Aya 19 – 28: Hawi Sawa Kipofu Na Mwenye Kuona
Maana
Hawi sawa kipofu na mwenye kuona, wala giza na nuru, wala kivuli na joto. Na hawawi sawa walio hai na walio maiti.
Makusudio ya kipofu ni yule mwenye kuacha njia ya haki na ya uongofu; kinyume chake ni mwenye kuona. Giza ni ujinga na upotevu, na nuru ni elimu na uongofu. Kivuli ni neema na joto ni moto wa Jahannam. Ama walio hai ni wale walio na nyoyo zinazosikia mazuri na zikayafuata; kinyume chao ni wafu.
Maana ni kuwa hawi sawa, mbele ya Mwenyezi Mungu na kihali halisi ilivyo, mwenye kuamini akafanya matendo mema na yule mwenye kukufuru akafanya ufisadi. Bali tofauti baina yao ni sawa na tofauti baina ya kipofu na mwenye macho, mwanga na giza, kivuli na joto na mauti na uhai.
Hakika Mwenyezi Mungu humsikilizisha amtakaye. Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio makaburini. Hukuwa wewe ila ni mwonyaji.
Maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu yanaathiri na kufanya kazi katika nafsi za wale wanaotafuta haki kwa ajili ya haki na kuisikiliza kwa ajili ya kutaka kuifanyia kazi.
Ama wale ambao hakuna linalowashtua isipokuwa masilahi yao wala hawafanyi lolote isipokuwa masilahi, wao hawasikilizi maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, wala Yeye, ambaye imetukuka hekima yake, hawasukumi kwenye uongofu. Vinginevyo zitabatilika thawabu na adhabu.
Hakika sisi tumekutuma kwa haki, uwe mbashiri na mwonyaji.
Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad (s.a.w.), kwa hoja za kutosheleza, kulingania kwenye haki na kuwa shahidi kwa viumbe. Basi akafikisha ujumbe kwa ukamilifu na akawa ni rehema kwa viumbe wote, hasa waarabu; pale alipowatoa kwenye ujinga wa wajinga na kuwapeleka kwenye nuru ya Uislamu na karama yake.
Imetangulia neno kwa neno katika Juz. 11 (10:42) na Juz.20 (27:80).
Kila Umma Una Mtume
Na hakuna uma wowote ila alipita humo muonyaji.
Katika Qur’an kuna Aya zinazofahamisha waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametuma Mtume kwa kila umma; miongoni mwa Aya hizo ni hizi zifuatazo:
Aya hii tuliyo nayo.
فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِنْ كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ {41}
وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَسُولًا {36}
وَلِكُلِّ أُمَّةٍ رَسُولٌ ۖ{47}
Kuongezea kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ {92}
Na pia kauli yake:
أَيَحْسَبُ الْإِنْسَانُ أَنْ يُتْرَكَ سُدًى {36}
Sio mbali kuwa makusudio ya mjumbe, muonyaji na shahidi ni kila linalosimamia hoja na kukata nyudhuru, liwe limetoka kwa Nabii, Mtume, Kitabu cha dini, kiongozi mwema au hukumu ya akili ya kimsingi, isiyopingika na wenye akili salama na umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu; kama ubaya wa dhulma na hiyana, na uzuri wa uadilifu na uaminifu n.k. Wala hatujui umma ulioishi kwa vurugu bila nidhamu na kumwachia kila mtu afanye atakavyo bila ya kumhisabu kwa kauli na vitendo.
Unaweza kuuliza: Je, hii haipingani na kauli yake Mwenyezi Mungu, iliyo katika Juzuu hii: “Wala hatukuwatumia muonyaji kabla yako.” (34:44). Ambapo Aya tuliyo nayo inathibitisha kuwa kila kaumu ina muonyaji na ya pili inakataa kuwa kaumu ya Muhammad (s.a.w.) ilikuwa na muonyaji kabla yake?
Jibu: Muonyaji katika Aya tuliyo nayo inachanganya kila muonyaji awe mtume au la. Ama katika Aya ya pili inahusuiana na Mtume. Kwa hiyo hakuna kupingana baina ya Aya mbili na maana ni kuwa kaumu ya Muhammad (s.a.w.) hawakujiwa na Mtume kabla ya kutumwa yeye, lakini walijiwa na muonyaji wa akili na maumbile; nayo ni muonyaji tosha wa kuwapa hoja; hasa katika kuabudu kwao mawe.
