read

Aya 50 – 52: Tumekuhalalishia Wake Zako

Maana

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika Aya hii ametaja aina ya wanawake walio halali kwa Mtume (s.a.w.) na kumwachia hiyari ya kumlalia na kutomlalia anayemtaka. Kisha akamharamishia kuzidisha wale aliokuwa nao au kubadilisha mwingine. Wakati huo alikuwa na wake tisa. Ufuatao ni ufafanuzi:

Ewe Nabii! Hakika sisi tumekuhalalishia wake zako ambao umewapa ujira wao.

Makusudio ya ujira hapa ni mahari. Na kuwapa hayo mahari kunakuwa ni lazima. Aya inaashiria kuwa Mtume anaweza kuoa idadi yoyote anayoitaka. Haya ni katika mambo yanayomuhusu yeye tu.

Unaweza kuuliza: kufunga ndoa kunaswihi hata kama mahari hayakuta- jwa, kwa nini basi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameufunga uhalali kwa mahari?
Jibu: Ulazima hapa ni wa kuyatoa hayo mahari sio kuyataja kwenye ndoa. Ikiwa mahari hayakutajwa kwenye ndoa, basi ni lazima kutoa mahari kifani; yaani yanayofana na mwingine wa aina yake. Mahari ya mtume, wakati huo, yalikuwa ni Dirhamu 500. wamekadiria Dirhamu moja kuwa ni sawa na Lira 25 za dhahabu.

Na uliowamiliki kwa mkono wako wa kuume katika aliokupa Mwenyezi Mungu katika mateka waliowatekwa nyara na waislamu kati- ka vita na washirikina, ambao wanaitwa masuria. Mwenyezi Mungu amemuhalishia Mtume wake na umma wake, wanawake hawa.

Na mabinti wa ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako na mabinti wa khalat zako waliohama pamoja nawe.

Unaweza kuuliza: Mabinti wa ami, wa shangazi, wajomba na wa khalat (dada wa mama) si wanaingia katika aina ya kwanza ya wanawake, sasa kuna haja gani ya kuhusishwa kutajwa?

Jibu: Inawezekana kuwa makusudio ya kutajwa ni kuwa inavyopendeza ni kuwa hadhi ya Mtume ni kuoa makuraishi aliohama nao kutoka mji wa ukafiri hadi mji wa Uislamu. Ama waumimi wengine ni bora kutowaoa.

Swali la pili: Watu wa sira wamesema kuwa Mtume alikuwa na ami tisa: Abbas, Hamza, Abu Twalib, Zabeir, Harith, Hijla, Muqawwam, Dhirar na Abu Lahab. Na shangazi sita: Swafiya, Ummu Hakim al-baydhau, Atika, Umayma, Arwa na Barra (Assiratu nnabaawiya cha Ibn Hisham).

Na wakasema: “Mtume hakuwa na wajomba wala khalat (mama wadogo au wakubwa), kwa sababu mama yake Amina bint Wahb (a.s.) hakuwa na kaka wala dada.” (Tafsir Ruuhul-bayan).

Sasa kuna wajihi gani wa Mwenyezi Mungu kusema: ‘Na mabinti wa ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako na mabinti wa khalat zako?’

Jibu: Makusudio ya wajomba na khalat wa Mtume ni ukoo wa mama yake unaoitwa Bani Zuhra, ambao walikuwa wakisema: “Sisi ni wajomba zake Mtume.”

Na mwanamke mumin akijitoa mwenyewe kwa Nabii ikiwa Nabii anataka kumuoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa waumini wengine.

Katika mambo yanayomuhusu Mtume tu ni kumuoa mwanamke, akitaka, ikiwa atajitoa mwenye kwa Mtume bila ya mahari, kwa masharti ya kuwa mumini. Ndio! Inajuzu kwa mwinginewe kuoa kwa mahari, kisha mke asamehe mahari, kama anavyosamehe mtu yoyote mali yake kwa mwingine.

Tunajua tuliyowafaradhishia wao kuhusu wake zao na wale waliomi- likiwa na mikono yao ya kuume. Ili isiwe dhiki juu yako. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Mwenyezi Mungu, ameweka idadi ya wake waungwana na akaharamisha mwanamke kujitoa mwenyewe bila mahari. Lakini akaliruhusu hilo kwa Mtume ili isiwe dhiki juu yake.

Vile vile kufahamisha utukufu wa cheo chake na juhudi zake. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye anayejua zaidi li lilo na masilahi zaidi kwa watu, akiwa anawahurumia na kuwaghufuria.

Unamwakhirisha umtakaye katika wao na na unamsogeza kwako umtakaye.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa uhuru Mtume wake mtukufu katika idadi ya wanawake na katika Aya hii amempa hiyari ya kuongeza au kupunguza zamu ya yeyote anayemtaka.

