read

Aya 1 – 12: Wewe Ni Katika Mitume

Maana

Yasin

Wafasiri wengi wamesema kuwa tamko hili lina maana kama mianzo mingine ya Sura yenye herufi za mkato; kama ilivyo katika Juz.1 (2:1). Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: “Amani kwa Ilyasin” (37:130), makusudio yake ni Ilyas.

Naapa kwa Qur’an yenye hekima. Hakika wewe bila shaka ni miongoni mwa waliotumwa juu ya njia iliyonyooka.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameapa, kwa Qur’an yenye hekima, kwamba Muhammad (s.a.w.) yuko kwenye dini ya ya sawasawa. Kuapa kwa Mwenyezi Mungu kwa Qur’an pamoja na kuisifu kuwa ina hekima, kunaashiria kwenye utukufu wa Qur’an na ukuu wake na kwamba ni dalili yenye nguvu zaidi juu ya ukweli wa Muhammad (s.a.w.) katika mwito wake.

Ama kujisifu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa nguvu na rehema, katika kauli yake:

Ni uteremsho wa Mwenye nguvu Mwenye kurehemu, ni ishara kuwa anawachukulia waasi kwa namna ya Mwenye uwezo na anawahurumia waumini na wenye kutubia. Imam Ali (a.s.) anasema: “Ghadhabu haimshughulishi (asiwe) na rehema, wala rehema haimshughulishi (asiwe) na mateso.”

Mdundo Wa Ndani Katika Qur’an

Mnamo mwaka 1959 Mustafa Mahmud, Mmisri, alitunga kitabu Allahu wal-insan (Mungu na mtu). Katika kitabu hicho alikana Mungu na ufufuo, nami nikamjibu kwa kutunga kitabu Allahu wal-Aqli (Mungu na Akili).

Kisha nikafuatilia makala zake na tungo zake. Nikasoma makala yake katika jarida linaloitwa Ruzil-yusf la tarehe 10-4-1967 akikiri kuweko ufufuo. Hayo nimeyaashiria katika Juz. 1 (2:28 – 29) kifungu cha ‘Ufufuo.’

Mustafa Mahmud ni mwana fasihi, mwenye akili inayogundua undani na siri za lugha. Ushahidi wa hayo ni aliyoyaandika kuhusu Qur’an katika jarida la Sabahul-khayr la tarehe 1-1-1970 kwa anuani ya “Usanifu wa Qur’an” Tunadokoa machache katika makala hiyo, kama yafuatavyo:

“Sijui niseme nini kuelezea hisia niliyoipata katika ibara ya kwanza ya Qur’an... Basi matamshi yake yalikuwa yakiingia kwenye nafsi yangu, kama kwamba ni kiumbe hai chenye maisha ya aina ya peke yake... Nikagundua simulizi za mdundo wa kindani katika ibara za Qur’an ... Hii ni siri ya ndani sana katika mpangilio wa Qur’an...

Yenyewe sio mashairi wala nathari au lugha ya mjazo; isipokuwa ni ubainifu maalum wa maneno yaliyoundwa kwa njia inayogundua mdundo wa kindani. Mdundo uliozoeleka unakuja kutoka nje na kufika masikioni, na sio ndani bali unatokana na mahadhi, wizani na kina.

Mdundo wa Qur’an hauna wizani wala kina au mahadhi, lakini pamoja na hayo, unashuka kwa kila herufi yake... kutoka wapi na vipi, hiyo ndiyo siri katika siri za Qur’an zisizofanana na mfumo wowote wa kifasihi. Inashangaza na wala hatuwezi kuujua mfumo wake. Ni mfumo wa kipekee haujapatakina katika kila kilichoandikwa kwa lugha ya kiarabu ya zamani na ya sasa. Haiwezekani kuuiga mfumo huu.”

