read

Aya 31-33: Hawataamini Qur’an

Maana

Na walisema waliokufuru: Hatutaiamini Qur’an hii, wala yaliyokuwa kabla yake, kama vile Tawrat na Injil. Walioyasema haya ni washirikina, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَٰذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا {30}

Na Mtume alisema: Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur’an ni mahame.” Juz. 19 (25:30).

Wameihama na kuikana kwa sababu inamfanya sawa mweusi na mweupe na ikawaambia:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِنْ قَوْمٍ عَسَىٰ أَنْ يَكُونُوا خَيْرًا مِنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِنْ نِسَاءٍ عَسَىٰ أَنْ يَكُنَّ خَيْرًا مِنْهُنَّ ۖ وَلَا تَلْمِزُوا أَنْفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ ۖ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ ۚ وَمَنْ لَمْ يَتُبْ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ {11}

“Enyi ambao mmeamini! Wanaume wasiwadharau wanaume wengine, huenda wakawa bora kuliko wao; wala wanawake kwa wanawake wengine, huenda wakawa bora kuliko wao. Wala msitiane kasoro, wala msiitane majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya imani.” (49:11).

Vile vile waliukana utume wa Muhammad (s.a.w.) kwa sababu alitaka kuwatoa kwenye ujinga na kurudi nyuma, waende kwenye elimu na maendeleo.
Mtaalamu mmoja wa Ulaya, Jack Rezler, aliyeandika kitabu kuhusu mwamko wa kiislamu na kingine kinachozungumzia maendeleo ya waarabu ambavyo vilichapishwa ufaransa mnamo 1962, alisema: “Hatua ya kwanza ya maendeleo ya waarabu ilianza kwa kujitokeza dini ya kiislamu.

Kuna sababu kadhaa zilizofanya maendeleo haya na kuenea kwake; sababu kubwa zaidi ni kuweko na roho ya kimaana kwa Waislamu kupitia dini hii mpya; jambo ambalo limeleta ushujaa, kiasi cha kufikia kuyadharau mauti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.”

Na ungeliwaona madhalimu watakaposimamishwa mbele ya Mola wao wakirudishiana maneno!

Baada ya Mtume (s.a.w.) kukata tamaa kuwa washirikina wataamini, Mola Mtukufu alimtuliza na kumwambia kuwa kesho utaona hawa waongo watakavyokuwa dhalili na kuhizika pale watakaposimama mbele ya Mwenyezi Mungu kwa hisabu, jinsi mfuasi atakavyomlaumu aliyemfuata – kila mmoja atamtia makosani mwingine wale wanyonge wakiwaambia wale waliojifanya wakubwa: Lau si nyinyi bila shaka tungelikuwa waumini.

Wanyonge ni wale wafuasi; na waliojifanya wakubwa ni viongozi.

Wale waliojiona wakubwa watawaambia wale wanyonge:

Kwani sisi ndio tuliowazuia na uongofu baada ya kuwafikia? Bali nyinyi wenyewe mlikuwa waovu, sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

كَمَثَلِ الشَّيْطَانِ إِذْ قَالَ لِلْإِنْسَانِ اكْفُرْ فَلَمَّا كَفَرَ قَالَ إِنِّي بَرِيءٌ مِنْكَ إِنِّي أَخَافُ اللَّهَ رَبَّ الْعَالَمِينَ {16}

“Kama mfano wa shetani anapomwambia mtu: Kufuru. Na akikufuru humwambia: Mimi si pamoja nawe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu. (59:16).

Sio mbali kuwa shetani katika Aya hii ni kinaya cha viongozi wapotevu wanaopoteza.

Na wale wanyonge watawaambia wale waliojifanya wakubwa: Bali ni vitimbi vyenu vya usiku na mchana, mlipokuwa mkituamrisha tumkufuru Mwenyezi Mungu na tumfanyie washirika.

Wafuasi na viongozi watakapokata tamaa ya kuokoka watatupiana lawama na kutuhumiana, kila kundi likijaribu kuwatupia makosa wengine; sawa na wezi wanapoafikiana kufanya uhalifu, lakini wanaposhikwa wanalaniana wao kwa wao.

