read

Aya 10 – 14: Daud Na Suleiman

Maana

Na kwa hakika tulimpa Daud fadhila kutoka kwetu. Enyi milima sabihini pamoja naye na ndege. Na tukamlainishia chuma.

Katika Juz. 6 (4:163) Mwenyezi Mungu anasema: “Na Daud tukamapa Zaburi,” kwenye Juz. 19 (27:15) anasema: “Na hakika tulimpa Daud na Suleiman elimu” na kwenye Aya hii tuliyo nayo anaseama kuwa amempa neema ya sauti nzuri ambayo ilikuwa inakurubia kwenda sambamba na sauti ya milima na ndege.

Katika Juz. 17 (21:79) tulisema kuwa inawezekana kuwa tasbihi ya milima na ndege ni tasbihi halisi hasa pamoja na Daud, Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. Kuna msemaji aliyesema kuwa makusudio ya kusabihi milima na ndege pamoja na Suleimani ni kuwa ilikuwa ikimfanya asabihi; alipokuwa akiiona husema: “Subhana man khalaqa wa swawwara...” (Kutakasika ni kwa aliyeumba na akatia sura...).

Pia Mwenyezi Mungu alimneeemesha Daud kwa kukifanya chuma vile anavyotaka yeye bila ya kukitia motoni au kukigonga na nyundo. Inawezekana kuwa Mwenyezi Mungu alimfahamisha sababu na nyenzo za kukilainisha chuma.

Kwamba utengeneze nguo za chuma pana na kadiria sawa katika kuunganisha.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Daud atengeneze deraya kutokana na chuma na atengeneze vizuri kuzuia panga mishale na mikuki na ziwe pana kwa namna ambayo mvaaji haitamzuia na harakati zozote.

Na tendeni mema. Hakika ninayaona mnayotenda.

Maneno yanaelekezwa kwa Daud na kizazi chake. Mwenyezi Mungu anawaamrisha wafanye mema na kuwa ameayaandalia malipo na thawabu. Umetangulia mfano wa Aya mbili hizi katika Juz. 17 (21:79 – 80).
Na kwa Suleiman upepo. Safari yake ya asubuhi ni mwendo wa mwezi mmoja na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi mmoja.

Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa upepo ulikuwa ukimchukua Suleiman, anakotaka, kwa amri ya Mungu na kwamba masafa ya mwezi mzima kwa ngamia au kutembea kwa miguu alikuwa akienda kwa asubuhi moja na vile vile jioni.

Na tukamtiririshia chemchemi ya shaba.

Makusudio ya kumtiririshia hapa ni kumyeyushia. Yaani Mwenyezi Mungu Mtukufu alimyeyushia chuma Suleimani kama alivyomyeyushia baba yake Daud. Inawezekana kuwa Mwenyezi Mungu alimuongoza kwenye sababu za kuyeyusha.

Na katika majini kuna waliofanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake. Na anayejitenga na amri katika wao tunamwonjesha adhabu ya moto unaowaka. Wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu na masanamu na sinia kubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyoondoka mahali pake.

Imetangulia pamoja na tafsiri yake katika Juz. 17 (21:82).

Fanyeni amali enyi watu wa Daud kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu wanaoshukuru.

Ibn Al-arabi ameitaja Aya hii katika Futuhat Juz. 4, akasema: Shukrani ni kuiona neema kuwa imetoka kwa Mungu si kwa mwingine. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimpa wahyi Musa akamwambia: Nishukuru kwa haki ya kushukuru. Akasema Musa: “Ni nani anayeweza hilo ewe Mola?” Akamwambia: “Ikiwa unaona neema imetokana na mimi basi umenishukuru.”

Tulipomkidhia mauti, hapana aliyewajulisha mauti yake ila mnyama wa ardhi aliyekula fimbo yake. Alipoanguka majini walitambua lau kuwa wangelijua ya ghaibu wasingelikaa katika adhabu ya kufedhehesha.

Aliyekidhiwa na mauti ni Suleiman. Mnyama wa ardhi ni mchwa anayekula miti. Maana ni kuwa Suleimani alifikiwa na mauti akiwa ameegemea fimbo yake; akabakia hivyo mpaka muda aliotaka Mwenyezi Mungu, majini na watu wakimwangalia na kumdhania kuwa yuko hai, mpaka pale mchwa walipokula fimbo yake kwa ndani, ikavunjika na Suleiman akaanguka; hapo wote wakajua kuwa amekufa; ikadhihirika kwa watu kuwa majini hawajui ghaibu. Kwa sababu lau wangelijua basi wasingelikuwa katika utumishi wa Suleiman akiwa ni maiti.

Ikiwa baadhi ya yaliyo katika Aya hii yanaonekana, kwa kawaida, ni vigumu kutokea, lakini kiakili inakubalika kutokea. Ndio maana tunayasadiki na kuyakubali; tukiwa tunaamini msingi wa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Mtume (s.a.w.) wake mtukufu.

Tazama Juz. 3 (3:45 – 51) kifungu cha “Lisilowezekana kiakili na kidesturi.”