Ndio haiwezekani kuuiga. Na hapa ndio inapatikana siri ya muujiza wa Qur’an. Baada ya mwandishi huyu kuleta ushahidi mwingi wa hakika hii katika maneno ya Mwenyezi Mungu na Aya zake, aliendelea kusema:

“Na sio mdundo wa kindani tu ndio kitu cha aina yake katika Qur’an, bali kuna sifa nyingine inayokutambulisha kuwa hii ni sanaa ya muumba sio ya muumbwa... Hebu isikilize Qur’an ikisifia mfungamano wa maingiliano ya kijinsia baina ya mume na mke, kwa tamako laini na la heshima, jambo ambalo huwezi kulipata kwenye lugha yoyote: “Alipomkurubia1 alishika mimba nyepesi.” Juz. 9 (7:189).

Tamko hili taghashaha alimfunika (kwa maana ya kumkurubia) linamchanganya mume na mke kama vinavyochanganyika vivuli viwili au kama rangi inavyofunika rangi nyingine. Tamko hili la ajabu linalofahamisha muingiliano mkamilifu wa mume na mke, ni ukomo wa ibara.

Hakika Qur’an ina hali ya kipekee na ya ajabu, inayoleta unyenyekevu katika nafsi na kuathiri moyo, pale tu matamshi yake yanapogusa masikio, kabla ya akili kuanza kuyafanyia kazi. Na ikianza kufanya uchambuzi na kutaamali, inagundua vitu vipya vinavyomzidisha unyenyekevu. Lakini hii ni hatua ya pili; inaweza kutokea na isitokee, inaweza kugundua siri za Aya na inaweza isigundue, na inaweza kuleta busara au isilete, lakini unyenyekevu upo.”

Hii nayo ni aina mojawapo ya muujiza wa Qur’an. Mwandishi huyu wa kitabu Allahu wal insan alimaliza makala yake ndefu kwa kusema: “Hakika Qur’an ni matamshi na maana kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye amekizunguuka kila kitu kwa ujuzi.”

Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa, basi ni wenye kughafilika.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja kuwa Muhammad (s.a.w.) ni Mtume wa haki na kwamba Qur’an imetoka kwake, sasa anabainisha umuhimu wa Qur’an kuwa inakataza aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, kwenye masikio ya waarabu, walioghafilika na Mwenyezi Mungu na haki, bila ya kufikiwa na muonyaji kabla ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.).

Huko nyuma kwenye Juzuu hii, kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na hakuna uma wowote ila alipita humo muonyaji (35:24),” tumesema kuwa makusudio ya muonyaji hapo ni kila linalosimamia hoja, iwe ni akili au nakili na kwamba makusudio ya muonyaji kwenye Aya hii tuliyo nayo ni Mtume hasa.

Imekwishathibiti kauli juu ya wengi wao, kwa hiyo hawaamini.

Makusudio ya kauli hapa ni kiaga cha adhabu, na wengi wao ni hao maba- ba zao; yaani mababa za waarabu waliokuwa wakati wa Muhammad (s.a.w.), waliokufa kwenye ushirikina. Ni wachache sana waliokuwa kwenye dini ya Tawhid. Tazama Juz. 15 (17:105–111) kifungu ‘Wanyoofu.’

Hakika tumeweka minyororo shingoni mwao, nayo inafika videvuni, kwa hiyo vichwa vyao viko juu.

Mikono ikifungwa kwa minyororo mpaka shingoni kichwa huinuka juu, na aliyefungwa anakuwa hawezi kugeuka kuume wala kushoto au kuangalia mbele; atakuwa anaangalia juu tu.

Na tumeweka kizuizi mbele yao na kizuizi nyuma yao na tumewafunika, kwa hiyo hawaoni.

Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atawaweka kwenye vizuizi viwili vya moto. Kimoja mbele yao na kingine nyuma yao, hawawezi kwenda mbele wala kurudi nyuma; wala hawezi kuona mbingu, kwa sababu vizuizi viwili vimefunika macho yao.

Sio mbali kuwa hiki ni kinaya cha ukali na uchungu wa adhabu. Kwa vyovyote iwavyo, adhabu haihusiki na washirikina tu, bali itaenea kwa kila mwenye hatia na dhalimu.

Imam Ali (a.s.) anasema: “Ama watu wa maasia atawaweka mahali pa baya, atawafunga mikono kwa minyororo hadi videvuni, utosi utafungwa na nyayo, na atawavisha kanzu za lami na nguo za moto. Watu wake watafungiwa mlango katika Moto mkali wenye kuvuma.”

Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii (34:33).

Ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye hawataamini.

Ni sawa kwao ewe Muhammad, uwape mawawidha au usiwape, basi hakika wao, hawatafanya lolote isipokuwa kwa hawaa zao na masilahi yao. Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:6).

Hakika unamuonya yule tu anayefuata ukumbusho na akamcha Mwingi wa rehema kwa ghaibu. Basi mbashirie maghufira na ujira wa heshima.

Anayekusikiliza ni yule anayeitafuta haki kwa ajili ya haki na kwenda nayo kwa matokeo yoyote yatakayokuwa. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii (35: 18).

Hakika sisi tunawahuisha wafu na tunayaandika wanayoyatanguliza na athari zao. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari linalobainisha.

Daftari linalobainisha ni kinaya cha elimu ya Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa, Mwenyezi Mungu atawafufua, na ameyahifadhi wanayoyafanya ya kheri na ya shari na athari walizoziacha za manufaa au madhara, na kwamba Yeye atamlipa kila mmoja alilolifanya, nao hawatadhulumiwa.

وَاضْرِبْ لَهُمْ مَثَلًا أَصْحَابَ الْقَرْيَةِ إِذْ جَاءَهَا الْمُرْسَلُونَ {13}

Na wapigie mfano wenyeji wa mji Mitume walipowafikia.

إِذْ أَرْسَلْنَا إِلَيْهِمُ اثْنَيْنِ فَكَذَّبُوهُمَا فَعَزَّزْنَا بِثَالِثٍ فَقَالُوا إِنَّا إِلَيْكُمْ مُرْسَلُونَ {14}

Tulipowatuma wawili wakawakadhibisha. Basi tukawaongezea nguvu kwa (mwingine) wa tatu Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.

قَالُوا مَا أَنْتُمْ إِلَّا بَشَرٌ مِثْلُنَا وَمَا أَنْزَلَ الرَّحْمَٰنُ مِنْ شَيْءٍ إِنْ أَنْتُمْ إِلَّا تَكْذِبُونَ {15}

Wakasema nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na mwingi wa rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.

قَالُوا رَبُّنَا يَعْلَمُ إِنَّا إِلَيْكُمْ لَمُرْسَلُونَ {16}

Wakasema: Mola wetu anajua kwamba sisi tumetumwa kwenu.

وَمَا عَلَيْنَا إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ {17}

Wala si juu yetu ila kufikisha waziwazi.

قَالُوا إِنَّا تَطَيَّرْنَا بِكُمْ ۖ لَئِنْ لَمْ تَنْتَهُوا لَنَرْجُمَنَّكُمْ وَلَيَمَسَّنَّكُمْ مِنَّا عَذَابٌ أَلِيمٌ {18}

Wakasema: Hakika sisi tunapata mkosi kwa ajili yenu. Kama hamtakoma basi hakika tutawapiga mawe na itawafika adhabu chungu kutoka kwetu.

قَالُوا طَائِرُكُمْ مَعَكُمْ ۚ أَئِنْ ذُكِّرْتُمْ ۚ بَلْ أَنْتُمْ قَوْمٌ مُسْرِفُونَ {19}

Wakasema: Mkosi wenu mnao wenyewe. Je, ni kwa kuwa mnakumbushwa? Bali nyinyi ni watu mnaopituka mipaka.

وَجَاءَ مِنْ أَقْصَى الْمَدِينَةِ رَجُلٌ يَسْعَىٰ قَالَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُوا الْمُرْسَلِينَ {20}

Na akaja mtu mbio kutoka upande wa mbali wa mjini akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni Mitume.

اتَّبِعُوا مَنْ لَا يَسْأَلُكُمْ أَجْرًا وَهُمْ مُهْتَدُونَ {21}

Wafuateni wasiowaomba ujira nao wameongoka.
  • 1. Neno alipomkurubia limefasiriwa kimaana kutoka neno la kiarabu ‘taghashaha’ tarjuma yake ni alipomfunika. Kwa hiyo mwandishi hapa anasifia jinsi Qur’an ilivyotumia neno kufunika katika tendo la kuonana mume na mke – Mtarjumu