Mwisho ushindi utakuwa ni wa wafuasi, kwa kuwakabili waliojifanya wakubwa kwa njama walizozifanya usiku na mchana na kuwadanga na ukafiri na ushirikina kwa njia mbalimbali.

Hata hivyo hilo halitawaondolea adhabu wala kuwapunguzia, maadamu walikuwa na akili na kulifanya hilo kwa hiyari yao: “Wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola wetu! Hawa ndio waliotupoteza basi uwape adhabu ya moto maradufu. Atasema: Itakuwa maradufu kwenu nyote, lakini hamjui.” Juz. 8 (7:38).

Nao wataficha majuto watakapoiona adhabu. Yaani wafuasi na waliofuatwa. Kila mwenye kuzembea na kupituka mipaka mwisho wake ni adhabu na majuto.

Na tutaweka minyororo shingoni mwa wale waliokufuru, viongozi na wafuasi wao. Kwani wanalipwa ila kwa waliyokuwa wakiyatenda? Kabisa! Mtu atalipwa kwa aliyoyafanya tu na Mola wako si mwenye kuwadhulumua waja.

وَمَا أَرْسَلْنَا فِي قَرْيَةٍ مِنْ نَذِيرٍ إِلَّا قَالَ مُتْرَفُوهَا إِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُمْ بِهِ كَافِرُونَ {34}

Na hatukumtuma mwonyaji yeyote kwenye mji ila walisema wapenda anasa wake: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyotumwa nayo.

وَقَالُوا نَحْنُ أَكْثَرُ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ {35}

Na wakasema: Sisi tuna mali nyingi zaidi na watoto, wala sisi hatutaadhibiwa.

قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَنْ يَشَاءُ وَيَقْدِرُ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {36}

Sema: Hakika Mola wangu humkunjulia riziki amtakaye na huikunja, lakini watu wengi hawajui.

وَمَا أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ بِالَّتِي تُقَرِّبُكُمْ عِنْدَنَا زُلْفَىٰ إِلَّا مَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَأُولَٰئِكَ لَهُمْ جَزَاءُ الضِّعْفِ بِمَا عَمِلُوا وَهُمْ فِي الْغُرُفَاتِ آمِنُونَ {37}

Na si mali yenu wala watoto wenu watakaowajongeza kwetu muwe karibu, isipokuwa aliyeamini na akatenda mema. Hao basi watapata malipo maradufu, kwa waliyoyafanya nao watakuwa salama katika maghorofa.

وَالَّذِينَ يَسْعَوْنَ فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَٰئِكَ فِي الْعَذَابِ مُحْضَرُونَ {38}

Na wale ambao wanajitahidi kuzipinga ishara zetu, wakaona watashinda, hao watahudhurishwa kwenye adhabu.

قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَنْ يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ ۚ وَمَا أَنْفَقْتُمْ مِنْ شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ {39}

Sema: Hakika Mola wangu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake na humkunjia. Na chochote mtakachotoa Yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanaoruzuku.

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ {40}

Na siku atakayowakusanya wote, kisha atawaambia Malaika: Je, hawa walikuwa wakiwaabudu?

قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنْتَ وَلِيُّنَا مِنْ دُونِهِمْ ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ ۖ أَكْثَرُهُمْ بِهِمْ مُؤْمِنُونَ {41}

Watasema: Umetakasika! Wewe ndiye walii wetu sio hao. Bali walikuwa wakiwaabudu majini; wengi wao wakiwaamini hao.

فَالْيَوْمَ لَا يَمْلِكُ بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ نَفْعًا وَلَا ضَرًّا وَنَقُولُ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا ذُوقُوا عَذَابَ النَّارِ الَّتِي كُنْتُمْ بِهَا تُكَذِّبُونَ {42}

Na leo hii hawataweza baadhi yenu kuwaletea nafuu wengine wala kuwadhuru. Na tutawaambia wale ambao wamedhulumu: Onjeni adhabu ya Moto mliokuwa mkiukadhibisha.