Aya 13 – 27; Wajumbe Wawilia Waliowaongezewa Nguvu Kwa Wa Tatu
وَمَا لِيَ لَا أَعْبُدُ الَّذِي فَطَرَنِي وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ {22}
أَأَتَّخِذُ مِنْ دُونِهِ آلِهَةً إِنْ يُرِدْنِ الرَّحْمَٰنُ بِضُرٍّ لَا تُغْنِ عَنِّي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا وَلَا يُنْقِذُونِ {23}
إِنِّي إِذًا لَفِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {24}
إِنِّي آمَنْتُ بِرَبِّكُمْ فَاسْمَعُونِ {25}
قِيلَ ادْخُلِ الْجَنَّةَ ۖ قَالَ يَا لَيْتَ قَوْمِي يَعْلَمُونَ {26}
بِمَا غَفَرَ لِي رَبِّي وَجَعَلَنِي مِنَ الْمُكْرَمِينَ {27}
Maelezo:
Tutaanza kufafanua Aya 13 na zinazofuatia zilizoishia kwenye juzuu iliyotangulia, kwa vile zinaungana na hapa.
Maana
Na wapigie mfano wenyeji wa mji Mitume walipowafikia.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume awaambie washirikina wa Kiarabu. Ama mji, wafasiri wengi wamesema ni Antiokia, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuelezea. Kwa sababu makusudio ya kupiga mfano ni kupata mawaidha na mazingatio, sio jina la mji na sehemu yake.
Dhana kubwa ni kuwa wafasiri wametegemea vitabu vya kinaswara; ambapo imeelezwa kwenye Matendo ya mitume 11: 19 – 26, kwamba Barnaba na Sauli walikwenda Antiokia na kuwafundisha watu wengi. Na kwamba mitume ni wanafunzi 12 aliowachagua Bwana Masih (a.s.) ili wamsaidie na wamwone atakapotoka kaburini, waelezee walimwengu; kama ilivyoelezwa kwenye Mathayo na Matendo ya mitume.
Barnaba alikuwa ni Mkupro (Cyprus) akaingia kwenye ukiristo katika zama za mitume na akawa ni mhubiri; kama ilivyoelezwa katika ‘Kamusi ya Kitabu kitakatifu’
Tulipowatuma wawili wakawakadhibisha. Basi tukawaongezea nguvu kwa (mwingine) wa tatu.
Katika tafsiri nyingi imeelezwa kuwa mitume walikuwa ni wanafunzi wa Isa (a.s.) na kwamba yeye ndiye aliyewatuma wawili mjini kisha akawaongezea nguvu kwa mwingine wa tatu.
Lakini neno mitume likitegemezwa kwa Mwenyezi Mungu, kama ilivyo katika neno ‘tulipowatuma’ na ‘tukawaongezea nguvu,’ huwa linafahamisha kuwa wao walitumwa kwa amri ya Mwenyezi Mungu moja kwa moja sio kwa kwa amri ya Isa (a.s.).
Vyovyote iwavyo, la kuzingatia ni utendaji si majina. Zaidi ya hayo sisi hatutaulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu, wala hilo halina uhusiano wowote na maisha yetu kwa karibu au mbali. Maana yaliyo wazi, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwatuma mitume watatu kwenye mji huo, watoe mwito wa haki.
Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu. Wakasema; nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na mwingi wa rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.
Hii ndio nembo ya wapinzani siku zote. Tazama Juz. 13 ( 14:10), Juz. 15 (17:94), Juz. 17 (21:3), Juz. 18 (23:24) na Juz. 19 (26:154).
Wakasema: Mola wetu anajua kwamba sisi tumetumwa kwenu. Wala si juu yetu ila kufikisha waziwazi.
Baada ya mitume kusimamisha hoja za kusadikisha ukweli wao, waliwaambia wakadhibishaji kuwa sisi tumetumwa kwenu na Mwenyezi Mungu, akatupa ubainifu, kama mnavyouona, na tumetekeleza ujumbe wake, kama inavyotakikana. Basi si juu yetu tena hisabu yenu wala si juu yenu nyinyi hisabu yetu. Yeye ni mjuzi mwenye kuhisabu.
Wakasema: Hakika sisi tunapata mkosi kwa ajili yenu. Kama hamtakoma basi hakika tutawapiga mawe na itawafika adhabu chungu kutoka kwetu. Wakasema: Mkosi wenu mnao wenyewe. Je, ni kwa kuwa mnakumbushwa? Bali nyinyi ni watu mnaopituka mipaka.
Mkosi wenu mnao wenyewe; yaani hakuna mkosi, bali hizo ni dhana zenu tu. Kuna Hadith mashuhuri isemayo: “Hakuna kuambukiza, wala mkosi wala nyuni” Imam As-Sadiq (a.s.) anasema: “Mkosi unaufanya wewe, ukiupuuza utakupuuza, ukiutilia mkazo utakutilia mkazo na ukiufanya si chochote nao hautakuwa ni chochote” Yaani hakuna kitu kama kisirani, ndege au mkosi; wala hauna athari yoyote kwa mtu; isipokuwa unaathiri nafsi ya mtu na mishipa yake, kwa vile anavyouwazia tu; kama mtoto anavyotishika na zimwi.
Maana ni kuwa wakadhibishaji waliwaambia mitume kuwa mmetuletea mkosi, kwa hiyo tunahofia tutagawanyika; sasa bora mnyamaze, la sivyo tutawanyamazisha kwa kuwapiga mawe na adhabu kali. Ndio Mitume wakawaambia, chimbuko la hofu ya mkosi linatokana na wasiwasi wenu nyinyi wenyewe, kwamba mwito wetu ni mkosi na shari; na hali yakuwa shari inatoka kwenu kwa kufanya shirki, ujahili na ufisadi.
