read

Aya 1 – 3: Sifa Njema Ni Za Mwenyezi Mungu

Maana

Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Muumba wa mbingu na ardhi aliyewafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili mbili, tatu tatu na nne nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza juu ya kila kitu.

Mwenyezi Mungu amejisifu Yeye mwenyewe ili atufundishe jinsi ya kumsifu na kumshukuru. Aya inafahamisha kuwa katika Malaika kuna walio na mbawa mbili, wenye tatu na wenye nne na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu huzidisha mbawa vile atakavyo. Haya na yanayofanana nayo yanaafikiana na uwezo wa Mwenyezi Mungu na akili haiyakatai. Yasiyokuwa hayo tunamwachia Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kwa vile sisi hatutaulizwa wala hayana uhusiano wowote na maisha yetu, wala hayana dalili na Aya au Hadith mutawatir.
Ninahofia wale wanaolazimisha kuzifanyia taawili nukuu za dini ziende sambamba na elimu ya kisasa waseme kuwa mbili mbili ni ishara ya ndege yenye injini mbili, tatu tatu ni yenye tatu, nne nne ni yenye nne na kuzidisha katika kuumba ni kuwa ndege zitakazokuja baadaye zenye injini nyingi.

Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hakuna wa kuizuia na anayoizuia hakuna wa kuiachia isipokuwa Yeye, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

Makusudio ya rehema hapa sio mali tu; kama walivyosema baadhi ya wafasiri. Wala sio mali, afya na cheo; kama walivyosema wengine. Kwani mali inapelekea uasi na ukandamizaji. Tumewaona wengi wenye mali wamewageuza wengine wanyonge kuwa ni mashirika wanayoyamiliki na kuwageuza kuwa ni watumwa wao wanaowatumikia au wawe wakimbizi.

Afya nayo inampelekea mtu kwenye hatari. Ama cheo, ndio kabisa, aghlabu kinakuwa ni chombo cha dhulma na uadui. Elimu nayo mara nyingine inakuwa ni afadhali ujinga; kama vile elimu iliyotengeneza bomu la nyukilia na silaha za maangamizi.

Hapana! Makusudio ya rehema yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, katika Aya hii, sio mali peke yake, wala afya pekee yake wala sio cheo na elimu tu. Isipokuwa makusudio ni huruma ya Mwenyezi Mungu, mwongozo wake wa heri na kinga yake ya shari. Imam Ali (a.s.) anasema: “Shida inapofika kikomo huja faraja na inapokaza sana minyororo ya dhiki hupatikana raha.”

Mara nyingi tumeshuhudia matatizo madogo yanazidi kuwa makubwa kila mwenyewe anavyojitahidi kuyatatua, na tunaona yale makubwa yanatatu- ka kwa wepesi au kwa haraka. Hakuna siri ya hilo ila matakwa ya Mwenyezi Mungu na rehema yake. Amesema kweli aliyesema: “Mtu anaweza kulala kwenye miba, pamoja na rehema ya Mwenyezi Mungu, akaamka kwenye tandiko. Na anaweza kulala kwenye hariri bila ya rehe- ma ya Mwenyezi Mungu akaamka kwenye miba.”1

Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Je, yuko muumba mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu anayewapa riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Hapana Mola ila Yeye basi mnageuzwa wapi?

Ukumbusho huu wa neema ya Mwenyezi Mungu na kwamba Yeye peke yake ndiye muumba na mwenye kuruzuku ni kuisisitiza Aya iliyotangulia: ‘Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu...’

Katika Nahjul-Balagha imeelezwa: “Mara ngapi Mwenyezi Mungu amewahusisha na neema yake na akwaunganisha na rehema yake. Mmekuwa uchi akawasitiri, mkafanya ya kuwaadhibu akawapa muda. Basi zikamilisheni neema za Mwenyezi Mungu kwa kuwa na subira ya kumtii na kujiweka mbali na maasi, kwani hakika kesho kuanzia leo ni karibu.”

وَإِنْ يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِنْ قَبْلِكَ ۚ وَإِلَى اللَّهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ {4}

Na kama wakikukadhibisha, basi wamekwisha kadhibishwa Mitume kabla yako na mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu.

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ ۖ فَلَا تَغُرَّنَّكُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا ۖ وَلَا يَغُرَّنَّكُمْ بِاللَّهِ الْغَرُورُ {5}

Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Basi yasiwadanganye maisha ya dunia, wala mdanganyifu asiwadanganye juu ya Mwenyezi Mungu.

إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا ۚ إِنَّمَا يَدْعُو حِزْبَهُ لِيَكُونُوا مِنْ أَصْحَابِ السَّعِيرِ {6}

Hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi lake liwe katika watu wa motoni.

الَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ مَغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ {7}

Wale ambao wamekufuru watakuwa katika adhabu kali na wale ambao wameamini watapata maghufira na malipo makubwa.

أَفَمَنْ زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ فَرَآهُ حَسَنًا ۖ فَإِنَّ اللَّهَ يُضِلُّ مَنْ يَشَاءُ وَيَهْدِي مَنْ يَشَاءُ ۖ فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ {8}

Je, yule aliyepambiwa ubaya wa tendo lake akaliona ni jema - basi hakika Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye na humwongoa amtakaye. Basi roho yako isitoke kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya.
  • 1. ‘Unaweza kulala maskini ukaamka tajiri’ – Msemo wa kiswahili