read

Aya 45 – 54: Ogopeni Yaliyo Mbele Yenu

Maana

Na wanapoambiwa: Ogopeni yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa.

Wanaoambiwa ni washirikina wa kiarabu. Makusudio ya yaliyo mbele yao ni kumuasi Mwenyezi Mungu na aliyoyaharamisha, na yaliyo nyuma yao ni adhabu ya hayo. Kwenye Nahjul-balagh imeelezwa: “Hakika Kiyama kimewazingira kwa nyuma yenu.” Maana ni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewakataza kumuasi Mwenyezi Mungu na akwahadharisha na adhabu yake wakimuasi. Akawapa bishara ya rehema yake na thawabu zake wakimtii, lakini waligeuka nyuma.

Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao ila wao huwa ni wenye kuipuuza.

Kila alipowajia Mtume na muujiza wa dhahiri au hoja iliyo wazi, walimkadhibisha kwa jeuri na inadi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 19 (26:5)

Na wanapoambiwa: Toeni katika aliyowapa Mwenyezi Mungu, waliokufuru huwaambia walioamini: Je! Tumlishe ambaye Mwenyezi Mungu angependa angelimlisha? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhahiri.

Wapenda anasa wana msingi na dini moja tu; kupupia utajiri wao na maslahi yao. Ndio mazungumzo yao na vitendo vyao. Wakiambiwa msifanye ufisadi, wanasema sisi ni watengenezaji. Wakiambiwa aminini kama walivyoamini watu, wanasema: Tuamini kama walivyoamini wapumbavu? Wakiambiwa msujudieni Mwingi wa rehema, wanasema: Ni nani huyo Mwingi wa rehema? Sisi tunasujudia pesa.

Na wakiamriwa kuwapatia wenye haja wanasema Mwenyezi Mungu amewahukumia kuwa mafukara na sisi tuwe matajiri. Hawajui au wamejitia kutojua kuwa ufukara unatokana na yanayofanywa ardhini sio yanayofanywa mbinguni; kama vile ufisadi, serikali za kidhalimu, za unayanyasaji na uporaji.

Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?

Mwenyezi Mungu na Mtume anapowahadharisha na mwisho mbaya, wanasema kwa dharau yatakuwa lini haya? Umetangulia mfano wake kati- ka Aya kadhaa.

Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakaowachukua nao wanazozana.

Yaani wakizozania mambo ya dunia yao. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَأَخَذْنَاهُمْ بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ {95}

“Basi tuliwaachukua kwa ghafla hali hawatambui.” Juz. 9 (7:95).

Basi hawataweza kuusia, wala hawatarejea kwa watu wao.

Ukija ukelele wa adhabu hakuna yeyote atakayepata muda wa kuusia watu wake mambo muhimu, na akiwa mbali nao hataweza kurudi kwao.

Na itapulizwa Parapanda, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (18:99).

Watasema: Ole wetu! Nani aliyetufufua malaloni petu?

Watastaajabu kwa kufufuliwa kwao baada ya mauti, na hapo mwanzo walikuwa wakimfanyia mzaha yule anayewaandalia na kuwamarisha kujianda nao. Baada ya kushuhudia watasema: Haya ndiyo aliyoyaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume kwamba Kiyama kitafika tu, bila ya shaka yoyote na kwamba Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini.

Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu.

Kuumba, mauti na ufufuo kwa Mwenyezi Mungu ni sawa, kunakuwa kwa neno moja tu:

مَا خَلْقُكُمْ وَلَا بَعْثُكُمْ إِلَّا كَنَفْسٍ وَاحِدَةٍ ۗ {28}

“Hakukuwa kuumbwa kwenu wala kufufuliwa kwenu ila ni kama nafsi moja tu.” Juz. 21 (31:28)

Umetangulia mfano wake katika Aya 32 ya sura hii tuliyo nayo.

Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyokuwa mkiyatenda.

Kauli nyingine yenye maana haya ni:

الْيَوْمَ تُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۚ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ ۚ إِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ {17}

“Leo kila nafsi italipwa kwa iliyoyachuma. Hapana dhulma leo. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu” (40:17).

إِنَّ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ الْيَوْمَ فِي شُغُلٍ فَاكِهُونَ {55}

Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi.

هُمْ وَأَزْوَاجُهُمْ فِي ظِلَالٍ عَلَى الْأَرَائِكِ مُتَّكِئُونَ {56}

Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fahari.

لَهُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ وَلَهُمْ مَا يَدَّعُونَ {57}

Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakachokitaka.

سَلَامٌ قَوْلًا مِنْ رَبٍّ رَحِيمٍ {58}

Salaam! Ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mwenye kurehemu.

وَامْتَازُوا الْيَوْمَ أَيُّهَا الْمُجْرِمُونَ {59}

Na jitengeni leo enyi wakosefu.

أَلَمْ أَعْهَدْ إِلَيْكُمْ يَا بَنِي آدَمَ أَنْ لَا تَعْبُدُوا الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُبِينٌ {60}

Je, sikuagana nanyi, enyi wanadamu, kuwa msimuabudu Shet’ani? Hakika yeye ni adui dhahiri kwenu.

وَأَنِ اعْبُدُونِي ۚ هَٰذَا صِرَاطٌ مُسْتَقِيمٌ {61}

Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia iliyonyooka.

وَلَقَدْ أَضَلَّ مِنْكُمْ جِبِلًّا كَثِيرًا ۖ أَفَلَمْ تَكُونُوا تَعْقِلُونَ {62}

Na hakika yeye amewapoteza viumbe wengi miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkim- tia akili?

هَٰذِهِ جَهَنَّمُ الَّتِي كُنْتُمْ تُوعَدُونَ {63}

Hii ndiyo Jahannamu mliyokuwa mkiahidiwa.

اصْلَوْهَا الْيَوْمَ بِمَا كُنْتُمْ تَكْفُرُونَ {64}

Ingieni leo kwa vile mlivyokuwa mkikufuru.

الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَىٰ أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُمْ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ {65}

Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyokuwa wakiyachuma.

وَلَوْ نَشَاءُ لَطَمَسْنَا عَلَىٰ أَعْيُنِهِمْ فَاسْتَبَقُوا الصِّرَاطَ فَأَنَّىٰ يُبْصِرُونَ {66}

Na lau tungelipenda tungeliyafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wangeionaje?

وَلَوْ نَشَاءُ لَمَسَخْنَاهُمْ عَلَىٰ مَكَانَتِهِمْ فَمَا اسْتَطَاعُوا مُضِيًّا وَلَا يَرْجِعُونَ {67}

Na lau tungelitaka tungewageuza hapo hapo walipo, basi wasingeweza kwenda wala kurudi.

وَمَنْ نُعَمِّرْهُ نُنَكِّسْهُ فِي الْخَلْقِ ۖ أَفَلَا يَعْقِلُونَ {68}

Na tunayempa umri tunampindua katika umbo. Basi je! hawatii akilini?