Aya 40 – 43: Anazizuia Mbingu Na Ardhi
Maana
Katika Aya hii ya kwanza hapa, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewapa hoja tatu washirikina:
Sema mnaona hawa washirika wenu mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, nionyesheni wameumba nini katika ardhi?
Niambieni enyi washirikina! Ni jambo gani lililowafanya mumfanye Mwenyezi Mungu ana washirika? Je, ardhini kuna kitu chochote kinachofahamisha kuwa kimetengenezwa na wengi? Hapana! Vitu vyote vina- julisha kuweko Mungu mmoja tu, na mpangilio wake ni ushahidi wa utukufu wake na hekima yake.
Au wana ushirika wowote katika mbingu?
Yaani hao mnaowaabudu wana athari yoyote mbinguni kujulisha kuwa wao ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika kuumba?
Au tumewapa Kitabu, nao kwa hicho, wakawa na hoja.
Tuliowapa ni hao washirikina sio washirika wanaoabudiwa. Maana ni kuwa au mumewafanya washirika wa Mungu hao mnaowabudu kwa kutegemea Kitabu kilichoteremshwa au Nabii aliyetumwa? Kwa ujumla ni kuwa hakuna hoja yoyote ya kiakili na kinakili kwa wanavyovishirikisha; bali wao wanamangamanga tu.
Lakini madhalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu.
Makusudio ya udanganyifu hapa ni ubatilifu. Viongozi wa washirikina walikuwa wakiwaambi wafuasi wao kuwa masanamu yatawaombea kesho. Hakuna mwenye shaka kuwa ahadi hii ni uwongo, uzushi na ubatilifu.
Kwa hakika Mwenyezi Mungu huzuia mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka hapana yeyote wa kuzizuia isipokuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole, Mwingi wa maghufira.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amezizuwia sayari kwa nguvu ya mvutano; sawa na anavyowazuia ndege angani kwa mbawa zao. Mwenyezi Mungu ametegemeza kwake, kwa sababu yeye ni muumba wa ulimwengu na msababishi wa sababu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:65).
Na waliapa kwa ukomo wa kuapa kwao, kwamba akiwafikia mwonyaji bila ya shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote.
Walioapa ni washirikina. Katika Bahrul-Muhit imesemwa kuwa watakuwa waongofu ambao hawana mfano. Makuraishi walikuwa wakiwapinga Mayahudi kwa kupotoka kwao na dini yao na kuwaua mitume wao. Wakaapa viapo vya nguvu kwamba akiwajia Mtume kutoka kwa kwa Mwenyezi Mungu watakuwa watiifu zaidi.
Lakini alipowajia muonyaji hakuwazidishia ila kukimbia kwa kutak- abari kwao katika ardhi na kufanya vitimbi viovu.
Hatimaye mjumbe wa Mwenyezi Mungu aliwajia na hoja na ubainifu, lakini wao walimkadhibisha na wakamkimbia na wakamfanyia kiburi yeye na mwito wake. Vile vile walimfanyia vitimbi yeye na wafuasi wake na wakawazuia watu kuamini utume wake. Hata hivyo mwisho walishindwa na wakasalimu amri wakiwa dhalili na wanyonge.
Na vitimbi viovu havimpati ila mwenyewe.
Vitimbi viovu ni kumdhamiria ubaya ndugu yako na kumpangia njama, bila ya yeye kujua, ili atumbukie. Hata hivyo, akiwa hajui yaliyodhamiri- wa na kupangwa, basi Mwenyezi Mungu anajua na atamlipa mpanga njama malipo ya muongo mwenye hadaa na balaa litamrudia yeye.
Basi hawangoji ila desturi ya wa zamani. Hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu, wala hutapata mageuzi katika desturi ya Mwenyezi Mungu.
Desturi ya wa zamani ni desturi ya Mwenyezi Mungu kwa watu wa zamani ambayo ni kuangamia waliowakadhibisha mitume wa Mwenyezi Mungu. Maana ni je, hawajui wanaomkadhibisha Mtume wetu Muhammad, kwamba Mwenyezi Mungu aliangamiza kaumu ya Nuh, A’ad, Thamud na mfano wao waliowakadhibisha mitume? Na kwamba hii ni desturi yake Mwenyezi Mungu isiyobadilika wala kugeuka? Je, hawapati funzo kwa wengine?
أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنْظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ وَكَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً ۚ وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُعْجِزَهُ مِنْ شَيْءٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ ۚ إِنَّهُ كَانَ عَلِيمًا قَدِيرًا {44}
وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِنْ دَابَّةٍ وَلَٰكِنْ يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُسَمًّى ۖ فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَإِنَّ اللَّهَ كَانَ بِعِبَادِهِ بَصِيرًا {45}