Na akaja mtu mbio kutoka upande wa mbali wa mjini.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuashiria jina la mtu huyu, lakini wafasiri wengi wakasema jina lake ni Habib An-Najar, na kwamba nyumba yake ilikuwa kandoni mwa mji. Alikuwa mumin. Aliposikia kuwa watu wake wanaazimia kuwaua mitume, alifanya haraka kuja kuwaokoa na kuwasaidia.
Sijui wafasiri wamelitoa wapi jina hili. Mimi nimetafuta mpaka katika Biblia ukurasa wa yaliyomo na kamusi ya Kitabu kitakatifu pia sikulipata.
Vyovyote iwavyo, jina la huyo mtu halina mfungamano wowote na sisi. Wala hakuna linalotushughulisha isipokuwa lile lililofahamishwa na Aya. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemsifu kuwa na imani na wema, kwa sababu alisema:
Enyi watu wangu! Wafuateni Mitume. Wafuateni wasiowaomba ujira nao wameongoka.
Aliwapa nasaha watu wake wakubali mwito wa Mitume wala wasiwapinge, kwa sababu ni kwa masilahi yao. Wanatoa mwito na hawataki malipo wala shukrani; wala uluwa au ufisadi katika ardhi.
Na kwa nini nisimwabudu yule aliyeniumba na kwake mtarejeshwa?
Kauli hii ni ya yule mumin anayetoa nasaha. Maana yake ni kuwa, ni kizuizi gani kitakachonizuia na ibada ya ambaye amenifanya niweko baada ya kutokuweko, kisha atatufufua sote baada ya mauti kwa ajili ya hisabu na malipo?
Hapa anawapinga watu wake walioacha ibada ya Mungu mmoja wa pekee. Anaendelea kuwagonga na kusema:
Je, nishike miungu mingine badala yake? Mwingi wa rehema akinitakia madhara, uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa. Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotofu ulio dhahiri.
Vipi niabaudu masanamu yasiyodhuru wala kunufaisha? Hayaokoi wala hayaombei? Nikifanya hivyo nitakuwa nimepotea, wala sitakuwa katika walioongoka. Hapana!
Hakika mimi nimemwamini Mola wenu, basi nisikilizeni.
Hawi jasiri wa maneno haya isipokuwa yule asiyeogopa mauti katika njia ya haki na kuinusuru. Kuna mapokezi yanayoeleza kuwa alipowajia watu wake na hakika hii, walimuua kwa kumpiga mawe na hakupata wa kumhami. Hili haliko mbali kulingana na sera ya mataghuti na wafisadi. Linalotia nguvu ukweli wa risala hii ni ile kauli ya washirikina kwa mitume: “Kama hamtakoma basi hakika tutawapiga mawe na itawafika adhabu chungu kutoka kwetu.”
Katika Tafsiri ya Zamakhshari na Tha’labi imesemwa: Watangulizi wa umma ni watatu, hawakukufuru hata kwa kupepesa jicho: Ali bin Abu Twalib, Mtu wa Yasin na Mumin wa watu wa Firauni.
Ikasemwa: Ingia Peponi!
Aliiuza nafsi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na thamani ya bei yake ikawa ni Pepo. Hiyo ni tosha kuwa ni thawabu na malipo.
Akasema: Laiti watu wangu wangejua jinsi Mola wangu alivyonighufiria na akanifanya katika waheshimiwa.
Hakusema hivi kwa kuwacheka watu, ingawaje walimkadhibisha, hapana! Watu wema hawawi hivi; bali alisema hivi kuwasikitikia na yaliyowapita, akitamani lau wangelijua kwamba yeye alikuwa akiwapa nasaha na kwamba zilikuwa ni njozi na ujinga kuwa yeye na mitume wana mikosi.
وَمَا أَنْزَلْنَا عَلَىٰ قَوْمِهِ مِنْ بَعْدِهِ مِنْ جُنْدٍ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا كُنَّا مُنْزِلِينَ {28}
إِنْ كَانَتْ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً فَإِذَا هُمْ خَامِدُونَ {29}
يَا حَسْرَةً عَلَى الْعِبَادِ ۚ مَا يَأْتِيهِمْ مِنْ رَسُولٍ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ {30}
أَلَمْ يَرَوْا كَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُمْ مِنَ الْقُرُونِ أَنَّهُمْ إِلَيْهِمْ لَا يَرْجِعُونَ {31}
وَإِنْ كُلٌّ لَمَّا جَمِيعٌ لَدَيْنَا مُحْضَرُونَ {32}
وَآيَةٌ لَهُمُ الْأَرْضُ الْمَيْتَةُ أَحْيَيْنَاهَا وَأَخْرَجْنَا مِنْهَا حَبًّا فَمِنْهُ يَأْكُلُونَ {33}
وَجَعَلْنَا فِيهَا جَنَّاتٍ مِنْ نَخِيلٍ وَأَعْنَابٍ وَفَجَّرْنَا فِيهَا مِنَ الْعُيُونِ {34}
لِيَأْكُلُوا مِنْ ثَمَرِهِ وَمَا عَمِلَتْهُ أَيْدِيهِمْ ۖ أَفَلَا يَشْكُرُونَ {35}
سُبْحَانَ الَّذِي خَلَقَ الْأَزْوَاجَ كُلَّهَا مِمَّا تُنْبِتُ الْأَرْضُ وَمِنْ أَنْفُسِهِمْ وَمِمَّا لَا يَعْلَمُونَ {36}