Aya 4 – 8: Walikadhibishwa Mitume Kabla Yako
Maana
Na kama wakikukadhibisha, basi wamekwisha kadhibishwa Mitume kabla yako na mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, amlipe thawabu muumini mwenye kusubiri katika jihadi yake na amuadhibu mwenye kuikadhibisha haki kwa sababu ya kukadhibisha kwake.
Lengo la Aya hii ni kumpoza Mtume (s.a.w.) na kuwakaripia mahasimu na maadui wake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 ( 3:183) na Juz. 17 (22:42).
Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Basi yasiwadanganye maisha ya dunia, wala mdanganyifu asiwadanganye juu ya Mwenyezi Mungu.
Makusudio ya ahadi hapa ni hisabu na malipo baada ya mauti. Udanganyifu wa dunia ni mali, jaha, wanawake, watoto na udanganyifu wa shetani. Umetangulia mfano wake katika Juz. 21 (31:33).
Hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi lake liwe katika watu wa motoni.
Shetani ametangaza waziwazi uadui wake na binadamu kwa kusema: “Kwa ulivyonipoteza, basi nitahakikisha ninawazaini hapa ardhini na nitawapoteza wote.” Juz. 14 (15:39).
Kundi lake ni wale wafuasi wake wanaosikiliza wasiwasi wake na udanganyifu wake. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametuhadharisha kumtii, kwa sababu mwito wake ni wa ufisadi na wa maangamizi, na Mwenyezi Mungu anatoa mwito wa kheri na rehema.
Wale ambao wamekufuru watakuwa katika adhabu kali na wale ambao wameamini watapata maghufira na malipo makubwa.
Kila mtu atakuwa na mwisho, mtamu au mchungu. Mwisho wa mwenye kukufuru na akafanya ufisadi ni Jahannam, makazi maovu; na mwisho wa mwenye kuamini na akatenda mema ni Pepo ambayo ni raha ya daima.
Je, yule aliyepambiwa ubaya wa tendo lake akaliona ni jema.
Kinahaw, hapa kuna maneno ya kukadiriwa kuwa: ‘ni kama ambaye hakupambiwa’ Hakuna mtu yoyote anayeishi bila ya falsafa na kuchukulia mfano wa juu; hata wale wanaokataa falsafa na mfano, huko kukataa kwao ndio falasafa yao na mfano wa juu. Ndio maana ikasemwa: Mwenye kukataa falsafa ndio amekuwa na falsafa.
Tofauti ni kuwa kuna yale anayeijengea falsafa yake kwenye majaribio na uchambuzi, mwengine anaijengea kwenye akili au dini na kuna yale anayeijengea kwenye dhati yake, mapendeleo yake na kupinga mengine yote.
Hafanyi utafiti wala kufikiri au kufanya uchambuzi, kwa sababu haamini akili wala dini; hakuna kitu isipokuwa kilicho kwenye rai yake na mapendeleo yake.
Mtu wa aina hii anaangalia nafsi zake kuwa ndio kipimo pekee cha haki heri na usawa, na kwamba yeye siku zote yuko sawa, hana upungufu wala hakosei.
Huyu tunaweza kumwita shahidi wa upumbavu na mwenye ghururi ya kuua. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemwashiria mtu huyu, katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: “Sema je, tuwaambie wale wenye hasara mno ya vitendo?” Juz. 16 (18:103) Nyingine ni:
وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ قَالُوا إِنَّمَا نَحْنُ مُصْلِحُونَ {11}
أَلَا إِنَّهُمْ هُمُ الْمُفْسِدُونَ وَلَٰكِنْ لَا يَشْعُرُونَ {12}
Basi Hakika Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye na humwongoa amtakaye.
Hii ni sababu ya kauli yake Mwenyezi Mungu iliyotangulia ‘Je, yule aliyepambiwa ubaya wa tendo lake akaliona ni jema.’ Yaani kwamba Mwenyezi Mungu amemuweka kwenye upotevu na mwisho mbaya kwa sababu amefuata njia inayopelekea hilo; sawa na alivyomuweka kwenye kifo mwenye kunywa sumu na kufa maji aliyejitia baharini akiwa hajui kuogelea.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:27) na Juz. 14 (16:93).
Basi roho yako isitoke kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya.
Usisikitike wala usihuzunike, ewe Muhammad, kwa wale ambao hawakuitikia mwito wako madamu wamefuata wenyewe njia ya uovu na ya maangamizi. Mwenyezi Mungu ameyadhibiti mambo yao, madogo na makubwa. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (18:2).
وَاللَّهُ الَّذِي أَرْسَلَ الرِّيَاحَ فَتُثِيرُ سَحَابًا فَسُقْنَاهُ إِلَىٰ بَلَدٍ مَيِّتٍ فَأَحْيَيْنَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا ۚ كَذَٰلِكَ النُّشُورُ {9}
مَنْ كَانَ يُرِيدُ الْعِزَّةَ فَلِلَّهِ الْعِزَّةُ جَمِيعًا ۚ إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ ۚ وَالَّذِينَ يَمْكُرُونَ السَّيِّئَاتِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۖ وَمَكْرُ أُولَٰئِكَ هُوَ يَبُورُ {10}
وَاللَّهُ خَلَقَكُمْ مِنْ تُرَابٍ ثُمَّ مِنْ نُطْفَةٍ ثُمَّ جَعَلَكُمْ أَزْوَاجًا ۚ وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنْثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ ۚ وَمَا يُعَمَّرُ مِنْ مُعَمَّرٍ وَلَا يُنْقَصُ مِنْ عُمُرِهِ إِلَّا فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرٌ {11}