Kupinga Fikra Ya Kidini

Kutoka na kutajwa majini na mambo yasiyo ya kawaida katika Aya hii, ni vizuri tutaje yaliyoelezwa kwenye kitabu kilichotoka hivi karibuni, kina- choitwa Naqdu lfikri ddiniy. (Kupinga fikra ya kidini).

Hivi sasa tuko katika mwezi wa Novemba 1969. Yamezungumzwa mengi kuhusu kitabu hicho na mtungaji wake. Mwenye kusoma kitabu hicho mara moja atamhukumu mtungaji wake kuwa ana shaka na wasiwasi na dini zote. Hilo amelisema waziwazi kwenye Uk. 29, 77 na nyinginezo.

Lakini mwenye kukifuatilia kitabu na kuchukua dhahiri yake, ataona kuwa yaliyopelekea shaka na wasiwasi huu ni mambo yafutayo:

Kwanza: Kujaribu baadhi ya waumini kulazimisha kuoanisha nukuu za Qur’an na ugunduzi wa kisayansi, na kuzama sana kuleta taawili iliyo mbali na matamshi. Mtunzi wa kitabu hicho amelitolea ushahidi mwingi hilo, yakiwemo yale aliyoyanukuu katika Uk. 37, kwamba ugunduzi wa chembe za mwanga unafahamisha kuweko malaika na majini.

Mtungaji akielezea kauli hii alisema: “Sijui kuna uhusiano gani baina ya nadharia ya mwanga na kuweko majini.”

Pili: Mazoweya na nembo za kidini zilizoganda haziendani na maendeleo ya karne ya ishirini; kama anavyodai mwandishi.

Tatu: Baadhi ya wakuu wa dini kuunga mkono ukabaila na ukoloni kwa kutumia jina na Uislamu au Ukristo. Kitabu kimejaa ushahidi wa hilo; kama vile kwenye uk. 23: “Dini huko ulaya ilikuwa rafiki mkubwa wa serikali za kikabaila, hali ambayo inaendelea hadi sasa katika miji mbalimbali, hasa ndani ya miji ya kiarabu na nje, na vile dini inavyoungana moja kwa moja na ukoloni mambo leo unaongozwa na Marekani.”

Mtungaji aliongeza katika kupinga kitabu “Almasihiyya wal Islamu fi Lubnan” (Ukiristo na Uislmu Lebanon) ambacho ni mkusanyiko wa mihadhara ya Lebanon ya mwaka 1965, iliyotolewa na wakuu wa kidini wane: mmoja wa kisunni, mwengine wa kishia na wawili wa kikiristo.

Na wengine wane wa wasiokuwa na dini yoyote, lakini walizungungumza kwa niaba ya dini. Wote wakamwahidi Mwenyezi Mungu kuwa watafanya bidii ya kudumu kuondoa pingamizi zinazowekwa baina ya Uislamu na ukiristo.

Miongoni mwa aliyoyasema mtungaji huyu, katika kuwarudi wale waliotoa ahadi, ni yale yaliyo katika ukurasa wa 64, wa Kitabu chake hicho: “Lengo la kwanza la mihadhara na ahadi hizo ni wakristo kuunga mkono serkali ya Lebanon, kwa vile inawanufaisha wao zaidi kuliko waislamu walio na ufukara sana.

Baadhi ya waislamu nao wanaikubali serikali na kuungana na wakiristo, na kuaiachia serikali usimamizi wote wa kisiasa, kijamii na kiuchumi, si kwa lolote ila ni kwa kuwa wanapata manufaa fulani na faida kutoka serikalini. Kiasi ambacho maovu ya serikali yamesahaulika na kuelekea kwenye nembo ya mshikamano wa wakiristo na waislamu.”

Dalili mkataa kuwa malengo ni masilahi sio mshikamano wa kidini, mwandishi anaiweka wazi kwenye Uk. 60, katika kitabu chake, akisema: “Hakika Uislamu hauikubali Biblia, utatu, mhanga, kusulubiwa Bwana Masih, kuzikwa kwake na kutoka kwake kaburini n.k. Kama ambavyo wakiristo nao hawaikubali Qur’an wala utume wa Muhammad (s.a.w.) n.k. Sasa hawa wahadhiri na ahadi zao wataondoa vipi pingamizi hizi? Usawa hasa ni kufahamiana na kuelewena Walebanoni kwa uzalendo wao tu na misingi ya ushirikiano kwa masilahi yao, lakini dini aachiwe hiyari kila mtu kulingana na alivyokinai na mazoweya yake.”

Kutokana na kauli ya mwandishi huyu na wengineo wengi, katika kupinga fikra ya dini, inatubainikia kuwa siri ya upinzani wao, kama tulivyodokeza mwanzoni, imetokana na wakuu wa dini kuukumbatia ukoloni, udhalimu na ukandamizaji na kuupamba kwa jina la dini.

Lau wakuu wote wa dini wangeifanyia ikhlasi, wakaifahamisha kwa ufahamu sahihi na wakaibanisha kama alivyoiteremsha Isa na Muhammad na wasiiuze kwa thamani ndogo, basi wapinzani au washambulizi wa kulipwa wasingelipata mwanya wa kuituhumu au kuwa na shaka na dini ya kiislamu wala ya kikiristo.

