read

Aya 9 – 15: Ahzab

Muhtasari Wa Kisa Cha Ahzab

Aya hizi tulizo nazo na zinazofuatia hadi 27, zilishuka kuhusu vita vya Ahzab (makundi), ambavyo pia vinaitwa vita vya Khandaq (handaki).

Kwa ufupi ni kuwa kikundi katika viongozi wa kiyahudi waliwahimiza makuraishi na makabila mengine ya waarabu kupigana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Walitoa mali nyingi sana na wakaweza kuunda jeshi ambalo halikuwahi kutokea katika bara Arabu. Basi jeshi, likiongozwa na Abu Sufyan, likaelekea Madina.

Mtume (s.a.w.), alipojua makusudio yao, aliaamrisha lichimbwe shimo kwa ushauri kutoka kwa Salman Al-Farisi. Mtume (s.a.w.) akafanya kazi kwa mkono wake, na waislamu wengine wenye ikhlasi pia wakafanya kazi. Salmani alikuwa akiwatia hamasa kwa kuwasimulia ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa wanaofanya matendo na wapiganaji jihadi. Wanafiki walikuwa wakijaribu kuivunja azma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na wakiponyoka bila ya Mtume kujua.

Lakini handaki lilikamilika, na vikosi vya majeshi vikaanza kuja kwa maelfu. Waislamu walipowaona, wengi wakajawa na hofu na wakaona wamefikwa na balaa, wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana nyingi. Fazaa yao ilizidi pale Bani Quraydh, kabila la kiyahudi waliokuwa wakikaa na Mtume (s.a.w.) Madina wakiwa na ahadi ya kutosaidia adui, na kuendelea na ahadi yao hiyo, lakini lilipokuja jeshi la Ahzab wakavunja ahadi na kutangaza vita katika wakati mgumu sana kwa waislamu.

Hivi ndivyo walivyo Mayahudi kila wakati na kila mahali. Wanajidhalilisha kama mbwa, wakiwa hawana nafasi, lakini mara tu wanapoipata wanaanza kuuma. Mtume (s.a.w.) alimtuma Sa’d Bin Muadh na maswahaba wengine kujaribu kuwaambia Bani Quraydha wasivunje ahadi, lakini wakang’angania kuivunja. Basi Waislamu wakawa wamezungukwa na adui wa nje na wa ndani. Juu kuna adui na chini kuna adui.

Katika kitabu Fiqhu ssira cha Sheikh Ghazali, anasema: “Amru bin Wud, Ikrima bin Abu Jahl na Dhirar bin Al-Khattwab walipitapita wakaona sehemu finyu kwenye handaki, Wakawarusha farasi wao na wakajitoma. Waislamu wakahisi hatari sana. Wapanda farasi wakiongozwa na Ali bin Abu Twalib, wakenda haraka kuziba mwanya.

Ali akamwambia Amru bin Wud, Shujaa mkubwa, mwenye uzoefu: ‘Ewe Amru! Ulimwahidi Mwenyezi Mungu kuwa mwanamume yote wa kikuraishi hatakupa mwito wa mojawapo ya mambo mawili ila utauchukua.” Akasema: “Ndio.” Ali akamwambia: “Ninakupa mwito uje kwa Mwenyezi Mungu kwenye Uislamu.” Akasema: “Sina haja.” Ali akasema. “Ninakuita kwenye mapambano.” Akasema: “Kwa nini ewe mwana wa ndugu yangu. Wallah mimi sipendi kukuua-alisema hivi kwa kumdharau - Ali akamwambia wallahi mimi ninapenda kukuua.

Basi Amru akakasirika, akaruka kutoka kwenye farasi wake, na akapiga uso wake; kisha akamkabili Ali wakaanza kupambana; Ali akamuua. Wakatoka wapanda farasi wa washirikina wakiwa wameshindwa hawana lolote.”

