Aya 51 – 54: Wataipata Wapi?
Maana
Na lau ungeliwaona watakapofazaika, basi hapana pa kukimbilia, na watakamatwa mahala pa karibu.
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.), kukamatwa mahala pa karibu ni kinaya cha kuwa kwenye uweza wa Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa, ewe Muhammad (s.a.w.) lau utaona kesho hofu na adhabu, isiyokuwa na kimbilio, itakayowapata wale wanaokadhibisha utume wako, basi utastaajabu.
Hii ni kemeo kwa washirikina na tulizo kwa Bwana wa Mitume.
Na watasema tumemwamini! Lakini watapata wapi kutoka huko mahali mbali?
Wanayesema ‘tumemwamini’ ni Muhammad (s.a.w.), kwa sababu amekwishatajwa kwenye Aya 46 ‘Mwenzenu hana wazimu.’
Maana ni kuwa, wale waliomkadhibisha Muhammad, watakapoiona adhabu watasema tumemwamini, lakini wataipata wapi imani hii au itawafaa nini huko mbali. Kwa sababu siku ya Kiyama ni siku ya hisabu na malipo sio siku ya imani na matendo. Imam Ali (a.s.) anasema: “Leo ni matendo si hisabu na kesho ni hisabu sio matendo... Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Jipimeni kabla ya kupimwa na mjihisabu kabla ya kuhisabiwa.”
Na walikwishamkataa hapo zamani. Muda wa kufaa imani umekwisha.
Wakiyatupilia mbali ya ghaibu kutoka mahali mbali.
Kutupilia mbali ni kusema bila ya ilimu, kutoka mahali mbali ni kinaya cha umbali wa kuliza na kutoamini kwao haki. Maana ni kuwa, wao walikuwa wakisema Muhammad ni mzushi, mchawi na mwendawazimu; wala hakuna Pepo au Moto. Waliyasema hayo kwa ujinga na bila ya dalili.
Na watawekewa kizuizi baina yao na hayo wanayoyatamani.
Wanatamani kuokoka na adhbau ya Jahannam, ndio wakakimbilia imani na toba, lakini baada ya kupita muda, basi watazidi majuto na machungu.
Kama walivyofanyiwa wenzao zamani.
Walikuwa na wanaofanana nao katika uma zilizopita; walimpinga Mola wao katika maisha ya dunia na kufazaika akhera. Wataambiwa:
قَالَ اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ {108}
Hakika wao walikuwa katika shaka ya kutia wasiwasi ya ufufuo.