Ndio maana Mtume (s.a.w.) alikuwa akiwajadili kwa mantiki ya akili na kuwaambia:
قُلْ أَتَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ مَا لَا يَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا ۚ وَاللَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ {76}
Na kama wakikukadhibisha, basi hakika wamekadhibisha wale waliokuwa kabla yako. Waliwajia Mitume wao kwa dalili wazi wazi na kwa maandiko na kwa kitabu chenye nuru.
Makusudio ya maandiko hapa ni hikima na mawaidha. Kitabu chenye nuru ni Tawrat iliyoteremshwa kwa Musa, Injil iliyoteremshwa kwa Isa na vitabu vinginevyo vilivyotermshwa kabla ya Mtume wa mwisho. Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:184).
Kisha nikawakamata wale waliokufuru; basi je, kulikuwaje kukanya kwangu?
Makusudio ya kukanya hapa ni adhabu. Yaani Mwenyezi Mungu aliwakanya kwa kauli na vitendo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:44) na Juzuu hii tuliyo nayo (34:45).
Je, huoni kuwa tumeteremsha kutoka mawinguni maji kutoka mbinguni na kwayo tumetoa matunda yenye kuhitalifiana rangi na ladha yake na harufu yake.
Hakuna mwenye shaka kwamba kutoafautiana huku kunatokana na sababu za kimaumbile, lakini zote hizi zinaishia kwa muumba wa hayo maumbile. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:4) katika kifungu cha ‘Sayyid Afghani na wanaomkana Mungu.’
Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbalimbali na myeusi.
Anasema, mkuu wa wasemaji, kwamba Yeye amefanya kwenye majabali njia; kuna nyeupe, nyekundu na nyingine ni nyeusi. Kila moja katika njia hizo tatu inatofautiana rangi.
Mazingatio katika kutofautiana huku ni kufahamisha juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu na matakwa yake; sawa na tofauti ya matunda.
Na katika watu na wanyama na wanyama howa pia rangi zao zinahitalifiana.
Kuunganisha wanyama na wanyama hoa, ni katika kuunganisha maalum kwenye ujumla, kwa sababu neno lililotumika kwa wanyama, Dawab, lina maana ya wanaotemebea ardhini, wakiwemo wanyama howa (mifugo) ambao ni ngamia, ng’ombe, kondoo na mbuzi.
Maana ni kuwa kutofautiana rangi za watu na kutofautiana wanyama, kunafahamisha uweza wa Mwenyezi Mungu; sawa na kutofautiana matunda na njia.
Hakika si mwengineyo wanaomcha Mwenyezi Mungu, katika waja wake ni wale wajuzi.
Makusudio ya wenye ujuzi hapa ni wale walioamini kwa kujua, sio kwa kuiga, na wakaujua utukufu wake kwa dalili na hoja.
Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kujua uweza wa asiyeshindwa na kitu wala kupitwa na kitu, hawezi kuacha kumuogopa; ndio maana wanaomjua Mwenyezi Mungu ndio wanaohofia zaidi hasira za Mwenyezi Mungu na ndio walio na matarajio zaidi ya fadhila na msamaha wake.
Sisi ni katika wale wanaoamini kuwa hakuna imani ya kweli bila ya takua wala hakuna takua bila ya mwamko. Ndio maana Mtume mtukufu (s.a.w.) akasema: “Ubora wa mjuzi juu ya mwenye kuabudu ni ubora wa mwezi usiku kwenye nyota.” Pia kuna Hadith mashuhuri ya Mtume (s.a.w.): “Usingizi wa mwenye ujuzi ni bora kuliko ibada ya mjinga.”
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye maghufira.
Mwenye nguvu katika kuwawaadhibu wenye kupituka mipaka na kufanya dhulma, na ni mwenye maghufira kwa mwenye kutubia na kurejea.
إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنْفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَنْ تَبُورَ {29}
لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُمْ مِنْ فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ {30}
وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ هُوَ الْحَقُّ مُصَدِّقًا لِمَا بَيْنَ يَدَيْهِ ۗ إِنَّ اللَّهَ بِعِبَادِهِ لَخَبِيرٌ بَصِيرٌ {31}
ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِنَفْسِهِ وَمِنْهُمْ مُقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ {32}
جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِنْ ذَهَبٍ وَلُؤْلُؤًا ۖ وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ {33}
وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي أَذْهَبَ عَنَّا الْحَزَنَ ۖ إِنَّ رَبَّنَا لَغَفُورٌ شَكُورٌ {34}
الَّذِي أَحَلَّنَا دَارَ الْمُقَامَةِ مِنْ فَضْلِهِ لَا يَمَسُّنَا فِيهَا نَصَبٌ وَلَا يَمَسُّنَا فِيهَا لُغُوبٌ {35}