Jeshi la washirikina lilipoona halina mahali pa kuvuka handaki wakaanza kurusha mishale yao kwa waislamu. Mshale mmoja ukampata Sa’ad Bin Mua’dh na ukamjeruhi sana kwenye mboni ya jicho. Mtume (s.a.w.) akaamuru apelekwe kwa mwanamke anayeitwa Rafida, aliyekuwa akiwatibu majeruhi wa kiislamu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Sa’ad alipoona jeraha lake linaweza kumuua, aliomba dua kwa kusema: “Ewe Mola wangu, Ikiwa bado umebakisha vita na Makuraishi basi nibakishe, kwani hakuna watu ninaopenda kuwapiga jihadi kuliko hawa waliomuudhi Mtume, wakamkadhibisha na kumfukuza. Na ikiwa vita umevimaliza baina yetu na wao basi nibakishe wala usiniue mpaka jicho langu litulie kwa Bani Quraydha.”

Basi Mwenyezi Mungu akamwitikia dua yake akamfanya ni hakimu kwa Bani Quraydha, akawauwa wanume wao na akateka wake zao. Ufafanuzi utakuja kwenye Aya 26 inshallah.

Waislamu wakaendelea kuzingirwa kwa kiasi cha siku ishirini; hakuna kitu isipokuwa kutupiana mishale na mawe. Mara ukaja upepo mkali uliopondaponda kambi ya Ahzab, ukaizua mahema yao, na kila kitu kikaharibika, wakarudi wamedhalilika wakiongozwa na Abu Sufyan.

Mwenyezi Mungu akampa nguvu Mtume wake kwa ushindi; akawa anasema: Lailaha ill- lallha, wahdahu, swadaqa wa’dahu wanaswara abdahu, wa a’zza jundahu wahazama l-a’hzaba wahadau, fala shay-unba’dah (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, amesma kweli kiaga chake na akamusuru mja wake na akawatia nguvu askari wake na akavishinda makundi akiwa peke yake, basi hakuna kitu baada yake).

Wapokezi wameafikiana kuwa vita hivi vilikuwa mwaka wa tano wa Hijra na wakatofautiana katika mwezi. Kuna waliosema ni Dhul qaada (mfunguo pili) na waliosema ni Shawwal (mfunguo mosi). Kwa ujumla hivyo ndivyo vilivyokuwa vita vya Ahzab (makundi). Ufafanuzi wake ni kama ufuatavyo katika ufafanuzi wa Aya:

Enyi ambao mmeamini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu; pale yalipowafikia majeshi, tukayapelekea upepo.

Kumbukeni enyi waumini mliokuwa pamoja na Mtume (s.a.w.) katika vita vya Khandaq, mkizungukwa na maadui kila upande. Kumbukeni hilo na mshukuru neema ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa na ikhlasi na subira, pale alipowapelekea madui zenu upepo mkali na majeshi msiyoyaona na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

Wafasiri wanasema walikuwa ni malaika. Inawezekana kuwa ni kinaya cha khofu na utishio alioutia Mwenyezi Mungu kwenye nyoyo za majeshi ya Ahzab.

Katika Bahrul-muhit ya Abu Hayan Al-Andalusi imeelezwa kuwa jeshi la wa Ahzab lilikuwa na watu 15,000 na waislamu walikuwa 3000.

Wafasiri na watu wa sera wameafikiana kwamba ulitokea mwamba ndani ya handaki wakati wa kuchimba, ukavunja vyuma na kukawa na uzito. Mtume (s.a.w.) akachukua sururu kutoka kwa Salman akaupiga mwamba ukatoa cheche, akapiga mara ya pili ukatoa cheche na mara ya tatu pia ukatoa cheche. Mtume (s.a.w.) akasema: “Kwenye cheche za kwanza nimeona Madain mji wa mfalme Kisra, mara ya pili nikaona kasri ya Kaizari na mara ya tatu nikaona kasri ya Sanaa. Na Jibril amenipa habari kuwa umma wangu utaingia kote huko, basi furahini.”

Yote aliyoyasema, Bwana wa majini na watu, yalitokea.

Walipowajia kutoka juu yenu na kutoka chini yenu.

Yaani jeshi la Ahzab liliwazingira waislamu bila kuwapa mwanya wowote. Kundi la wafasiri wamesema kuwa walikuja Ghatafan, Banu Quraydha na Banun Nadhir katika Mayahudi kutoka upande wa mashariki, wakaja Makuraishi, Banu Kinana na watu Tihama kutoka upande wa magharibi.
Na macho yakakodoka na nyoyo zikapanda kooni.

Hiki ni kinaya cha hofu kubwa na fazaa.

Na mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbali mbali.

