na wale ambao wana maradhi katika nyoyo zao, Mwenyezi Mungu na Mtume wake hakutuahidi ila udanganyifu.

وَإِذْ قَالَتْ طَائِفَةٌ مِنْهُمْ يَا أَهْلَ يَثْرِبَ لَا مُقَامَ لَكُمْ فَارْجِعُوا ۚ وَيَسْتَأْذِنُ فَرِيقٌ مِنْهُمُ النَّبِيَّ يَقُولُونَ إِنَّ بُيُوتَنَا عَوْرَةٌ وَمَا هِيَ بِعَوْرَةٍ ۖ إِنْ يُرِيدُونَ إِلَّا فِرَارًا {13}

Na kundi moja miongoni mwao liliposema: Hapana pa kukaa nyinyi leo, basi rudini. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume wakisema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa ni tupu; hawakutaka ila kukimbia tu.

وَلَوْ دُخِلَتْ عَلَيْهِمْ مِنْ أَقْطَارِهَا ثُمَّ سُئِلُوا الْفِتْنَةَ لَآتَوْهَا وَمَا تَلَبَّثُوا بِهَا إِلَّا يَسِيرًا {14}

Na lau wangeingiliwa kwa pande zake, kisha wakatakiwa fitna, wangelifanya, na wasingelisita isipokuwa kidogo tu.

وَلَقَدْ كَانُوا عَاهَدُوا اللَّهَ مِنْ قَبْلُ لَا يُوَلُّونَ الْأَدْبَارَ ۚ وَكَانَ عَهْدُ اللَّهِ مَسْئُولًا {15}

Na kwa hakika walikuwa wamemwahidi Mwenyezi Mungu kabla kwamba hawatageuza migongo. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa.