read

Aya 28 – 30: Ewe Nabii, Waambie Wake Zako

Maana

Wake za Mtume (s.a.w.) walimtaradhia Mtume matumizi zaidi na mapambo, kutokana na ngawira alizompa Mwenyezi Mungu, ndipo ikashuka Aya hii:

Ewe Mtume! Waambie wake zako: Ikiwa nyinyi mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni niwape kitoka-nyumba na niwaache mwachano mzuri. Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia watenda mema, miongoni mwenu, malipo makubwa.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake mtukufu awahiyarishe wakeze mambo mawili: Ama awaache pamoja na kitoka-nyumba, ikiwa wanataka, wanayoyataka wanawake wengine, ya dunia.

Kitoka-nyumba ni kitu anachotoa mtaliki kumpa mtalaka wake, kwa kuangalia uwezo wa mwanamume. Tazama Juz. 2 (2:236 – 237).

Au waishi na Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kuvumilia shida1na malipo yao mbele ya Mwenyezi Mungu huko akhera yatakuwa makubwa.

Basi wake za Mtume (s.a.w.) wakachagua akhera na wakaiacha dunia na mapambo yake. Aya hii inaitwa Ayatut-takhyir (Aya ya kuhiyarisha).

Mtume Na Wake Wengi

Aya ya takhyir ni dalili mkataa ya kukadhibisha madai ya wanaokuza mambo, kuwa Mtume alikuwa na wake kwa sababu ya matamnio ya nafsi. Kwa sababu mwenye pupa ya kustarehe na wanawake – kama alivyosema Mustafa Sadiq Rafi – hawezi kuwahiyarisha baina ya kuachana nao au kuishi maisha ya tabu mpaka siku ya mwisho; bali angeliwabembeleza na kuwaambia kuwa atafanya bidii awatimizie. Kuna mithali isemayo: “Tandiko la harusi liko ghali.”

Anasema Al- aqad katika kitabu chake: Abaqriyatul-Islamiyya: “Lau ladha ya hisia kama ingelikuwa ndio kichocheo cha kuoa baada ya kufa Khadija, basi angeliridhisha hisia zake kwa kuoa wasichana tisa wanaosifika kwa urembo huko Makka na Madina na Bara Arabu kwa ujumla. Na bila shaka angewataka wangelimkubali haraka na kwa kujionea fahari, pia mawalii wao wangeliuridhia na kuuonea fahari ukwe huu ambao haushindwi na ukwe wowote.”

Kisha Al-aqad akataja wake za Mtume mmoja baada ya mmoja na akabainisha sababu zilizopelekea kuwaoa na akasema: “Hakika wanaokuza mambo wamesahahu kila hakika miongoni mwa hakika za maisha haya ya ndoa na wakasahau kuwa Muhammad aliitwa mtakatifu na mtawa wakati wa ujana wake, na kwamba yeye alikaa miaka ishirini na tano na hakuchoka katika kuitafuta halali.

Pia wamesahau kwamba alipotaka kuoa katika miaka hiyo alimuoa mwanamke wa miaka 40 aliyemchagua kwa haja ya kuzoena, wala hakuchagua uzuri uliotakiwa kwa starehe. Wamesahau kwamba mtu waliyempa sifa za hisia za starehe, siku nyingine hakuwa akishiba na mkate wa shairi. Yote haya wameyasahau, na yamethibiti katika historia. Wameyasahau kwa vile wanataka kutia kasoro na kuupotosha uhakika.”

Enyi wake wa Mtume! Yeyote kati yenu atakayefanya uchafu dhahiri, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi.

Makusudio ya uchafu hapa ni maasi ya aina yoyote na dhahiri ni waziwazi. Wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu wana daraja tukufu mbele ya Mwenyezi Mungu na ya watu kwa kuungana kwao na Mtume mtukufu (s.a.w.). Yeyote atakayefanya maasi atakuwa amehatarisha nafasi yake na kustahiki mara mbili zaidi ya anavyostahiki mwingine. Kwa sababu Mwenyezi Mungu huwahesabu watu kulingana na vyeo vyao; kama wanavyohisabiwa kadiri ya akili zao. Amewalaumu manabii kwa namna ambayo hamlaumu mwingine.

  • 1. Baada ya vita vya Ahzab na kuwafurusha Bani Quraydha kutoka Madina, waislamu walipata ngawira na mateka wengi, jambo lililopelekea hali yao ya uchumi kuwa nzuri. Hii iliwathiri wake za Mtume kutaka matumizi zaidi, kwa sababu Mtume aliendelea kuishi vile vile alivyokuwa kimaskini. Inasemekana kuwa jambo hili, la kutaka masurufu zaidi, lilimsikitisha sana Mtume, kiasi ambacho ali- jitenga nao. – Mtarjumu.