Aya 1 – 6: Sifa Njema Zote Ni Za Mwenyezi Mungu
Maana
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na sifa ni zake katika Akhera. Naye ni Mwenye hekima, Mwenye habari.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye mwenye kustahiki kusifiwa kwa sifa njema katika nyumba mbili. Ni mmliki wa ulimwengu na mpangiliaji wake kwa vyote vilivyomo ndani yake, kulingana na elimu yake na hekima yake.
Kwenye Nahjul-Balagha, imesemwa: “Tunamsifu kwa ukubwa wa hisani yake na wema wa dalili yake na ziada ya fahila zake na neema zake. Sifa ambazo ni haki yake (sisi) kuzitekeleza na kulipa shukrani zake na kujikurubisha kwenye thawabu zake na kutaka ziada ya wema wake.”
Anayajua yanayoingia katika ardhi na yanayotoka humo na yanayoteremka kutoka mbinguni na yanayopanda huko na Yeye ni Mwenye kurehemu, Mwingi wa maghufira.
Maana ya Aya hii yamekaririka katika Aya kadhaa; ikiwemo Juz. 7 (6:59) na Juz. Juz. 11 (10:61). Ufupisho wake ni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Na walisema wale ambao wamekufuru: Haitatufikia saa ya Kiyama. Sema: Ndio! Naapa kwa Mola wangu, itawafikia.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 11(10:53).
Mjuzi wa ghaibu. Hapana kinachofichikana kwake hata chenye uzito wa chembe, si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho kidogo katika hivyo wala kikubwa zaidi; ila vimo katika Kitabu chenye kubainisha.
Kitabu chenye kubainisha ni kinaya cha kuhifadhi. Maana ni kuwa hakuna anayejua wakati wa Kiyama isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake. Tazama Juz. 9 (7:187).
Ili awalipe wale ambao wameamini na wakatenda mema. Hao watapata maghufira na riziki yenye heshima. Na wale ambao wamehangaika kuzipinga ishara zetu wakiona watashinda, hao watapata adhabu mbaya yenye uchungu.
Huu ni ubainifu wa hekima ya ufufuo, ambayo ni kulipwa mema waliofanya wema na wale waliofanya uovu walipwe kwa uovu wao. Tazama Juz. 11 (10:3-4). Kifungu cha “Hisabu na malipo ni lazima.”
Na wale ambao wamepewa ilimu wanaona kuwa uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako ni haki na huongoza kwenye njia ya Mwenye nguvu, Mwenye kusifiwa.
Makusudio ya wale waliopewa ilimu ni kila mwenye ilimu aliye na insafu, wakati wowote na mahali potepote. Na makusudio ya uliyoteremshiwa ni Qur’an. Maana ni kuwa yeyote mwenye ilimu atakayeisoma Qur’an kiusahihi, lazima ataishia kuwa ni haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu; kwa sababu iko sawasawa kwenye itikadi yake, sharia yake na mafunzo yake yote.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا هَلْ نَدُلُّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ يُنَبِّئُكُمْ إِذَا مُزِّقْتُمْ كُلَّ مُمَزَّقٍ إِنَّكُمْ لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ {7}
أَفْتَرَىٰ عَلَى اللَّهِ كَذِبًا أَمْ بِهِ جِنَّةٌ ۗ بَلِ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ فِي الْعَذَابِ وَالضَّلَالِ الْبَعِيدِ {8}
أَفَلَمْ يَرَوْا إِلَىٰ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ مِنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ إِنْ نَشَأْ نَخْسِفْ بِهِمُ الْأَرْضَ أَوْ نُسْقِطْ عَلَيْهِمْ كِسَفًا مِنَ السَّمَاءِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِكُلِّ عَبْدٍ مُنِيبٍ {9}