Lakini jambo la kuvunja moyo ni kuwa watu wamelitumia jina la dini kwa uzushi na wengine wakasimama kuiharibu na kuingiza shaka baada ya kulipwa na maadui wa Mwenyezi Mungu; ndio ikawa radiamali hii kuto- ka kwa mwandishi huyu wa kitabu ‘Kupinga fikra ya dini’ na wengineo. Inasemekana pia mwandishi huyu ni katika wanaolipwa.

Hata hivyo, kwani dini itakuwa imekosea nini ikituhumiwa na wazushi na wenye upendeleo? Ilitakikana mwandishi aangalie ushahidi mwingi ulio katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na suna za Mtume wake na pia katika historia ya Uislamu kuwa dini ni nguvu inayomwelekeza mtu kwenye maisha bora na kwamaba iko mbali na kila jambo lisiloingilika akilini na kugongana na hakika ya maisha.

Hakika hii wanakubaliana nayo wataalamu wengi wa mashariki na wa magharibi wasiokuwa waislamu. Tazama Juz. 1 (2:1-5) kifungu cha ‘Qur’an na Sayansi,’ Juz. 9 (8:24) kifungu cha ‘Dini na maisha,’ na Juz. 15 (17:9-12) kifungu cha ‘Uislamu ni dini ya maumbile’

لَقَدْ كَانَ لِسَبَإٍ فِي مَسْكَنِهِمْ آيَةٌ ۖ جَنَّتَانِ عَنْ يَمِينٍ وَشِمَالٍ ۖ كُلُوا مِنْ رِزْقِ رَبِّكُمْ وَاشْكُرُوا لَهُ ۚ بَلْدَةٌ طَيِّبَةٌ وَرَبٌّ غَفُورٌ {15}

Hakika ilikuwa ishara kwa wasabaa katika maskani yaobustani mbili, kulia na kushoto. Kuleni katika riziki ya Mola wenu na mumshukuru. Mji mzuri na Mola mwenye maghufira.

فَأَعْرَضُوا فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ سَيْلَ الْعَرِمِ وَبَدَّلْنَاهُمْ بِجَنَّتَيْهِمْ جَنَّتَيْنِ ذَوَاتَيْ أُكُلٍ خَمْطٍ وَأَثْلٍ وَشَيْءٍ مِنْ سِدْرٍ قَلِيلٍ {16}

Lakini wakaacha, basi tukawapelekea mafuriko makubwa na tukawabadilishia bustani zao kwa bustani nyingine mbili zenye matunda makali na mivinje na miti michache ya kunazi.

ذَٰلِكَ جَزَيْنَاهُمْ بِمَا كَفَرُوا ۖ وَهَلْ نُجَازِي إِلَّا الْكَفُورَ {17}

Hayo tuliwalipa kwa vile walikufuru, nasi kwani tunamwadhibu isipokuwa anayekufuru?

وَجَعَلْنَا بَيْنَهُمْ وَبَيْنَ الْقُرَى الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا قُرًى ظَاهِرَةً وَقَدَّرْنَا فِيهَا السَّيْرَ ۖ سِيرُوا فِيهَا لَيَالِيَ وَأَيَّامًا آمِنِينَ {18}

Na baina yao na miji mingine tuliyoibariki, tuliweka miji iliyo dhahiri na tukaweka humo vituo vya safari: Nendeni humo usiku na mchana kwa amani.

فَقَالُوا رَبَّنَا بَاعِدْ بَيْنَ أَسْفَارِنَا وَظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ فَجَعَلْنَاهُمْ أَحَادِيثَ وَمَزَّقْنَاهُمْ كُلَّ مُمَزَّقٍ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ {19}

Wakasema: Mola wetu, weka mwendo mrefu baina ya safari zetu. Na wakazidhulumu nafsi zao. Basi tukawafanya ni masimulizi na tukawatawanyatawanya. Hakika katika hayo, bila shaka kuna ishara kwa kila aliye na subira sana mwenye kushukuru.

وَلَقَدْ صَدَّقَ عَلَيْهِمْ إِبْلِيسُ ظَنَّهُ فَاتَّبَعُوهُ إِلَّا فَرِيقًا مِنَ الْمُؤْمِنِينَ {20}

Na hakika Ibilisi alisadikisha dhana yake juu yao. Na walimfuata isipokuwa kundi la waumini.

وَمَا كَانَ لَهُ عَلَيْهِمْ مِنْ سُلْطَانٍ إِلَّا لِنَعْلَمَ مَنْ يُؤْمِنُ بِالْآخِرَةِ مِمَّنْ هُوَ مِنْهَا فِي شَكٍّ ۗ وَرَبُّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَفِيظٌ {21}

Naye hakuwa na mamlaka yoyote juu yao, ila ni kwa sababu tujue ni nani mwenye kuamini Akhera na nani anayetilia shaka. Na Mola wako ni mwenye kuhifadhi kila kitu.