Baadhi ya walioamini walidhani kuwa Mwenyezi Mungu hatainusuru dini yake na Mtume wake. Baadhi ya wanafiki wakasema Muhammad anatuahidi hazina za Kaizari na leo mtu hawezi hata kwenda chooni.

Hapana mwenye shaka kuwa daima kuna udhuru kwa wanafiki. Lakini mwenye kuamini kisha akajiuliza huku akikereka: Kwa nini Mwenyezi Mungu asiwadidimize madhalimu ardhini au awateremshie kimondo kutoka mbinguni, huyu hatumshangai kuwa yeye ni mwenye kusamehewa kwa Mungu, maadamu anamwamini kwenye moyo wake.

Hapo waumini walijaribiwa na wakatikiswa mtikiso mkali.

Uhakika wa nafsi ulivyo haujitokezi ila wakati wa shida na mtihani wa mambo ya kuhofisha na ya kuchukiza. Vita vya Khandaq vilikuwa ni mtihani mkubwa sana kwa waumini na wanafiki; ambapo hakika ya kila mmoja ilijitokeza waliposema wanafiki walioficha unafiki na kudhihirisha imani na wale ambao wana maradhi katika nyoyo zao. Hawa ni wale wenye imani dhaifu waliowaamini wanafiki bila ya kufikiria. Hawa na wale wakasema:

Mwenyezi Mungu na Mtume wake hakutuahidi ila udanganyifu.

Hao hawamwamini Mwenyezi Mungu wala Mtume wake. Kwa sababu mumin hawezi kusema maneno haya ya kufuru. Waliyasema haya ili kuwatia shaka wapumbavu na wenye akili dhaifu.

Na kundi moja miongoni mwao liliposema: Hapana pa kukaa nyinyi leo, basi rudini.

Mtume (s.a.w.) na maswahaba walipoanza kuchimba handaki, kundi moja la wanafiki likasema: “Handaki litafaa nini na vita hivi, halifai lolote hilo.” Walisema hivi kabla ya kufika majeshi. Yalipokuja majeshi wakasema: “Hamuliwezi jeshi hili kubwa wala hamponi isipokuwa kukimbia na kujisalimisha.”

Wakati nikifafanua Aya hizi nimekumbuka vibaraka wa wazayuni na wa wakoloni wanavyoeneza hofu na fazaa kutoka kwa waisrail. Nimekumbuka hivyo kwa kujua kuna wanaofanana nao katika zama zilizopita na kwamba vita vya maneno vilianza zamani; wala havikuanza na uzayuni na ukoloni; lakini la umuhimu ni kuwa hahadaiki nayo isipokuwa mwenye akili finyu na asiyekuwa na mtazamo wa mbali.1

Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume wakisema: Hakika nyumba zetu ni tupu.

Wanafiki walikuwa wakitafuta vijisababu vya kukimbia kambi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwa kusema kuwa wataibiwa kwa vile nyumba zao hazina watu, lakini Mwenyezi Mungu akafichua uwongo na unafiki wao kwa kusema: wala hazikuwa ni tupu. Hawakutaka ila kukimbia tu kutoka kwenye jihadi na kuinusuru haki.

Na lau wangeingiliwa kwa pande zake, kisha wakatakiwa fitna, wan- gelifanya, na wasingelisita isipokuwa kidogo tu.

Makusudio ya fitna hapa ni kurtadi. Yaani lau jeshi la washirikina lingeingia Madina na likauzingira mji kila upande, na washirikina wawambie wanafiki wartadi na kutangaza shirk, basi wangeliitika haraka sana bila ya kusita au wangelisita kidogo tu.

Ilivyo ni kuwa mumin wa kweli hawezi kurtadi itikadi yake, bali anaipigania akiwa anajua kuwa mwema ni yule anayeigombania dini, vyovyote itakavyokuwa; kama walivyo mashahidi, hawaogopi silaha za wauaji.

Na kwa hakika walikuwa wamemwahidi Mwenyezi Mungu kabla kwamba hawatageuza migongo.

Walitumia uongo kukwepa jeshi la Mtume baada ya kutoa ahadi kwamba watashiriki hadi mauti. Katika Tafisir Tabariy imesemwa: “Bani Haritha na Bani Salama, walidhamiria waislamu washindwe siku ya Uhud; kisha wakamwahidi Mwenyezi Mungu kuwa hawatarudia milele; ndipo Mwenyezi Mungu akawakumbusha ahadi hii waliyoitoa wenyewe.” Tazama Juz. 4 (3:122).

Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa siku ya Kiyama kuhusu utekelezwaji wake,

فَمَنْ نَكَثَ فَإِنَّمَا يَنْكُثُ عَلَىٰ نَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِمَا عَاهَدَ عَلَيْهُ اللَّهَ فَسَيُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا {10}

“Basi mwenye kuvunja ahadi kwa hakika anaivunjia nafsi yake tu, na anayetekeleza aliyomwahidi Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa.” (48:10).

قُلْ لَنْ يَنْفَعَكُمُ الْفِرَارُ إِنْ فَرَرْتُمْ مِنَ الْمَوْتِ أَوِ الْقَتْلِ وَإِذًا لَا تُمَتَّعُونَ إِلَّا قَلِيلًا {16}

Sema: Hakutawafaa kukimbia; ikiwa mnakimbia kifo au kuuawa. Na hata hivyo hamtastareheshwa isipokuwa kidogo tu.

قُلْ مَنْ ذَا الَّذِي يَعْصِمُكُمْ مِنَ اللَّهِ إِنْ أَرَادَ بِكُمْ سُوءًا أَوْ أَرَادَ بِكُمْ رَحْمَةً ۚ وَلَا يَجِدُونَ لَهُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا {17}

Sema, ni nani atakayewalinda na Mwenyezi Mungu akiwatakia uovu au akiwatakia rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

قَدْ يَعْلَمُ اللَّهُ الْمُعَوِّقِينَ مِنْكُمْ وَالْقَائِلِينَ لِإِخْوَانِهِمْ هَلُمَّ إِلَيْنَا ۖ وَلَا يَأْتُونَ الْبَأْسَ إِلَّا قَلِيلًا {18}

Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanaozuilia na wanaowaambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu.

أَشِحَّةً عَلَيْكُمْ ۖ فَإِذَا جَاءَ الْخَوْفُ رَأَيْتَهُمْ يَنْظُرُونَ إِلَيْكَ تَدُورُ أَعْيُنُهُمْ كَالَّذِي يُغْشَىٰ عَلَيْهِ مِنَ الْمَوْتِ ۖ فَإِذَا ذَهَبَ الْخَوْفُ سَلَقُوكُمْ بِأَلْسِنَةٍ حِدَادٍ أَشِحَّةً عَلَى الْخَيْرِ ۚ أُولَٰئِكَ لَمْ يُؤْمِنُوا فَأَحْبَطَ اللَّهُ أَعْمَالَهُمْ ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرًا {19}

Wana choyo juu yenu. Ikija hofu utawaona wanakutazama na macho yao yanazunguka kama ambaye amezimia kwa mauti, lakini hofu inapoondoka wanawaudhi kwa ndimi kali, na wanaifanyia choyo kheri. Hao hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amezipomosha amali zao. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi.

يَحْسَبُونَ الْأَحْزَابَ لَمْ يَذْهَبُوا ۖ وَإِنْ يَأْتِ الْأَحْزَابُ يَوَدُّوا لَوْ أَنَّهُمْ بَادُونَ فِي الْأَعْرَابِ يَسْأَلُونَ عَنْ أَنْبَائِكُمْ ۖ وَلَوْ كَانُوا فِيكُمْ مَا قَاتَلُوا إِلَّا قَلِيلًا {20}

Wanadhani yale makundi hayajaondoka. Wanatamani wangelikuwa jangwani pamoja na mabedui wakiuliza habari zenu. Na lau wangelikuwa pamoja nanyi wasingelipigana isipokuwa kidogo tu.
  • 1. Nami nakumbuka mwaka huu wa 2007, kabla ya kuanza vita vya Israil, yenye nguvu zote za kijeshi, kupigana na Hizbullah, lilitolewa onyo kali kwa Hizbullah, kuwa wajisalimshe. Onyo hili lilitolewa na hata wale wanaodai ni maadui wa Israil, na kuwaambia. hamtachukua hata siku mbili mtafyekwa nyote. Matokeo yake tuliyaona. Waliweza kupambana kwa zaidi ya mwezi hadi Israili iliposalimu amri – Mtarjumu.