Na unayemtaka katika uliyemtenga si vibaya kwako.

Yaani anaweza kumrudia aliyemaliza zamu naye na kumwacha aliyekuwa kwenye zamu yake. Kwa ibara ya wanaoimudu lugha ni, anaweza kumtanguliza wa mwisho na kumweka mwisho wa kwanza.

Hivyo itakuwa ni karibu zaidi kuburudika macho yao wala wasihuzunike na wawe radhi juu ya kile unachowapa wao wote.

‘Hivyo’ ni huko kuachiwa hiyari Mtume (s.a.w.). Maana ni kuwa wao wakijua kuwa hiyari ni yako sio yao ya zamu sawa, basi kila mmoja ataridhia na vile utakavyokuwa kwake kwa siku kidogo au nyingi kwa kujua kuwa ziada hiyo imetokana na wewe wala si wajibu kwako. Pamoja na hayo, lakini Mtume alikuwa akikaa siku sawa baina ya wake zake.

Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni mwenu ya kupondokea zaidi kwa baadhi ya wake zenu kuliko wengine. Mwenyezi Mungu hayachukulii mapenzi yaliyo moyoni au chuki; isipokuwa anachukulia matendo. Hii ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mpole.

Hawakuhalalikii wanawake baadaye wala kuwabadilisha kwa wake wengine, ijapo uzuri wao utakupendeza.

Wafasiri wametaja maana tatu za Aya hii; iliyo karibu zaidi na maana ya dhahiri ni ile isemayo kuwa Mwenyezi Mungu baada ya kumhalalishia Mtume wanawake aliowaishiria katika Aya iliyotangulia, amewajibisha katika Aya hii kutosheka na alio nao ambao walikuwa tisa na akaharamishiwa kumwacha yeyote katika wao na kuweka mwingine mahali pake, hata kama atakuwa amempendeza.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Ijapo uzuri wao utakupendezainafahamisha kuwa mwanamume anaruhusiwa kumwangalia mwanamke anayetaka kumuoa.

Na ndio mafakihi wakalitolea fatwa hilio kwa kutegemea Aya hii na Hadith za Mtume mtukufu (s.a.w.).

Isipokuwa uliyemmiliki kwa mkono wako wa kuume, aliokupa Mwenyezi Mungu katika mateka.

Na Mwenyezi Mungu ni Mchungaji wa kila kitu, hata kilicho siri na kwenye dhamiri:

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنْتُمْ ۚ {4}

“Naye yu pamoja nanyi popote mlipo.” (57:4).

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَنْ يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَىٰ طَعَامٍ غَيْرَ نَاظِرِينَ إِنَاهُ وَلَٰكِنْ إِذَا دُعِيتُمْ فَادْخُلُوا فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَانْتَشِرُوا وَلَا مُسْتَأْنِسِينَ لِحَدِيثٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ يُؤْذِي النَّبِيَّ فَيَسْتَحْيِي مِنْكُمْ ۖ وَاللَّهُ لَا يَسْتَحْيِي مِنَ الْحَقِّ ۚ وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِنْ وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ ۚ وَمَا كَانَ لَكُمْ أَنْ تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّهِ وَلَا أَنْ تَنْكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِنْ بَعْدِهِ أَبَدًا ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ عِنْدَ اللَّهِ عَظِيمًا {53}

Enyi ambao mmeamini! Msiingie majumba ya Mtume ila mkipewa ruhusa ya kwenda kula, sio kungojea kiive. Lakini mtakapoitwa, basi ingieni. Na mkisha kula, tawanyikeni wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii, naye anawastahi nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa haki. Na mnapowaomba chombo cha nyumbani, basi waulize nyuma ya mapazia. Hilo linasafisha zaidi nyoyo zenu na nyoyo zao. Haiwafalii nyinyi kumuudhi Nabii wala kuwaoa wake zake kabisa. Hakika hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

إِنْ تُبْدُوا شَيْئًا أَوْ تُخْفُوهُ فَإِنَّ اللَّهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا {54}

Mkidhihirisha chochote au mkikificha, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

لَا جُنَاحَ عَلَيْهِنَّ فِي آبَائِهِنَّ وَلَا أَبْنَائِهِنَّ وَلَا إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ أَخَوَاتِهِنَّ وَلَا نِسَائِهِنَّ وَلَا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ ۗ وَاتَّقِينَ اللَّهَ ۚ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا {55}

Hapana ubaya kwao kwa baba zao, wala watoto wao, wala kaka zao, wala watoto wa kaka zao, wala watoto wa dada zao, wala wanawake wao, wala wale waliomilikiwa na mikono yao ya kuume. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kushuhudia kila kitu.