read

Aya 9 – 11: Amali Njema Huipandisha

Maana

Na Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma pepo ziyatimue mawingu, nasi tukayafikisha kwenye nchi iliyokufa, tukaifufua ardhi baada ya kufa kwake. Ndio kama hivyo kufufuliwa.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:57).

Mwenye kutaka enzi basi enzi yote ni ya Mwenyezi Mungu.

Enzi ni ya Mwenyezi Mungu na ya dini ya Mwenyezi Mungu hasa; na kwa mawili hayo ndio binadamu anakuwa na enzi. Mwenye kujienzi kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu atadhalilika. Ibn Arabi katika kitabu Futuhatul-Makkiyya, anasema:

“Enzi ya haki hasa ni kuwa hakuna Mola ila Yeye, na enzi ya Mtume wake ni kwa Mwenyezi Mungu, na enzi ya waumini ni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi yanathibiti kwenye tanzu yale yaliyonayothibiti kwenye asili.”

Kudhalilika kwa waislamu leo kumetokana na kuwa wao wanajienzi kwa usiokuwa Uislamu. Hapo mwanzo walikuwa ni wachache kuliko sasa, lakini walikuwa ni wengi kwa kujienzi na jamii na umoja wao dhidi ya adui wa Mwenyezi Mungu na adui wao.

Kwake hupanda neno zuri na amali njema huiinua.

Kupanda maneno na kuinuka matendo kwenda kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kinaya cha kuyakubali na kuyalipa thawabu. Maneno mazuri ni yale yanayonufaisha, na vile vile amali njema.
Aya inaashiria kwamba sababu ya kuenziwa na kutukuzwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kauli na vitendo vinavyowanufaisha watu.

Na wanaopanga njama za maovu watapata adhabu kali, na njama za hao zitaangamia.

Kupanga njama za maovu ni kupanga kuwaudhi waumini na viongozi wema. Lakini njama zao zitaambulia patupu. Maana ya Aya hii ni kama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Na vitimbi viovu havimpati ila mwenyewe.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:5).

Kisha akawafanya aina kwa aina, mweusi na mweupe na mume na mke. Na mwanamke yeyote hachukui mimba wala hazai, ila kwa elimu yake, kwa sababu yeye amekizunguka kila kitu.

Wala hapewi umri mwenye umri mrefu wala hapunguziwi umri wake, ila yamo katika Kitabu. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

Kupunguziwa umri ni kuwa na umri mfupi; na kuwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni kuwa katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu. Maana kwa ujumla ni kuwa umri wote uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Katika Nahjul-Balagha imeelezwa:

“Hampati neema katika dunia ila ni kwa kuimaliza nyingine; wala hapati umri mwenye umri miongoni mwenu ila ni kwa kuumaliza mwingine.” Tazama Juz. 4 (3:144 – 148) kifungu cha ‘Ajalihainakinga’

وَمَا يَسْتَوِي الْبَحْرَانِ هَٰذَا عَذْبٌ فُرَاتٌ سَائِغٌ شَرَابُهُ وَهَٰذَا مِلْحٌ أُجَاجٌ ۖ وَمِنْ كُلٍّ تَأْكُلُونَ لَحْمًا طَرِيًّا وَتَسْتَخْرِجُونَ حِلْيَةً تَلْبَسُونَهَا ۖ وَتَرَى الْفُلْكَ فِيهِ مَوَاخِرَ لِتَبْتَغُوا مِنْ فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ {12}

Na bahari mbili haziwi sawa; hii ni tamu mno, kinywaji chake kinateremka uzuri, na hii ni chumvi sana. Na kutokana na zote, mnakula nyama freshi. Na mnatoa humo mapambo mnayoyavaa. Na unaona vyombo vikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake na mpate kushukuru.

يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُسَمًّى ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِنْ دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِنْ قِطْمِيرٍ {13}

Anauingiza usiku katika mchana na anauingiza mchana katika usiku. Na amelitiisha Jua na Mwezi, kila kimoja kinaendelea mpaka muda uliotajwa. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu, ufalme ni wake. Na wale mnaowaomba badala yake hawamiliki hata utando wa kokwa ya tende.

إِنْ تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ {14}

Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu. Na wakisikia hawajibu. Na siku ya Kiyama watakataa shirki yenu. Na hapana atakayekuambia kama Yeye mwenye habari.

يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنْتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّهِ ۖ وَاللَّهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ {15}

Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.

إِنْ يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ وَيَأْتِ بِخَلْقٍ جَدِيدٍ {16}

Akitaka atawaondoa na alete viumbe wapya.

وَمَا ذَٰلِكَ عَلَى اللَّهِ بِعَزِيزٍ {17}

Na hilo kwa Mwenyezi Mungu si gumu.

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ وَإِنْ تَدْعُ مُثْقَلَةٌ إِلَىٰ حِمْلِهَا لَا يُحْمَلْ مِنْهُ شَيْءٌ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۗ إِنَّمَا تُنْذِرُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ بِالْغَيْبِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ ۚ وَمَنْ تَزَكَّىٰ فَإِنَّمَا يَتَزَكَّىٰ لِنَفْسِهِ ۚ وَإِلَى اللَّهِ الْمَصِيرُ {18}

Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine. Na kama aliyelemewa akiomba achukuliwe mzigo wake, hautachukuliwa hata kidogo, ingawa ana ujamaa. Hakika unawaonya wale tu wanaomcha Mola wao kwa ghaibu na wakasimamisha Swala. Na anayejitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.